Jan 24, 2017 09:15 UTC

Sura ya Ar-Rum, aya ya 14-19 (Darsa ya 719)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 719 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 30 ya Ar-Rum. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 14, 15 na 16 ambazo zinasema:

وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ يَوْمَئِذٍ يَتَفَرَّقُونَ

Na siku itakapo simama Saa (ya Kiyama), siku hiyo watagawanyika.

فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فَهُمْ فِي رَوْضَةٍ يُحْبَرُونَ

Ama wale walio amini na wakatenda mema watakuwa katika Bustani wakifurahishwa.

وَأَمَّا الَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَلِقَاء الآخِرَةِ فَأُولَئِكَ فِي الْعَذَابِ مُحْضَرُونَ

Na ama wale walio kufuru na wakazikanusha Ishara zetu na mkutano wa Akhera, hao basi watahudhurishwa katika adhabu.

Aya hizi zinawagawa watu makundi mawili kutokana na jinsi watakavyokuwa Siku ya Kiyama. Kundi la kwanza ni la watu waliokuwa waumini na watenda mema; na kundi jingine ni la watu ambao matendo yao yalisimama katika msingi wa ukafiri na kuikana haki. Mambo mengine yote ambayo yaliwapambanua na kuwatafautisha watu duniani na kuwafanya wawe makundi na matabaka mbalimbali kama umri, elimu, jinsia, rangi, lugha, mali na vyeo, vyote hivyo havitakuwa na taathira yoyote siku hiyo. Kitu pekee kitakachotafautisha hatima ya mtu mmoja na mwingine ni kuamini au kukufuru kwake ambako kulifuatiwa na amali zake njema au mbaya. Nukta ya kutafakari hapa ni kwamba ili kuingia peponi, imani tupu haitoshi bali lazima imani hiyo ifuatishwe na amali njema na za kheri; lakini kukufuru na kukanusha tu kunatosha kumfanya mtu aingie motoni. Kwa sababu kukufuru na kuikana haki ni dhulma kubwa kabisa ambayo mtu anaifanyia nafsi yake na rasilimali ya uhai ambayo Allah amemtunukia mwanadamu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Siku ya Kiyama ni siku ya kupambanuka na kutengana waja safi na wachafu na watu wema na wale walio wabaya na waovu. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tendo jema lenye thamani ni lile lililofanywa kwa nia ya kupata radhi za Allah SW na ambalo limetokana na imani ya mtu juu ya Mola. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kukadhibisha aya za Mwenyezi Mungu na Siku ya Kiyama kunatokana na hulka ya inadi na ukanushaji iliyomo katika nafsi ya mtu. Vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba hatima ya mwanadamu huko akhera imefungamana na matendo yake katika maisha ya hapa duniani.

Ifuatayo sasa ni aya ya 17 na 18 ambazo zinasema:

فَسُبْحَانَ اللَّهِ حِينَ تُمْسُونَ وَحِينَ تُصْبِحُونَ

Basi msabihini Mwenyezi Mungu mnapofikia jioni na mnapofikia asubuhi,

وَلَهُ الْحَمْدُ فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَعَشِيًّا وَحِينَ تُظْهِرُونَ

Na sifa zote njema ni zake katika mbingu na ardhi, na jioni na mnapofikia mchana.

Baadhi ya wafasiri wa Qur'ani wanaitakidi kuwa aya hizi zinaashiria nyakati za Sala za faradhi zinazopasa kusaliwa katika nyakati za mchana na usiku kwa kueleza kwamba: Mdhukuruni Mwenyezi Mungu wakati wa asubuhi na usiku na mchana na jioni na muwe mkimhimidi na kumsabihi; kwa sababu vyote vilivyomo katika ulimwengu mzima wa maumbile vinakiri na kushuhudisha adhama, utakasifu na utukukaji wake na vyote hivyo ni ishara ya elimu na uwezo wake usio na kikomo. Naam; ili kujiweka mbali na shirki, inapasa tuwe tunamsabihi Allah katika hali zote na kumtakasa kwa moyo na ulimi kuwa hana mshirika yeyote wala hana ila na kasoro yoyote ile. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kumhimidi na kumsabihi Mwenyezi Mungu mtukufu katika nyakati zote na mwahala mote (mbinguni na ardhini) ni amali njema na ya thamani. Pamoja na hayo baadhi ya nyakati ni mwafaka zaidi kwa ajili ya kumdhukuru Allah SW. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kumsabihi na kumtakasa Mwenyezi Mungu na kila aina ya ila na kasoro ni utangulizi wa kumhimidi na kumshukuru Yeye Mola. Kwa sababu hiyo kumsabihi na kumtakasa kumetangulia kumhimidi na kumshukuru Yeye Allah SW.

Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 19 ambayo inasema:

یخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَيُحْيِي الأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا وَكَذَلِكَ تُخْرَجُونَ

Hukitoa kilicho hai kutokana na kilicho kufa, na hukitoa kilicho kufa kutokana na kilicho hai. Na huihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Na kama hivyo ndivyo mtakavyo fufuliwa. 

Aya hii inatoa jawabu kwa shubha na shaka wanazozusha watu wanaokanusha ma'adi na kufufuliwa viumbe kwa kuashiria mifano kadhaa ya kufufuliwa na kupewa uhai tena vitu vyenye uhai vilivyofishwa hapa duniani kwa kueleza kwamba: Vipi mnaona ni jambo baidi na muhali kufufuliwa tena wafu Siku ya Kiyama ilhali Mwenyezi Mungu muda wote yuko katika hali ya kuhuisha na kufisha viumbe. Wakati wa msimu wa baridi miti na mimea hufa na wakati wa msimu wa machipuo huhuika tena; na hali hii inajirudia na kujikariri kila mwaka na mnajionea nyinyi wenyewe kwa macho yenu. Isitoshe ni kwamba kila mwaka kutoka kwenye ardhi isiyo na uhai huchipua na kuonesha uhai anuai za miti na mimea kama ambavyo viumbe chungu nzima vyenye uhai hupoteza uhai wao na kugeuka mchanga.

Maji na chakula tunachokula si vitu vyenye uhai. Lakini wakati tunapovila na kuvinywa hugeuka vikawa sehemu ya miili yetu kwa kubadilika kuwa seli hai. Katika mfumo wa maumbile pia daima viumbe hai hutoka kwenye vitu visivyo na uhai na vitu vyenye uhai huishia kuwa vitu visivyo na roho wala uhai. Na huu ni ushahidi bora kabisa wa kuthibitisha nguvu na uwezo wa Mola Muumba wa kuwahuisha na kuwafufua tena waliokufa Siku ya Kiyama.

Tab'an aya hii inaweza kufasiriwa pia katika sura na mtazamo wa kimaanawi. Ni kama ilivyoelezwa katika baadhi ya hadithi, kwamba kuzaliwa mtu muumini kutoka kwa mzazi kafiri na mtu kafiri kutokana na mja muumini, au mtu aalimu kutoka kwenye kizazi cha watu wajinga na majahili au mtu mjinga kutoka kwenye kizazi cha watu wenye elimu ni mifano ya vihai vinavyotoka kwenye wafu na wafu wanaotokana na vilivyo hai. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba ikiwa mwanadamu atakuwa na insafu na busara hatobakiwa na chembe ya shaka ya kuamini Kiyama na kufufuliwa viumbe huko akhera. Kwa sababu Mwenyezi Mungu SW ameshaonesha katika dunia hii nguvu na uwezo wake wa kufisha na kuhuisha viumbe. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa katika mfumo wa ulimwengu huu unashuhudiwa mzunguko na mabadiliko ya viumbe kutoka hali ya uhai na mauti; na hili ni jambo linaloendelea mpaka Siku ya Kiyama. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 719 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuhuishe katika kalima ya tauhidi, atufishe katika kalima ya tauhidi na atutufue katika kalima ya tauhidi. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags