Iran yakosoa kupunguzwa misaada ya kimataifa kwa wakimbizi wa Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i134198-iran_yakosoa_kupunguzwa_misaada_ya_kimataifa_kwa_wakimbizi_wa_afghanistan
Iran imeikosoa jamii ya kimataifa kwa kushindwa kutimiza hata ahadi za kimsingi za kuwasaidia mamilioni ya wakimbizi wa Kiaghani; ikisema kuwa kupunguzwa misaada kumeifanya nchi hiyo kubeba mzigo mkubwa wa kifedha licha ya indhari za miaka mingi.
(last modified 2025-12-12T02:38:58+00:00 )
Dec 12, 2025 02:38 UTC
  •  Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran UN, Amir Saeed Iravani
    Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran UN, Amir Saeed Iravani

Iran imeikosoa jamii ya kimataifa kwa kushindwa kutimiza hata ahadi za kimsingi za kuwasaidia mamilioni ya wakimbizi wa Kiaghani; ikisema kuwa kupunguzwa misaada kumeifanya nchi hiyo kubeba mzigo mkubwa wa kifedha licha ya indhari za miaka mingi.

Akihutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Afghanistan, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran UN, Amir Saeed Iravani ameeleza kuwa ufadhili wa kimataifa kwa ajili ya wakimbizi wa Afghanistan nchini Iran unatazamiwa kupungua kwa zaidi ya asilimia 60 mwaka 2026.

"Iran imebeba mzigo usio na uwiano kwa miongo kadhaa kwa kuwahifadhi mamilioni ya wakimbizi wa Afghanistan huku yenyewe ikiwekewa vikwazo vikali vya upande mmoja. Jukumu hili limesababisha mashinikizo makubwa ya kiuchumi na kiusalama, na gharama za kila mwaka zimefikia karibu dola bilioni kumi, bila ya kuwepo msaada wa kutosha wa kimataifa," amesema Amir Saeed Iravani.

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran UN ameongeza kuwa, gharama inazotumia Iran kila mwaka kwa ajili ya kuwahifadhi wakimbizi wa Afghanistan zinafika karibu dola bilioni 10 na kwamba Tehran hugharamia huduma za afya na elimu, makazi, miundombinu, usalama na ruzuku ya serikali kama vile chakula, mafuta na umeme.

Kiwango hicho kinaonyesha fedha inazotumia Iran kwa ajili ya wakimbizi wa Kiafghani, na Tehran inasema kuwa inalazimika kubeba gharama zote hizo peke yake. 

Wakati huo huo Iravani amekadhibisha madai ya Zalmay Khalilzad, mjumbe wa zamani wa Marekani nchini Afghanistan, kwamba Iran inawafukuza bila utaratibu wakimbizi wa Kiafghani. Amesema, inachokifanya Iran ni kuwarejesha Afghanistan raia wa nchi hiyo wasio na vibali rasmi, yaani wahamiaji haramu.