Jan 24, 2017 09:23 UTC

Sura ya Ar-Rum, aya ya 23-26 (Darsa ya 721)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwingine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 721 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 30 ya Ar-Rum. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 23 na 24 ambazo zinasema:

وَمِنْ آيَاتِهِ مَنَامُكُم بِاللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَابْتِغَاؤُكُم مِّن فَضْلِهِ إِنَّ فِي ذَلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَسْمَعُونَ

Na katika Ishara zake ni kulala kwenu usiku na mchana, na kutafuta kwenu fadhila zake. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao sikia.

وَمِنْ آيَاتِهِ يُرِيكُمُ الْبَرْقَ خَوْفًا وَطَمَعًا وَيُنَزِّلُ مِنَ السَّمَاء مَاء فَيُحْيِي بِهِ الأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا إِنَّ فِي ذَلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ

Na katika Ishara zake hukuonyesheni umeme kwa kukutieni khofu na tamaa. Na hukuteremshieni maji kutoka mbinguni, na kwa hayo huihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao zingatia.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa katika aya kadhaa za sura hii ya Ar-Rum, Qur'ani tukufu imetaja alama na ishara za Allah SW katika uumbaji wa mwanadamu na ulimwengu. Aya hizi tulizosoma zinaashiria mifano mingine miwili ya ishara hizo katika maisha ya mwanadamu na kueleza kwamba: Pengine usingizi na kulala unaweza kuonekana jambo la kawaida kwenu nyinyi lakini kulala na kuamka huko kunakotokea kwa sura ya kupishana usiku na mchana ni katika ishara za hikma ya Mwenyezi Mungu, ili pale mwanadamu anapokuwa amechangamka na mwenye ukunjufu wa moyo afanye kazi na kujishughulisha na harakati za maisha, na pale anapokuwa amechoka aweze kupumzika. Laiti kama mtu asingeweza kulala na kupata usingizi, angekuwa muda wote anahisi machofu na hali ya ulegevu na unyong'onyevu wala asingekuwa na uchangamfu na ukakamavu anaotakiwa kuwa nao kwa ajili ya kuendelea na harakati za maisha.

Radi na umeme unaoshuhudiwa mbinguni, ambao baadhi ya wakati unazitia woga na hofu nyoyo za watu, nao pia ni utangulizi wa kunyesha mvua ambayo inategemewa kwa ajili ya maisha ya ardhini ya watu, wanyama na mimea. Kama itatokea eneo fulani kukosa mvua kwa muda mrefu, wakaazi wa eneo hilo hudiriki na kufahamu barabara umuhimu na thamani ya chanzo hicho cha uhai. Leo hii tunashuhudia mabilioni ya dola zinatumika kugharamia ujenzi, ufungaji na utunzaji mabomba pamoja na uchimbaji mashimo ya chini kwa chini kwa ajili ya kusambaza mafuta na gesi kutoka kwenye viwanda vya kusafishia nishati hizo hadi kwenye miji na vijiji. Lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mrehemevu ameuweka mfumo wa maumbile, wa upepo kusukuma mawingu yanayosababisha kunyesha mvua zinazotoa maji ya mito, maziwa na bahari yanayotumiwa bila ya gharama wala malipo yoyote na wakaazi wa ardhini. Kwa hivyo inapasa tukae na kutafakari juu ya neema hizi zisizokadirika za Allah SW ili tuwe washukurivu kwa atiya na rehma za Mola kwetu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tusizipite vivi hivi neema za Allah. Mfumo wa kulala na kuamka ni miongoni mwa neema kubwa za Mola. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kufanya kazi na kuhangaika kutafuta riziki ya halali ili kukidhi mahitaji ya maisha ni jambo jema na lenye kuhimizwa na kusisitizwa na dini. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba umeme tunaoshuhudia mbinguni, mvua zinyeshazo kutoka angani, na mimea inayochipua na kuota ardhini, si mambo yanayotokea kwa bahati tu. Matukio yote hayo ya kimaumbile yanajiri kwa kufuata mpango makini na ulioratibiwa kwa mahesabu kamili na Mola Muumba wa ulimwengu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa kumjua Mwenyezi Mungu kunapasa kutokane na elimu, kutafakari na kutumia akili.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 25 ya sura yetu hii ya Ar-Rum ambayo inasema:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَن تَقُومَ السَّمَاء وَالأَرْضُ بِأَمْرِهِ ثُمَّ إِذَا دَعَاكُمْ دَعْوَةً مِّنَ الأَرْضِ إِذَا أَنتُمْ تَخْرُجُونَ

Na katika Ishara zake ni kuwa mbingu na ardhi zimesimama kwa amri yake. Kisha atakapo kuiteni mwito mmoja tu, hapo mtatoka kwenye ardhi.

