Jun 13, 2024 02:23 UTC
  • Hizbullah yainyeshea Israel kwa mvua ya maroketi baada ya kamanda kuuawa

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imeshambulia kwa mamia ya maroketi ngome na maeneo ya walowezi wa Kizayuni huko kaskazini mwa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel.

Press TV iliripoti habari hiyo jana Jumatano na kunukuu taarifa ya jeshi la Israel iliyosema kuwa, Hizbullah imevurumisha maroketi zaidi ya 200 kutoka kusini mwa Lebanon kuelekea eneo linalokaliwa kwa mabavu na Wazayuni maghasibu la al-Jalil (Galilee).

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, shambulio hilo ambalo ni moja ya mashambulio makubwa yaliyofanywa na Hizbullah katika miezi ya hivi karibuni, lililenga pia jiji la Tiberias kwa mara ya kwanza.

Shambulio hilo kubwa la maroketi ya Hizbullah dhidi ya ngome za walowezi wa Kizayuni limejiri baada ya kamanda mwandamizi wa kundi hilo la muqawama kuuawa shahidi kusini mwa Lebanon. 

Sami Abdallah 'Abu Taleb' aliuawa mapema jana Jumatano katika hujuma za anga za Wazayuni zilizolenga jengo la makazi ya watu katika mji wa Jwaya, yapata kilomita 95 kusini mwa Beirut, mji mkuu wa Lebanon.

Sami Abdallah, kamanda mwandamizi wa Hizbullah aliyeuawa shahidi

Wakati huo huo, Naibu Katibu Mkuu wa Hezbollah amesema kile ambacho Hizbullah tayari imeonyesha katika kipindi cha vita vya kuunga mkono Gaza na katika kuilinda Lebanon ni sehemu ndogo tu ya uwezo wake wa kijeshi. Sheikh Naim Qassem amesisitiza kwamba Hizbullah haitaki vita lakini amesema “Ikiwa adui anataka kuanzisha vita vipya (dhidi ya Lebanon) basi Hizbullah hatutasita kujibu. Waisraeli wanafahamu ukweli huo.”

Utawala wa Israel umekuwa ukishambulia mara kwa mara eneo la kusini mwa Lebanon tangu tarehe 7 Oktoba ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza.

Tags