Jun 12, 2024 11:14 UTC
  • Mgombea wa urais Iran: Waislamu tuungane kuitetea Gaza

Mmoja wa wagombea wa urais nchini Iran ametoa mwito kwa Waislamu kuwa na umoja na mshikamano katika kulitetea taifa madhulumu la Palestina, hasa wakazi wa Ukanda wa Gaza wanaokabiliwa na mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni wa Israel tokea Oktoba mwaka jana 2023.

Mostafa Pourmohammadi ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Waziri wa Sheria hapa nchini ametoa mwito huo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Alam na kuongeza kuwa, kuna haja ya kuundwa ustaarabu mpya wa Kiislamu na kuhuisha hadhi na izza ya umma wa Kiislamu.

Pourmohammadi ameeleza bayana kuwa, "Tuunganeni ili kulinda haki zetu sisi kwa sisi na kuimarisha uhusiano wetu, tuunde maslahi ya pamoja, na tumairishe usalama na uthabiti wetu."

Mgombea huyo wa uchaguzi wa rais nchini Iran amesisitiza kwa kusema: Tunapasa kuungana dhidi ya maadui, na tushirikiane katika kuwahami wananchi madhulumu wa Palestina na watu wa Gaza, na tuunde ustaarabu mpya wa Kiislamu, na tuhuishe izza ya mataifa ya Kiislamu.

Wagombea wa kiti cha rais nchini Iran wameanza kubainisha mipango yao kuhusu ustawi wa nchi huku kampeni za uchaguzi zikianza kushika kasi.

Wagombea wa urais nchini Iran 2024

Wagombea sita wameidhinishwa na Baraza la Kulinda Katiba kuwania urais katika uchaguzi wa rais wa kabla ya wakati uliopangwa kufanyika Juni 28.

Kura hiyo iliitishwa baada ya Rais Ebrahim Raisi kufa shahidi akiwa na watu wengine saba mnamo Mei 19, wakati helikopta iliyokuwa imewabeba ilipoanguka katika mkoa wa Azerbaija Mashariki, eneo la milima la kaskazini-magharibi mwa Iran huku kukiwa na hali ya ukungu. 

 

Tags