Jun 13, 2024 07:41 UTC
  • HAMAS: Blinken amevuruga juhudi za usitishaji vita Gaza

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken anabeba dhima ya kutofikiwa makubaliano tarajiwa ya kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza.

Osama Hamdan, Mwakilishi wa HAMAS nchini Lebanon amesema hayo na kuongeza kuwa, utawala wa Kizayuni unafanya kila liwezekanalo kuzuia kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita Gaza.

Amesema katika mahojiano na televisheni ya al-Araby kuwa, "Utawala wa Marekani ni mshirika wa Israel katika kukwepa kutoa dhamana ya kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita wa kudumu Gaza."

HAMAS imekosoa vikali matamshi ya Blinken kwa kudai kwamba harakati hiyo ya muqawama ndio inakwamisha kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita Gaza. Hamdan amesema: Kwa matamshi hayo, Blinken ni sehemu ya matatizo na wala si suluhu ya mgogoro. 

Kundi hilo la kupigania ukombozi wa Palestina limesema kuwa limeonyesha mtazamo na msimamo chanya katika hatua zote za mazugumzo yasiyo ya moja kwa moja ya kujadili mapendekezo ya usitishaji vita.

Wziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken

Juzi Jumanne, harakati kuu za muqawama na ukombozi wa Palestina za HAMAS na Jihadul-Islami zilitoa jibu rasmi kwa pendekezo linaloungwa mkono na Marekani la kusitisha mapigano Gaza na kubadilishana mateka kwa wafungwa kwa kuongeza baadhi ya "maoni" kuhusu mpango huo. Hayo yalithibitishwa na wapatanishi wa Qatar na Misri.

HAMAS na Jihadul-Islami zimesisitiza kuwa ziko tayari kuzungumzia kwa mtazamo chanya mpango huo na kufikia makubaliano na kwamba kipaumbele chao ni "kusimamishwa kikamilifu" mashambulizi yanayoendelea ya Israel dhidi ya Gaza.

Tags