Jan 16, 2017 11:50 UTC

Sura ya Al-A'nkabut, aya ya 62-66 (Darsa ya 715)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 715, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 29 ya Al-A'nkabut. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 62 ambayo inasema:

اللَّهُ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاء مِنْ عِبَادِهِ وَيَقْدِرُ لَهُ إِنَّ اللَّهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

Mwenyezi Mungu humkunjulia na humdhikishia riziki amtakaye katika waja wake. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

Katika darsa iliyopita tulieleza kwamba Waislamu walikuwa wakiudhiwa na kunyanyaswa na washirikina katika mji wa Makka na hata kwa miaka kadhaa wakawekewa vikwazo vya kiuchumi na ususiaji wa kibiashara na maadui hao wa dini ya Allah. Lakini pamoja na kukabiliwa na hali hiyo baadhi ya Waislamu hawakuwa tayari kuhajiri na kuacha nyumba, milki na mali zao. Katika aya tuliyosoma watu hao wanaambiwa msiache imani yenu kwa sababu ya kukosa njia za kupatia pato na kwa sababu ya kupatwa na matatizo ya maisha; bali kuweni imara na thabiti katika imani zenu na mjue kwamba riziki iko mikononi mwa Allah. Ikiwa itakulazimuni muhajiri, uacheni mji wenu muhajiri na kuhamia Madina. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kufanya jitihada na kujituma kwa ajili ya kujikimu kimaisha ni jukumu letu sisi. Lakini kuhusu kiwango cha pato na riziki tutakayopata, hilo haliko mikononi mwetu bali linahusiana na hekima yake Mola. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kutafautiana watu katika kiwango cha kipato na riziki pamoja na neema za kidunia, kama wanavyotafautiana wao wenyewe katika viwango vya akili, vipawa na uhodari ni jambo lenye hekima maalumu inayotokana na Mwenyezi Mungu mwenyewe. Tab'an kuwepo tofauti hizo ni jambo la lazima kwa jamii ya wanadamu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 63 na 64 ambazo zinasema:

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّن نَّزَّلَ مِنَ السَّمَاء مَاء فَأَحْيَا بِهِ الأَرْضَ مِن بَعْدِ مَوْتِهَا لَيَقُولُنَّ اللَّهُ قُلِ الْحَمْدُ لِلَّهِ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لا يَعْقِلُونَ

Na ukiwauliza: Ni nani aliye teremsha maji kutoka mbinguni, na akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake? Bila ya shaka watasema: Ni Mwenyezi Mungu. Sema: Alhamdu Lillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Bali wengi wao hawafahamu.

وَمَا هَذِهِ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلاَّ لَهْوٌ وَلَعِبٌ وَإِنَّ الدَّارَ الآخِرَةَ لَهِيَ الْحَيَوَانُ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ

Na haya maisha ya dunia si chochote ila ni pumbao na mchezo. Na nyumba ya Akhera ndiyo maisha khasa; laiti wangeli kuwa wanajua!

Kwa kuzingatia kwamba kuendelea maisha ya mwanadamu na upataji riziki yake vimefungamana na kunyesha mvua; kiasi kwamba ikiwa mvua haitonyesha kwa miaka kadhaa katika eneo lolote lile, kukosekana maji husababisha kutoweka miti, mimea na wanyama na kuzusha baa la njaa na ukame kwa watu aya tuliyosoma inasema: Hata washirikina wa Makka nao pia walikuwa wakiitakidi kwamba kunyesha mvua kuko kwenye mamlaka ya Allah SW, lakini pamoja na hayo wakawa wanaendelea kuyaabudu masanamu huku wakiamini kwamba yana taathira katika maisha yao. Kama washirikina walikuwa wakiukubali ukweli huo inakuwaje waumini wana hofu ya kupata riziki yao na wanakuwa hawako tayari kuhajiri katika njia ya Allah kwa kuchelea kukosa riziki? Kwani wao hawajui kama riziki na maisha ya kweli yako katika ulimwengu wa akhera na dunia yote hii ya mapambo na marembo ni mchezo na pumbao tu! Watoto wadogo huwa wanajipumbaza na kujiburudisha kwa anuai za vitu mbalimbali vya kuchezea; na watu wazima wanajiburudisha kwa magari, majumba, viwanda n.k. Katika michezo ya kitoto mmoja huwa mfalme mwingine akawa waziri, mmoja huwa mgonjwa na mwingine akawa tabibu na mmoja hujifanya mama na mwengine akawa mwana, lakini baada ya mchezo kumalizika hubainika kuwa hadhi na nafasi zote hizo zilikuwa za kutunga na za kufikirika tu. Katika maisha ya utu uzima pia yamkini kila mtu akapigania kuwa na hadhi na cheo hiki na kile katika jamii. Lakini wakati umri unapomalizika ndipo mtu hubaini kuwa yote hayo yalikuwa mambo ya kupita tu na ya kujibunia na kwamba yeye ameyapoteza maisha yake kwa kucheza nafasi mbalimbali za uigizaji katika mchezo huo. Leo hii wako wapi wafalme na masultani waliokuwa wakijigamba katika zama mbali mbali za historia?! Wako wapi makamanda na majemadari wa vita vikubwa vikubwa katika historia?! Ni kama kwamba muda wa mchezo wao umemalizika, na hivi sasa ni zamu ya kundi jingine kuingia mchezoni. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kumjua Mwenyezi Mungu ni suala la fitra na maumbile; na kama vumbi la dhambi na upotofu litasafika kwenye nyoyo za watu waliopotoka, wao pia watakiri na kuukubali ukweli huo. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa watu wengi huwa wanajitia pambani na kujighafilisha; na hawako tayari kukaa wakatafakari juu ya mwanzo na mwisho wao wenyewe pamoja na dunia wanayoishi ndani yake. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kujisahaulisha akhera na kutoelewa hakika yake huufanya moyo wa mtu uipende dunia na kushughulishwa na mambo ya kimaada na ya kidunia. Aidha tunajifunza kutokana na aya hizi kuwa maisha halisi na ya kweli ni ya akhera ambako kila mtu atakuwa katika hadhi na nafasi yake halisi. Huko hakuna machungu, dhulma wala uonevu na hakuna haki ya mtu yeyote yule itakayopotea.

Darsa ya 715 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 65 na 66 ambazo zinasema:

فَإِذَا رَكِبُوا فِي الْفُلْكِ دَعَوُا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ إِذَا هُمْ يُشْرِكُونَ

Na wanapo panda katika marikebu, humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafia ut'iifu. Lakini anapo wavua wakafika nchi kavu, mara wanamshirikisha.

لِيَكْفُرُوا بِمَا آتَيْنَاهُمْ وَلِيَتَمَتَّعُوا فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ

Ili wapate kuyakana tuliyo wapa, na wapate kujistarehesha. Lakini punde watajua!

Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia ambazo ziliashiria alama za uwezo na qudra ya Allah mbinguni na ardhini ili kuamsha hisia za kifitra na kimaumbile za wanadamu. Aya tulizosoma zinawakumbusha wanadamu kwa kuwauliza, wakati mnapohisi hatari imekukabilini mukawa mumekata tamaa ya kupata msaada wa kitu au mtu yeyote yule, ni nani mnayemuelekea na kumwomba msaada? Ni nani mnayemtaradhia na kumtaka msaada wakati meli inapokuwa inazama? Wakati ndege inapotaka kuanguka ni nani mnayemwomba akuokoeni? Ni Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye Mweza wa kukuokoeni na kukunusuruni na kifo cha wazi kabisa.

Katika maisha yake, wakati mwanadamu anapofikwa na matatizo na misukosuko, kwa kawaida hutegemea na kuomba msaada kwa sababu na nyenzo za kimaada na kwa jamaa na marafiki zake. Kwa sababu hiyo, ndiyo maana humsahau Mwenyezi Mungu. Lakini wakati anapokabiliwa na hatari kukawa hakuna kitu wala mtu yeyote wa kuitikia kilio chake cha kuomba msaada, hapo mwanadamu humwomba Mwenyezi Mungu peke yake na kuwasahau wengine wote. Lakini ajabu ni kwamba mwanadamu huyo huyo aliyeokolewa na Allah kwenye hatari ya shimo la mauti, humsahau tena Mola wake na kuendelea na maisha yake ya kimaada na kujistarehesha na neema za kidunia pasina hata kumshukuru Mwenyezi Mungu na kumkumbuka kwa neema hizo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba vumbi la mghafala na kujisahau hufanya ukungu kwenye fitra na maumbile ya mtu; lakini majanga na matukio ya hatari husafisha na kuliweka kando vumbi hilo na kuziamsha tena hisi za fitra ya mtu ya kumjua Mwenyezi Mungu. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa dua inayoombwa kwa ikhlasi hujibiwa na Mola. Hata mtu kafiri pia kama ataomba kwa ikhlasi anaweza kutakabaliwa. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kumshirikisha Mwenyezi Mungu ni aina fulani ya utovu wa shukrani kwake na kukufuru neema zake; na tauhidi ni aina mojawapo ya ushukurivu wa at'iya zake Mola. Wapenzi wasikilizaji darsa yetu ya leo imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa washukurivu wa neema zake, kubwa na ndogo, tunazozijua na tusizozijua. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

Tags