Msimamo wa Makundi ya Mapambano ya Palestina Kuhusu Azimio la UN
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i112826-msimamo_wa_makundi_ya_mapambano_ya_palestina_kuhusu_azimio_la_un
Makundi ya mapambano ya Palestina yametoa mjibizo kwa hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kupitisha azimio lililopendekezwa na Marekani kuhusu matukio ya Ghaza kwa kusisitiza kuwa: azimio hilo linahitaji hakikisho la utekelezaji.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Jun 11, 2024 23:24 UTC
  • Msimamo wa Makundi ya Mapambano ya Palestina Kuhusu Azimio la UN

Makundi ya mapambano ya Palestina yametoa mjibizo kwa hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kupitisha azimio lililopendekezwa na Marekani kuhusu matukio ya Ghaza kwa kusisitiza kuwa: azimio hilo linahitaji hakikisho la utekelezaji.

Azimio lililopendekezwa na Marekani la kutekelezwa usitishaji vita huko Ghaza na kuachiliwa huru mateka lilipitishwa katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa cha Jumatatu tarehe 10 Juni kwa kura 14 za ‘ndiyo’ za wanachama wa baraza hilo na kura moja ya Russia ya kujizuia kupiga kura pasi na kupingwa hata kwa kura moja.

Katika azimio nambari 2735 la Baraza la Usalama ambalo lina vifungu saba imeelezwa kuwa, azimio hilo lililopendekezwa na Marekani linaungana na maazimio yote yanayohusiana na hilo kuhusu hali ya eneo la Asia Magharibi, likiwemo suala la Palestina, na kutilia mkazo umuhimu wa juhudi za kidiplomasia za mtawalia zinazofanywa na Misri, Qatar na Marekani kwa lengo la kuwezesha kufikiwa na kutekelezwa kwa awamu tatu mapatano ya kusitisha vita kikamilifu katika Ukanda wa Ghaza.

 

Kusitishwa mapigano bila kupoteza muda, kuondoka jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika maeneo yenye watu wengi ya Ukanda wa Ghaza, kurejea makwao raia wa Palestina, pamoja na kusambazwa kwa usalama na kwa kiwango chenye athari kubwa misaada ya kibinadamu katika eneo lote la Ghaza pamoja na kubadilishana mateka ni miongoni mwa masuala makuu yaliyozungumziwa katika azimio hilo.

Hata hivyo kwa upande wao, makundi ya wanamapambano wa Palestina yametaka kwa umoja wao na kwa sauti moja yapewe hakikisho la kutekelezwa kivitendo azimio hilo.

Wanamuqawama wa Palestina

 

Mahmoud Mardawi ambaye ni mmoja wa viongozi wa harakati ya Hamas, ametoa mjibizo kwa hatua ya Baraza la Usalama la UN ya kupitisha rasimu ya azimio 2735 kwa kueleza kwamba harakati hiyo iko tayari kutoa ushirikiano kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha vita. Mardawi ameongezea kwa kusema: “tumelipokea vizuri azimio lililopitishwa na Baraza la Usalama kuhusu usitishaji vita huko Ghaza na tuko tayari kutoa ushirikiano kwa ajili ya utekelezaji wake; nao wapatanishi inapasa wachukue ahadi ya hadharani kutoka kwa utawala ghasibu unaokalia ardhi kwa mabavu kuhusu usitishaji vita ili tuingie katika mazungumzo”.

Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina nayo pia imetoa taarifa inayosisitiza kuwa, kupitishwa azimio lililopendekezwa na Marekani la kusitisha vita huko Ghaza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kunahitaji dhamana ya utekelezaji ili kuwezesha kusimamishwa kwa sura ya kudumu uvamizi na kuondoka kikamilifu Wazayuni huko Ghaza. Taarifa ya harakati hiyo imebainisha kuwa, kuna sentensi za maelezo ya jumla na tungo zenye utata kwenye andiko la azimio hilo ambazo inapasa zitolewe ufafanuzi wa kina ili kwa kisingizio chochote kile utawala ghasibu wa Kizayuni usije ukapatiwa fursa ya kuanzisha tena uchokozi na uvamizi wake wa kijeshi. Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imetahadharisha kuwa: Misimamo ya kiadui ya Marekani dhidi ya wananchi wa Palestina na kushiriki kwake katika vita angamizi vya Wazayuni huko Ghaza kunaifanya kila hatua inayochukuliwa na Marekani itiliwe shaka; na kwa hiyo inapasa kuwa na hadhari.

Riyadh Mansour, Mwakilishi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina alihutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa cha kupitisha rasimu ya azimio la usitishaji vita huko Ghaza na akasema: sasa jukumu la utekelezaji wa azimio hili liko upande wa Israel. Riyadh Mansour alisisitiza kwa kusema: “hatutaki hata nyanda moja ya ardhi ya Ghaza iwe chini ya udhibiti wa jeshi la utawala wa Israel”.

Msimamo wa pamoja wa makundi ya Palestina kuhusiana na azimio lililopendekezwa na Marekani unaonyesha mwamko na uelewa walionao na jinsi wanavyokwenda sambamba na mwenendo wa matukio yanayojiri katika eneo na kukabiliana na uchu wa kujivutia upande wao zilionao Washington na Tel Aviv. Matukio ya miaka ya hivi karibuni hususan baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa yameonyesha kuwa, Ikulu ya White House ambayo ni muitifaki mkuu na mshirika wa jinai zinazofanywa na Wazayuni huko Ghaza, haiko tayari kusimamisha uungaji mkono wake kwa utawala wa Kizayuni.

Biden, mshirika wa jinai za Israel Ghaza

 

Viongozi wa Marekani wameonyesha waziwazi kuwa wanatumia kila fursa waipatayo kuwaunga mkono Wazayuni na kuweka vizuizi na mashinikizo dhidi ya Wapalestina. Katika miezi ya hivi karibuni, na kutokana na kushadidi maandamano ya kupinga utawala wa Kizayuni na Marekani duniani kote, viongozi wa Marekani wamelazimika kujionyesha kidhahiri kuwa ni wapatanishi wa kuhitimisha vita vya Ghaza.

Pamoja na hayo, kwa kuzingatia kumbukumbu za historia, viongozi wa Marekani hawako tayari kusitisha uungaji mkono wao kwa utawala wa Kizayuni. Katika hali hiyo, kutokana na makundi ya Muqawama ya Palestina kulielewa hilo barabara na kwa kuzingatia mafanikio yaliyopata katika vita na utawala wa Kizayuni, yameyafanya malengo na matakwa yao kuhusiana na Ghaza katika mazungumzo ya usitishaji vita kuwa ndio masharti na masuala yao ya msingi na kutaka yapewe hakikisho na dhamana ya kutekelezwa azimio la Baraza la Usalama la UN.

Kuondoka kikamilifu jeshi la utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza, kurejea wakimbizi wa Kipalestina na suala la kujengwa upya Ghaza sambamba na kuchukuliwa hatua maghasibu wavamizi wa Kizayuni, ni miongoni mwa misingi mikuu ya matakwa ya makundi ya Muqawama ya Palestina ambayo yameshurutisha kukubaliwa masuala hayo na utawala wa Kizayuni na muungaji wake mkuu yaani Marekani, na makundi hayo kuwa tayari kuendelea na mazungumzo ya kusitisha mapigano…/