Jan 24, 2017 09:20 UTC

Sura ya Ar-Rum, aya ya 20-22 (Darsa ya 720)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwingine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 720 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 30 ya Ar-Rum. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 20 ambayo inasema:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَكُم مِّن تُرَابٍ ثُمَّ إِذَا أَنتُم بَشَرٌ تَنتَشِرُونَ

Na katika Ishara zake ni kuwa kakuumbeni kwa udongo. Kisha mmekuwa watu mlio tawanyika kote kote.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya ambazo ziliashiria nguvu na uwezo wa Allah SW wa kufufua wafu na kufisha walio hai. Aya hii na nyingine kadhaa zinazofuatia zinazungumzia nguvu na uwezo wa Mola Mwenyezi katika kuumba viumbe na hasa mwanadamu. Kwa kuanzia aya inasema: Asili ya uwepo wenu nyote nyinyi wanadamu ambao leo hii mumeenea katika sayari yote ya dunia ni udongo usio na uhai. Aya hii wapenzi wasikilizaji inaweza kuwa inaashiria uumbwaji wa mwanadamu wa mwanzo kutokana na udongo, uumbaji ambao umezungumziwa katika baadhi ya aya za Qur'ani, na vilevile inaweza kuwa inaashiria chakula cha mwanadamu ambacho mada zake zinatokana kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja na udongo na ardhi. Na kwa msingi huo tunaweza kusema, ujudi na uwepo wa mwanadamu unatokana na udongo.

Ikiwa mwanadamu atatafakari na kuzingatia uumbwaji wake na maisha yake ataona ni vipi Muumba wa ulimwengu aliweza kuumba kutokana na udongo usio na roho wala uhai seli makini za ubongo ambao maendeleo yote ya sayansi na fani mbalimbali aliyopata na anayoendelea kupata mwanadamu ni matunda yanayotokana na ubongo huo.

Udongo, ambao hauna harakati, hisi wala uelewa umepitia kwenye mabadiliko ya kimiujiza na kugeuka kuwa seli ambazo zinamfanya mwanadamu kuwa ni kiumbe mwenye uelewa, hisi na harakati; na hili ni jambo la muujiza mkubwa mno. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kujijua na kujitambua mtu nafsi yake ni utangulizi wa kumjua Mola na Muumba wake; na mwanadamu ni moja ya madhihirisho ya wazi kabisa ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu SW katika sayari ya dunia. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa sisi wanadamu wote tunatokana na udongo na tutageuka tena kuwa udongo. Kwa hivyo tuache kujifaharisha kwa mambo yasiyo na thamani; wala tusiingiwe na ghururi na kiburi.

Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 21 ambayo inasema:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً إِنَّ فِي ذَلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ

Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri. 

Baada ya maudhui ya uumbwaji wa mwanadamu, aya hii tuliyosoma imeashiria moja ya ishara kubwa za Allah SW ambayo ni kanuni ya ndoa na kueleza kwamba: Mwenyezi Mungu amemwekea kila mtu mwenza wa kuwa mshirika na msaidizi wake katika maisha na kuweza kupata utulivu kutokana na kuwa kando yake. Mfungamano kama huo hupatikana kwa mahaba na mapenzi yanayojengeka baina ya mke na mume ambayo ni majaaliwa ya Mola na ambayo huwa sababu ya kuwepo utegemeano na upendo baina yao katika umri wao wote. Mfungamano wa ndoa huwafanya mume na mke kila mmoja awe mkamilishi wa mwenzake na kuwapa wawili hao uchangamfu na ukunjufu wa maisha. Ni hakika kabisa kuwa moja ya athari muhimu za mfungamano wa ndoa ni kuongezeka kizazi na kudhamini kuendelea kuwepo kizazi cha wanadamu. Mfungamano wa ndoa vilevile ni msingi wa kujenga jamii na kuwafanya watu wawe wawajibikaji wa kubeba majukumu ya kijamii. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa mwanamke na mwanamme wanatokana na asili moja. Ni kinyume na baadhi ya mitazamo potofu na batili inayomchukulia mwanamke kuwa ni kiumbe duni kulinganisha na mwanamme. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa katika utamaduni na mafundisho ya Uislamu familia maridhawa na inayokubalika ni ile ambayo kila mmoja kati ya mke na mume huwa ni chachu ya utulivu na faraja kwa mwenzake na si sababu ya kutiana tafrani, kuudhiana na kugombana. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba huruma na upendo ni hidaya ya Allah kwa mke na mume ambayo huifanya ndoa yao idumu na kunawirika. Wa aidha tunajielimsha kutokana na aya hii kuwa kama ambavyo upendo na mahaba ni sababu ya kuanzishwa mfungamano baina ya wanandoa, mahaba na mapenzi hayohayo yanahitajika ili kuyafanya maisha hayo ya pamoja yadumu na kuimarika.

Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 22 ambayo inasema:

وَمِنْ آيَاتِهِ خَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاخْتِلافُ أَلْسِنَتِكُمْ وَأَلْوَانِكُمْ إِنَّ فِي ذَلِكَ لَآيَاتٍ لِّلْعَالِمِينَ

Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na kutafautiana ndimi zenu na rangi zenu. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa wajuzi.

Aya hii imefuatanisha uumbwaji wa mwanadamu na kuumbwa kwa mbingu na ardhi ili kiumbe huyo, mbali na kujiangalia nafsi yake mwenyewe, atafakari na kuzingatia pia ulimwengu uliomzunguka. Licha ya kuwepo anuai za satalaiti na darubini za kisasa kabisa, mwanadamu bado hajaweza kuwa na ujuzi na utambuzi wa kina kuhusu mbingu pamoja na chungu ya sayari na maumbo mbalimbali yaliyoko angani na anakiri juu ya adhama ya uumbaji wa mbingu na vilivyoko ndani yake. Ardhi nayo pia ina maajabu chungu nzima ambayo mengi yao mwanadamu hajaweza kuyatambua. Ndani ya kina cha tumbo la ardhi kuna dafina na hazina chungu nzima. Kwenye ardhi kwenyewe kuna mafuta, gesi na anuai nyingine za madini; na katika vina vikubwa vya bahari kuna anuai za samaki na viumbe vingine vingi vya majini ambavyo vina faida na manufaa mengi mno kwa mwanadamu. Kisha aya inaendelea kwa kumrudia tena kiumbe mwanadamu na kuashiria sifa zake maalumu mbili muhimu na kusema: Tofauti za lugha zimewezesha kuwepo lahaja mbalimbali; na tofauti za rangi zimewezesha kuwepo watu wa mbari na rangi na asili tofauti. Hebu fikiria, laiti kama watu wote wangekuwa na sura, umbo na rangi namna moja; na lugha na sauti zinazofanana, ingewezekanaje kumtambua na kumpambanua mtu mmoja na mwingine? Ni vipi mtoto angeweza kumtambua baba na mama yake kati ya maelfu ya wanaume na wanawake wenye umri na rika moja? Wanandoa nao wangewezaji kutambuana?

Kwa hakika tofauti hizi za sura na lugha ni njia bora kabisa ya kuwafanya watu wajuane na kutambuana. Isitoshe ni kwamba laiti kama hali hii ya anuwai na tofauti zote hizi zisingekuwepo, maisha katika jamii ya wanadamu yangechosha kutokana na kuwa ya hali namna moja tu. Ni kama kuingia katika mji wa watu kisha ukakuta gari zote za mji mzima ni za rangi moja na za aina moja. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mbali na sayansi za jarabati kumsaidia mwanadamu kunufaika zaidi na ulimwengu wa maumbile inapasa zimsaidie pia kujenga na kukuza imani yake juu ya Muumba wake Mweza na Mwenye hekima. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa katika mtazamo wa maulamaa na watu walioelimika kuwepo anuwai za mbari, rangi na lugha baina ya watu ni alama na ishara ya adhama na uwezo wa Mola Muuumba. Lakini kwa uoni wa watu wajinga na majahili tofauti hizo ni hoja tosha za kumfanya mtu mmoja amdunishe na kumkejeli mwenzake na kujikweza na kujifaharisha mbele yake. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba kila lugha ina asili, hadhi na thamani. Kwa hivyo mtu yeyote hana haki ya kudharau, kudunisha na kukejeli lugha na watu wa rangi na makabila mengine. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 720 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa wale wanaowaenzi watu kutokana na imani na matendo yao, si kwa asili na dhahiri yao. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags