Jan 16, 2017 16:38 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni tena katika mfululizo wa vipindi hivi vinavyokosoa kwa mujibu wa aya za Qur'ani Tukufu na hadithi mienendo ya makundi yenye kuwakufurisha Waislamu wengine na kutekeleza jinai na mauaji ya kutisha dhidi yao hii leo ikiwa ni sehemu ya 16 ya mfululizo huo.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia kadhia nzima ya uhalali wa shufaa, (uombezi) ambapo tuliweka wazi kuwa, jambo hilo ni halali, kama ambavyo Waislamu karibu wote ispokuwa Mawahabi na Masalafi wanaliamini. Ndugu wasikilizaji, moja ya maudhui nyingine ambazo Mawahabi wamekuwa wakieneza urongo juu yake ni suala la zima la kutembelea makaburi. Historia ya Uislamu, inaonyesha kwamba Waislamu wote wamekuwa wakilitambua suala hilo kuwa ni suna na wakiyazuru bila matatizo yoyote. Zaidi ya hayo kuna riwaya maarufu inayoelezea wasila iliyofanywa na Nabii Adam (as) kupitia adhama ya Mtume Muhammad (saw) riwaya iliyopokelewa na Omar Ibnil-Khatwab kwamba: “Nabii Adam alikuwa na habari kamili kwamba katika mustakabali ataumbwa Mtume wa Uislamu. Hivyo akaelekea kwa Mwenyezi Mungu na kusema: Ewe Allah! Kwa haki ya Muhammad ninakuomba unisamehe mimi.” Mwisho wa riwaya. Jambo lingine linalofaa kuashiriwa hapa ni kwamba, shufaa ina masharti yake maalumu. Hii ikiwa na maana kwamba, shufaa ya Mitume na mawalii wa Mwenyezi Mungu inawahusu watu wenye imani na wanaotenda mema. Kwa ajili hiyo mtu ambaye hamwamini Mwenyezi Mungu na mafundisho ya dini sambamba na kukumbwa na aina za machafu, hawezi kunufaika na shufaa (uombezi). Alaa kulli hal aya kadhaa za Qur’ani Tukufu zimeelezea wazi suala la uepo wa shufaa, na kwamba ni jambo lisilo na shaka yoyote ndani yake, lakini kwa bahati mbaya makundi ya ukufurishaji na Kiwahabi kwa kutegemea dalili dhaifu sana, yanapinga suala hilo. Ndugu wasikilizaji moja ya maudhui nyingine ambazo Mawahabi wamekuwa wakieneza urongo juu yake ni suala zima la kutembelea makaburi. Historia ya Uislamu, inaonyesha kwamba Waislamu wote walikuwa wakilitambua suala hilo kuwa ni suna na daima walikuwa wakiyazuru.

Mtu wa kwanza kupiga marufuku suala hilo, alikuwa ni Ibn Taymiyyah. Ibn Taymiyyah alizitaja kuwa dhaifu na bandia hadithi zote zinazosema kuwa Mtukufu Mtume alikuwa akifanya ziara kuyatembelea makaburi. Kuhusu suala hilo Ibn Baaz, mufti wa zamani wa Saudia alinukuliwa akisema kuwa, kuomba dua yoyote, kuomba msaada, kutoa nadhiri nk kupitia kaburi la Mtume (saw) na mawalii wa Mwenyezi Mungu ni sawa na kuomba dua na msaada kwa masanamu ya miti na mawe na kwamba suala hilo ni ushirikina moja kwa moja. Kadhalika shekhe huyo wa Kiwahabi alikutaja kuwa ni uzushi (bidaa) kufanya safari kwa lengo la kwenda kulizuru kaburi hilo la Nabii wa Allah. Kuhusu suala hilo Ibn Baaz alitumia aya ya 117 ya Surat Muuminun inayosema: "Na anayemuomba - pamoja na Mwenyezi Mungu - mungu mwenginewe hana ushahidi wa hili; basi bila ya shaka hisabu yake iko kwa Mola wake Mlezi. Kwa hakika makafiri hawafanikiwi."

***************************************************

Makundi ya ukufurishaji kwa kwenda kinyume na mafundisho sahihi ya Qur'ani Tukufu na riwaya, yanakutaja kufanya ziara kwenye makaburi kuwa ni jambo la ushirikiana  sanjari na kuwajibisha kuyaharibi kabisa makaburi hayo. Mwaka 2007, Abu Omar al-Baghdadi, kiongozi wa zamani wa genge la kigaidi na kitakfiri la Daesh aliigawa itikadi ya kundi hilo katika vipengee 19, ambapo cha kwanza kilikuwa cha kuharibu masanamu na makaburi ambayo kwa mujibu wa imani yake, ni dhihirisho la ushirikina. Kuhusiana na suala hilo anasema kama ninavyomnukuu: "Sisi tunaamini katika kuharibu kila dhihirisho la ushirikina na umuhimu wa kuziwekea vikwazo nyenzo zote za suala hilo. Kwa kutegemea riwaya sahihi iliyopokelewa kutoka kwa Abu al-Hayaj Asadi, Mtume Mtukufu (saw) alimwamuru Ali (ra) akisema: Nakutuma kwenye kitu ambacho mimi nimetumwa kwa ajili yake. Ya kwamba uhakikishe umeharibu masanamu na makaburi yote na kuyasawazisha na ardhi." Mwisho wa kunukuu. Katika fremu hiyo wanachama wa kundi la Kiwahabi la Daesh, wamekuwa wakiharibu kwa kubomoa makaburi ya Mitume, mawalii wa Mwenyezi Mungu, wajukuu wa Mtume na masahaba kwa madai yale yale kwamba makabari hayo ni dhidhirisho na nembo ya ushirikina. Aidha kundi hilo mbali na makaburi ya Mitume na watu watukufu miongoni mwa shakhsia wa kidini na mawalii wa Allah wa upande wa Kishia na Kisuni, linaharibu pia turathi za kihistoria na kiutamaduni ambazo zipo katika maeneo linayoyadhibiti, huku zingine zikiporwa na kupelekwa kusipojulikana. Magaidi wenye mafungamano na genge la Jab'hatu Nusra walishambulia kaburi la Hujr ibn 'Adi, mmoja wa masahaba wakubwa wa Mtume (saw) huko katika mji wa Adra uliopo jimbo la Rif Dimashq, kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Syria, Damascus. Baada ya magaidi hao wasio na utu mioyoni mwao kubomoa kaburi hilo, waliuchukua mwili wa sahaba huyo na kuupeleka mahala pasipojulikana. Ama miongoni mwa jinai nyingine zilizofanywa na wanachama wa makundi ya kigaidi hususan Daesh ni kuharibu kaburi la Uwais al-Qarani, mmoja wa wafuasi watiifu na wakweli wa Amirul-Muuminin Imam Ali (as) na Ammar Bin Yassir, mmoja wa masahaba wema wa Mtume Muhammad (saw) katika mji wa Al-Raqqah, kaskazini mwa Syria. Ndugu wasikilizaji makaburi ya mashahidi wa vita vya Siffin, yapo kusini mashariki mwa mji wa Al-Raqqah na katika umbali wa karibu kilometa moja kutoka pwani ya mto Furati (Euphrates). Kwa kipindi chote cha historia, makaburi hayo ya mashahidi watatu yaani Uwais al-Qarani, Ammar Bin Yaasir na Ubayy Bin Qais, ambao waliuawa mwaka 37 Hijiria wakiwa na Imam Ali (as) katika vita dhidi ya jeshi la Muawiya, yalikuwa yamejengwa juu yake. Kadhalika kundi la Daesh liliharibu kaburi la Wabisah Bin Muabbad al-Assadi, mmoja wa masahaba wa Mtume (saw) ambalo linatajwa kuwa moja ya athari za zamani sana nchini Syria. Hali ikiwa ni hiyo huko Syria, makaburi na turathi za Kiislamu nchini Iraq, Yemen Libya, Mali, nazo hazikusalimika kutokana na uharibifu wa magaidi hao wa Kiwahabi.

Ni vyema mfahamu kuwa, baada ya kuanguka utawala wa Kanali Muammar Gaddafi nchini Libya, harakati za makundi ya Kisalafi na ukufurishaji hususan genge la Kiwahabi la Answaru Sharia, lilianza kuharibu makaburi ya wajukuu wa Ahlu Bait wa Mtume (as) na makaburi ya masahaba watukufu wa Nabii wa Allah (saw). Moja ya matukio machungu ya uharibifu huo, ilikuwa ni kubomoa na kulisambaratisha kaburi la mjukuu wa Imam al-Hassan Mujtabah (as) maarufu kwa jina la Abd As-Salam Al-Asmar. Kando na kaburi la mtukufu huyo aliyeitwa al-Asmar kutokana na kutumia muda mwingi katika ibada majira ya usiku, kulikuwa na maktaba yenye vitabu adhimu vya Kisuni na Kishia na nakala muhimu za kihistoria za maelfu ya miaka. Na kwa mujibu wa Waziri wa Utamaduni wa Libya, maktaba hiyo ilikuwa ikihesabiwa kuwa maktaba kubwa zaidi na ya kipekee nchini Libya. Hata hivyo na kwa masikitiko makubwa, baada ya uvamizi wa magaidi hao, walivitwaa vitabu hivyo na kisha kuvichoma moto.

