Jan 24, 2017 09:11 UTC

Sura ya Ar-Rum, aya ya 9-13 (Darsa ya 718)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 718 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 30 ya Ar-Rum. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 9 na 10 ambazo zinasema:

أَوَلَمْ يَسِيرُوا فِي الأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ كَانُوا أَشَدَّ مِنْهُمْ قُوَّةً وَأَثَارُوا الأَرْضَ وَعَمَرُوهَا أَكْثَرَ مِمَّا عَمَرُوهَا وَجَاءَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَمَا كَانَ اللَّهُ لِيَظْلِمَهُمْ وَلَكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ

Je! Hawatembei katika ardhi wakaona ulivyo kuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Nao walikuwa na nguvu zaidi kuliko wao, na wakiilima ardhi na kuistawisha zaidi kuliko walivyo istawisha wao. Na Mitume wao wakawajia na dalili zilizo wazi. Basi hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wakijidhulumu nafsi zao wenyewe.

ثمَّ كَانَ عَاقِبَةَ الَّذِينَ أَسَاؤُوا السُّوأَى أَن كَذَّبُوا بِآيَاتِ اللَّهِ وَكَانُوا بِهَا يَسْتَهْزِؤُون

Kisha ukawa mwisho wa walio fanya ubaya ni kuzikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakawa wanazifanyia stihzai.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizowakosoa watu wasiotumia akili zao na kutafakari juu ya uumbwaji wa mbingu na ardhi na kuwataka watafakari juu ya mfumo huo wa uumbwaji wa ulimwengu na vilivyomo ndani yake ili waweze kubaini kuwa vyote hivyo viko kwa lengo maalumu na wajue kwamba mfumo huo umeumbwa kwa msingi wa haki. Aya tulizosoma zinawaelekea watu hao na kuwauliza: Kwa nini hampati mazingatio kutokana na historia ya waliotangulia? Kwa nini wakati mnaposafiri katika sehemu mbalimbali hamuangalii mabaki na magofu ya athari zilizoachwa na kaumu zilizopita na kupata funzo na ibra ndani yake? Kaumu ambazo zilikuwa na konde, mabustani na mashamba yaliyonawiri na yaliyosheheni mazao; na watu wake walikuwa na utajiri mkubwa mno; lakini waliangamizwa wao wenyewe na vyote walivyokuwa navyo kwa sababu ya kuikana haki na kufanya madhambi na maovu na hakijabakia chochote zaidi ya magofu yao. Kuangamizwa kwao huko yalikuwa matokeo ya dhulma waliyozifanyia nafsi zao. Kwa sababu katika utamaduni na mafundisho ya Uislamu haijuzu mtu kuwadhulumu watu na pia kuidhulumu nafsi yake mwenyewe. Kinyume na nadharia ya Umwanadamu kwa kimombo Humanism, ambayo inasema inajuzu mtu kufanya lolote atakalo isipokuwa pale atakaposababisha madhara kwa wengine, katika mafundisho ya Uislamu mtu hana haki ya kuidhuru hata nafsi yake mwenyewe seuze wanadamu wenziwe. Tab'an madhara makubwa zaidi anayoisababishia mtu nafsi yake ni kuacha kutumia akili na dhamiri yake na kukana hakika ambazo zinambainikia wazi pale anapoitumia sawasawa akili na dhamiri yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kufanya safari za kutembelea maeneo ya kale kwa madhumuni ya kutalii historia ya kaumu zilizopita na kupata ibra na mafunzo kutokana na hatima zilizowapata watu wa kaumu hizo ni jambo linalotiliwa mkazo na Qur'ani tukufu. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa matukio ya historia yana usuli na kanuni maalumu; na mtu anaweza kupata somo na funzo kwa waliopita kwa faida ya wanaokuja baada yao. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba furaha ya maisha na saada ya watu na mataifa havipatikani kwenye kivuli cha nguvu za mamlaka na madaraka, maendeleo na ustawi wa mambo ya kidhahiri; bali msingi wa saada na fanaka ya kweli ni imani juu ya Allah na kufuata njia ya Mitume wake. Aya hizi aidha zinatufunza kuwa kushupalia kufanya, kudumu na kurudia mara kwa mara madhambi humfanya mtu awe na mwisho mbaya na kuishia kuikadhibisha haki na kuifanyia kejeli na istihazi.