Katika aya zilizotangulia umezungumziwa uumbwaji wa mbingu na ardhi. Aya hii ya 25 inaashiria kudumu na kuendelea kubaki viwili hivyo kwa kueleza kwamba maumbo makubwa makubwa ya mbinguni, ambayo mwanadamu bado hajaweza kubaini hakika yake kwa undani kabisa – licha ya kugundua mamilioni ya nyota na sayari – yamo katika hali ya mwendo na mzunguko unaofuata mfumo maalumu; na endapo utatokea mkengeuko mdogo kabisa wa kutoka nje ya njia yake yanaweza kusababisha sehemu moja ya ulimwengu kuangamia ikiwemo sayari ya dunia pamoja na wakaazi wake. Lakini tadbiri na uendeshaji mambo wa Mola Muumba ni wa namna ambayo maumbo yote hayo yasiyohesabika yanatembea na kuzunguka kupitia njia maalumu chini ya kanuni ya mvuto na msukumo na kuufanya mfumo wa ulimwengu uendelee kubaki thabiti kama ulivyo. Na bila ya shaka atakapotaka Yeye Mola mfumo huo utasambaratika na dunia hii itafikia mwisho wake na mfumo wa ulimwengu mwingine utasimama na kuchukua nafasi yake. Katika mfumo huo mpya, kinyume na dunia hii ambapo watu wanazaliwa kutoka matumboni mwa mama zao, wanadamu watachipuka mithili ya mimea kutokea ardhini; na pasina kuwa na uhusiano na baba, mama, dada, kaka au jamaa zake wa duniani, kila mtu atahudhurishwa katika ulimwengu huo akiwa peke yake na atakwenda kujibu kuhusu amali na matendo yake aliyofanya katika dunia hii. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kuendelea kubaki thabiti mfumo wa ulimwengu wa maumbile hakutokei kwa bahati tu wala hakufanywi na mwengine yeyote, ghairi ya irada ya Allah tu SW. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa si uumbaji pekee bali tadbiri, upangaji na uendeshaji mambo yote ya ulimwengu uko mikononi mwa Mola Muumba. Si kwamba Yeye ameuumba tu ulimwengu kisha akauacha kama ulivyo; bali mfano wake Yeye ni kama mwenye konde, ambaye mbali na kupanda mbegu hushughulikia pia upaliliaji wake mpaka uchumaji na uvunaji wake. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba kutoka wanadamu kwenye udongo ni hoja na ushahidi wa kuthibitisha kuwa maadi na kufufuliwa viumbe kutakuwa kwa sura ya kiwiliwili, si kiroho tu, maana baada ya kufariki ni mwili wa mwanadamu unaoingia ardhini, si roho yake!

Tunaihatimisha darsa yetu ya leo kwa aya ya 26 ambayo inasema:

وَلَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ كُلٌّ لَّهُ قَانِتُونَ

Na vyake Yeye vilivyoko mbinguni na katika ardhi. Vyote vinamt'ii Yeye

Aya hii inaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia kuhusu kuondolewa mwanadamu katika ulimwengu huu na kupelekwa ulimwengu mwingine na kueleza kwamba, kwa kuwa Mwenyezi Mungu SW ndiye mwenye umiliki wa kiumbe mwanadamu pamoja na viumbe wengine kama malaika na majini, ana haki ya kufanya lolote atakalo kuhusiana na viumbe wake hao na hakuna yeyote mwenye uwezo wa kupingana naye. Kwa sababu japokuwa upo uwezekano wa viumbe hao kwenda kinyume na mfumo wa upangaji sharia uliowekwa na Yeye Mola lakini nafsi na ujudi wao unatii na kufuata mfumo wa maumbile aliouweka. Kwani hata hiyari na mamlaka waliyonayo viumbe inatokana na irada na idhini ya Allah SW. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba si vitu visivyo na uhai, mimea na wanyama pekee, bali hata viumbe wenye hisi za uelewa na ufahamu kama wanadamu, malaika na majini nao pia hawana uwezo wa kutoka nje ya mamlaka ya utawala wa Mwenyezi Mungu. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kama ambavyo katika mfumo wa maumbile, nafsi na ujudi wa mwanadamu unamtii Muumba wake na kwa sababu hiyo unafikia kwenye ukamilifu wa kimwili, katika mfumo wa upangaji sharia pia, ikiwa mwanadamu ataamua kwa hiyari yake kufuata na kutii amri za Mola atafikia ukamilifu wa kiroho na saada ya milele. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 721 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwezeshe kuwa washukurivu wa kweli wa neema zake, kubwa na ndogo, tunazozijua na tusizozijua. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/   

 

Tags