***********************************

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni Makala inayokosoa kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu na Sunna za Bwana Mtume, mienendo ya makundi ya ukufurishaji, kutoka Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ndugu wasikilizaji maulama wanne wa madhehebu ya Kisuni na kwa mujibu wa kitabu cha 'Al-Fiqhi alaa Madhaahibil-Arbaa' wanakutambua kuzuru makaburi kuwa ni jambo la Sunna. Katika kitabu hicho kumeandikwa hivi: "Kuzuru kaburi la Mtume ni miongoni mwa Sunna za hadhi ya juu na kuhusiana na suala hilo kumepokelewa hadithi nyingi sana." Mwisho wa kunukuu. Hata hivyo Mawahabi wa ukufurishaji wameendelea kushikilia baadhi ya riwaya zisizo na itibari zilizoandikwa katika vitabu vyao na kufikia kuhalalisha kuharibu maeneo matukufu. Kwa mujibu wa watu hao, kufanya ziara kwenye makaburi ya watu wakubwa wa Kiislamu akiwemo Mtume Muhammad (saw) ni kinyume cha Tawhidi ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu na ni ushirikina, suala ambalo katika uhalisia wake, ni uongo mkubwa. Hii ni kwa kuwa kuyazuru makaburi hayo hakuna maana ya kuyaabudu. Kwa mujibu wa aya kadhaa na riwaya, kuzuru makaburi ni kitendo halali kabisa. Katika aya ya 56 ya Surat Ahzab kumeashiriwa nukta muhimu sana. Aya hiyo inasema: " Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamswalia Nabii. Enyi mlioamini! Mswalieni na mumsalimu kwa salamu." Katika aya hiyo tunashuhudia kwamba licha ya kuwa Mtume Muhammad amekwishafariki dunia, lakini Mwenyezi Mungu na malaika wake wanamtumia salamu mtukufu huyo. Aidha Mwenyezi Mungu anawataka waumini nao kufungamana na Nabii wake kwa kumtumia salamu pia. Hii ikiwa na maana kwamba kinyume kabisa na dhana ya Mawahabi, na makundi ya ukufurishaji, Mtume Muhammad (saw) anapokea salamu za Mwenyezi Mungu, malaika na waumini kwa ajili yake. Kwa ajili hiyo, kumtakia amani na kumuombea dua Nabii huyo wa Allah si jambo lisilo na faida kama wanavyodai Mawahabi na ni kwa msingi huo ndio maana Mwenyezi Mungu akalisisitiza ndani ya Qur'ani Tukufu.

****************************************

Kwa mujibu wa mafundisho ya Qur'an Tukufu, kuwapenda Ahlu Bayti na watu wa karibu na Mtume (saw) ni suala ambalo limelazimishwa kwa waumini. Aya ya 23 ya Surat sh-Shura inasema: "Hayo ndiyo aliyowabashiria Mwenyezi Mungu waja wake walio amini na wakatenda mema. Sema: Sikuombeni malipo yoyote kwenu ila mapenzi kwa watu wangu wa karibu (Ahlu Bayti). Na anayefanya wema tutamzidishia wema. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu Mwenye shukrani." Kwa ajili hiyo na kwa kuzingatia kuwa kufanya ziara ni moja ya ishara za mapenzi, hivyo bila shaka kufanya ziara katika kaburi la Mtume na watu wake wa karibu ni ishara ya wazi ya kudhihirisha mapenzi ya hali ya juu kwa watukufu hao. Kwa ajili hiyo wakati mwanadamu anapofanya ziara kwenye makaburi ya watu hao anakuwa ameonyesha mapenzi kwa Mtume na Ahlu Bayti wake sanjari na kutangaza utayarifu wake wa kufuata na kuenzi njia yao. Aidha wakati mwanadamu anapozuru kaburi la watu wa karibu na Mtume (saw) hupata kukumbuka matukufu ya shakhasia hao na hivyo kufuata njia zao za uadilifu na kufikia ukamilifu wa tabia njema. Kuhusiana na suala hilo imenukuliwa riwaya moja kutoka kwa Mtume Muhammad (saw) akihimiza juu ya udharura wa kuzuru makaburi kwa kusema: "Tembeleeni makaburi kwani yanakukumbusheni Akhera." Mwisho wa kunukuu. Mbali na hayo kitabu cha Sahih Muslim kimenukuu riwaya kutoka kwa Bibi Aisha inayosema, "Mwishoni mwa usiku Mtume wa Allah (saw) alikuwa akiyatembelea makuburi ya Baqii na kuwatolea salamu watu waliozikwa mahala hapo." Mwisho wa riwaya. Aidha katika vitabu mbalimbali vya fiqhi vya Ahlus-Sunnah kumesisitiziwa sana udharura wa kuzuru makaburi na kwamba suala hilo ni suna. Hii ni katika hali ambayo kwa mujibu wa hadithi tofauti, Mtukufu Mtume (saw) amewahimiza watu juu ya suala hilo kwa kusema: "Atakayenizuru mimi baada ya kufariki kwangu dunia, atakuwa sawa na mtu aliyenizuru nikiwa hai." Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 16 ya makala hii inakomea hapa kwa leo, tukutane tena katika sehemu ya 17 wiki ijayo, mimi ni Sudi Jafari Shaban, kwaherini……./

 

 

 

 

 

Tags