Tunaihatimisha darsa yetu ya leo kwa aya ya 11, 12 na 13 ambazo zinasema:

اللَّهُ يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ ثُمَّ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ

Mwenyezi Mungu huanzisha uumbaji, tena akaurudisha mara ya pili, na kisha mtarejeshwa kwake.

وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ يُبْلِسُ الْمُجْرِمُونَ

Na Siku itapo simama Saa wakosefu watakata tamaa.

وَلَمْ يَكُن لَّهُم مِّن شُرَكَائِهِمْ شُفَعَاء وَكَانُوا بِشُرَكَائِهِمْ كَافِرِينَ

Wala hawatakuwa na waombezi miongoni mwa walio kuwa wakiwashirikisha (na Mungu); na wao wenyewe watawakataa hao washirikishwa wao.

Kwa mujibu wa aya za Qur'ani, mauti ni kitamatishi cha maisha ya mwanadamu katika dunia hii na kaburi ni mlango wa kupita kuelekea ulimwengu mwingine. Kama ambavyo kujifungua kwa mama ni kitamatishi cha maisha ya kiumbe mwanadamu ndani ya tumbo la mama yake na mlango wa kupita kwa ajili ya kuingia katika ulimwengu huu. Kuhusiana na nukta hiyo aya tulizosoma zinasema: Kuumbwa kwenu hapo kabla hakukuwa, wala kufa kwenu katika dunia hii hakuko kwenye mamlaka yenu. Nyinyi mumekuja hapa duniani kwa irada ya Mwenyezi Mungu na mtaondoka pia kwa kutaka Yeye Mola. Aidha maisha yenu ya mara ya pili Siku ya Kiyama huko akhera baada ya kufufuliwa, nayo pia si jambo la hiyari; mtake msitake, nyinyi mtahudhurishwa mbele ya Mola wenu siku hiyo. Kwa hiyo fanyeni amali njema ili msiende huko mikono mitupu na mkajuta kwa mliyoyafanya duniani. Msijenge mapenzi ya kupindukia kwa watu, vitu na mambo ya dunia, kwa sababu hakuna kitu chochote wala mtu yeyote atakayeweza kukusaidieni huko akhera. Wale mnaowadhania leo kuwa wana uwezo wa kukutakieni shufaa Siku ya Kiyama mtakuja kubainikiwa siku hiyo na udhaifu wao na mtajua kwamba wao hawawezi kufanya lolote ili muweze kuokoka.

Naam; washirikina, ambao walikuwa wakiyaona masanamu ni waombezi wao Siku ya Kiyama, siku hiyo watajua kwamba vitu hivyo visivyo na roho na uhai havikuwa na nafasi wala sifa yoyote ya uwezo wa kuendesha masuala ya ulimwengu; na kwa hakika hasa havikuwa na thamani yoyote. Wakati huo watakata tamaa ya kupata uombezi wa vitu hivyo na kubaki na huzuni na majonzi na vile vile hawatokuwa na matumaini yoyote ya kupata rehma za Mwenyezi Mungu. Na sababu yake ni kwamba hapa duniani walikuwa na uadui na Mitume na wakawapinga kwa kadiri kwamba hawakujibakishia hata upenyo mwembamba wa matumaini ya kwenda kupata rehma za Mola katika siku hiyo huko akhera.

Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mfumo wa ulimwengu umeanzia kwa Mwenyezi Mungu na unarejea tena kwake Yeye Mola Aliyetukuka. Kwa maneno mengine, uumbaji na ufufuo ni kitu kimoja. Na kughafilika na ukweli huu kutakuja kumfanya mtu ajute na kukata tamaa katika mustakabali huko anakoelekea. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tusiathiriwe wala kuhuzunishwa na furaha na kulewa raha na starehe kwa waovu na wafanya madhambi hapa duniani, kwa sababu Siku ya Kiyama watakuwa katika majuto, majonzi na huzuni kubwa mno. Aya hizi aidha zinatutaka tuelewe kwamba Siku ya Kiyama mapenzi bandia na mahaba yasiyo na msingi ya kidunia yatageuka kuwa chuki na uadui baina ya watu; na wale waombezi wa kubuni watakanushwa na kukataliwa. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 718 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa watakaostahiki kupata shufaa na uombezi wa waja wake wema Siku ya Kiyama. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

 

Tags