Jan 24, 2017 08:39 UTC

Sura ya Ar-Rum, aya ya 1-8 (Darsa ya 717)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Baada ya kuhatimisha tarjumi na maelezo ya sura ya 29 ya Al-A'nkabut, katika darsa hii ya 717 tutaanza kutoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 30 ya Qur'ani tukufu ya Ar-Rum. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya kwanza hadi ya tano ya sura hiyo ambazo zinasema:

الم

 Alif Lam Mim (A.L.M.)

غُلِبَتِ الرُّومُ

 Warumi wameshindwa,

في أَدْنَى الأَرْضِ وَهُم مِّن بَعْدِ غَلَبِهِمْ سَيَغْلِبُونَ

Katika nchi iliyo karibu. Nao baada ya kushindwa kwao watashinda

فِي بِضْعِ سِنِينَ لِلَّهِ الأَمْرُ مِن قَبْلُ وَمِن بَعْدُ وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ

Katika miaka michache. Amri ni ya Mwenyezi Mungu kabla yake na baada yake. Na siku hiyo Waumini watafurahi.

بِنَصْرِ اللَّهِ يَنصُرُ مَن يَشَاء وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ

Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Naye ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.

Kwa mujibu wa maandiko ya historia, kwa muda mrefu vilishuhudiwa vita na mapigano baina ya Falme za kale za Rumi na Iran. Wakati Bwana Mtume Muhammad SAW alipokuwa Makka, vita baina ya Rumi na Iran vilitokea karibu na ardhi hiyo ya Hijaz na Warumi wakashindwa. Mwenyezi Mungu SW alimpa habari Mtume wake kwamba japokuwa Warumi wameshindwa lakini katika vita vitakavyofuatia Warumi watapata ushindi. Kwa kuwa utabiri huo wa ghaibu ulithibiti waumini walipata yakini na uhakika kwamba ahadi ya ushindi wao dhidi ya washirikina pia itathibiti. Kwa sababu kila kitu kiko mikononi mwa Allah, ambaye humpa auni na msaada wake yeyote yule amtakaye na kumfanya awe na nguvu na izza na miongoni mwa wenye kupata rehma zake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba habari za ghaibu za Qur'ani na utabiri uliofanywa na kitabu hicho cha mbinguni ni miongoni mwa hoja za kuthibitisha miujiza iliyomo ndani yake. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tusiwe wenye kuvunjika moyo na kupoteza matumaini kutokana na kushindwa. Tunapaswa muda wote tuwe na matumaini ya kupata auni na msaada wa Mwenyezi Mungu. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba jambo lolote linalofanywa na Allah linakuwa na hekima ndani yake. Kushindwa na kushinda waumini nako pia kunatokana na hekima yake Mola. Pamoja na hayo waumini wanapaswa watekeleze wajibu wao; ama kuhusu natija na matokeo yake hilo haliko kwenye mamlaka yao; mwisho na hatima ya kila kitu iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 6 na ya 7 ambazo zinasema:

وَعْدَ اللَّهِ لا يُخْلِفُ اللَّهُ وَعْدَهُ وَلَكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لا يَعْلَمُونَ

Ni ahadi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake. Lakini watu wengi hawajui.

 يَعْلَمُونَ ظَاهِرًا مِّنَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ عَنِ الآخِرَةِ هُمْ غَافِلُونَ

Wanajua hali ya dhaahiri ya maisha ya dunia, na wameghafilika na Akhera.

Baada ya aya zilizotangulia kuzungumzia ahadi ya ushindi wa Waislamu dhidi ya washirikina, aya tulizosoma zinasema: Enyi watu, msitilie shaka ahadi ya Mwenyezi Mungu, kwani ahadi hiyo ni ya hakika na haiwezekani katu kwa Yeye Mola kukhalifu aliyoyaahidi. Tab'an kwa wale watu wasiomwamini Allah, au wenye imani dhaifu, hao hawana imani na yakini juu ya ahadi ya Mola Mwenyezi. Na sababu ni kwamba hawana uelewa wa elimu, nguvu na hekima ya Mwenyezi Mungu bali wanachokiona wao ni visababishi vya dhahiri vya kimaada na wanakuhakiki na kukutolea tafsiri kushinda na kushindwa kwa kutumia vipimo na sababu za kimaada tu. Kwa kuwa watu hao wameghafilika na akhera wanakiangalia kila kitu kwa kutumia miwani ya kidunia yenye mpaka wa uoni na kuzikosesha nafsi zao neema ya kubaini hakika halisi za ulimwengu.

Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kwa kawaida kukhalifu na kwenda kinyume na ahadi anazotoa mtu hutokana na ujinga, kukosa uwezo wa kutekeleza au kujuta kwa ahadi aliyotoa, sifa na hali ambazo Allah SW ametakasika nazo. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kupenda dunia na mambo ya kimaada humfanya mtu awe na uono finyu na wa kijuujuu wa mambo. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kushughulishwa na mambo ya dhahiri ya dunia na kutekwa nayo ndiyo chanzo cha kujisahau mtu na kughafilika na akhera.

Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 8 ambayo inasema:

أَوَلَمْ يَتَفَكَّرُوا فِي أَنفُسِهِمْ مَا خَلَقَ اللَّهُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا إِلاَّ بِالْحَقِّ وَأَجَلٍ مُّسَمًّى وَإِنَّ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ بِلِقَاء رَبِّهِمْ لَكَافِرُونَ

Je! Hawafikiri katika nafsi zao? Mwenyezi Mungu hakuumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake ila kwa Haki na kwa muda maalumu. Na hakika watu wengi bila ya shaka ni wenye kukataa kuwa watakutana na Mola wao Mlezi.

Aya hii kama zilivyo aya nyingine nyingi za Qur'ani inawataka watu watafakari juu ya mfumo wa ulimwengu wa maumbile na kuzirejea dhamiri na akili zao. Wakae na kujiuliza, ni nani hasa aliyeziumba mbingu na ardhi? Hivi kweli uumbaji huu umetokea kwa bahati tu na bila ya lengo? Je, dunia haina mwanzo ilikoanzia wala mwisho inakoelekea? Kweli mtu anaweza kuamini kwamba yeye mwanadamu awe na akili, hisia na ufahamu na afanye mambo yake kwa ratiba na mipango maalumu, lakini ulimwengu huu wa maumbile wenye adhama kama hii, huku yeye mwanadamu mwenyewe akiwa moja ya sehemu zake ndogo tu zilizomo ndani yake, uwe hauendeshwi kwa tadbiri wala hisi zozote za uelewa? Mtu anaweza kweli kukubali kwamba maisha yetu sisi wanadamu yanaishia katika dunia hii na wala hakutakuwepo na ulimwengu mwingine? Bila ya shaka watu wengi wenye mapenzi ya dunia wanakanusha kuwepo akhera na kuhudhurishwa mbele ya mahakama ya uadilifu ya Allah, ili kwa mawazo yao waweze kupata raha na starehe za dunia hii bila ya wasiwasi wala hofu ya chochote. Lakini watu wenye kutafakari na kutumia akili zao wanaamini kuwa mfumo wa ulimwengu una lengo sahihi na la mantiki na wanaitakidi kwamba uumbaji una mfumo maalumu na wa uhakika unaodhihirisha hekima ya Muumba wa dunia na vyote vilivyomo ndani yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Uislamu umewatolea wito watu wa kuwataka watafakri kuhusu mfumo wa ulimwengu ili imani zao juu ya Allah na dini hiyo tukufu zitokane na maarifa na utambuzi sahihi. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa uumbaji una lengo na pia umeainishiwa muda na wakati maalumu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba kukanusha Siku ya Kiyama hakutokani na fikra na hoja yenye mantiki bali chimbuko lake ni kupenda dunia na uchu wa kutaka kuendelea kubaki daima ndani yake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 717 ya Qur'ani, na ya kwanza kuzungumzia sura ya 30 ya Ar-Rum imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe maarifa ya kumtambua kwa namna inavyostahiki na kumwabudu kwa namna anavyostahiki kuabudiwa. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags