Jan 24, 2017 09:31 UTC

Sura ya Ar-Rum, aya ya 30-34 (Darsa ya 723)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwingine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 723 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 30 ya Ar-Rum. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 30 ambayo inasema:

فَأَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ حَنِيفًا فِطْرَةَ اللَّهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا لا تَبْدِيلَ لِخَلْقِ اللَّهِ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لا يَعْلَمُونَ

Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini - ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilo waumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo Dini iliyo nyooka sawa. Lakini watu wengi hawajui.

Katika darsa kadhaa zilizopita tulisoma aya zilizozungumzia ishara kadhaa za kuwepo Mwenyezi Mungu pamoja na uwezo na nguvu zake Mola katika uumbaji wa mbingu na ardhi. Aya tuliyosoma inasema: Mbali na yanayoshuhudiwa katika mfumo wa vitu vya maumbile, mwanadamu anapozingatia batini na fitra yake mwenyewe pia humfikisha kwenye utambuzi wa kumjua Mola wake. Kwa sababu batini ya wanadamu wote inashuhudia uwepo wa Mola Muumba, Mweza na Aliyetukuka. Katika aya hii ya 30 ya Suratu Rum Allah SW anamtaka Bwana Mtume SAW na waumini wote wasiiamini dini na itikadi ya haki kidhahiri na kwa ndimi zao tu bali waikubali kwa nyoyo na batini zao na kujiweka mbali na kila aina ya upotofu. Ni hakika iliyo wazi kabisa kwamba dini zote za Tauhidi zimeletwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu, lakini akthari yao zimepotoshwa na kukengeuka mkondo na njia yake halisi ambayo ni kuwaongoza na kuwafikisha watu kwenye saada. Aya hii inasema: Dini pekee ambayo imebaki thabiti, imara na ambayo mafundisho yake ya asili hayakupotoshwa ni Uislamu; dini ambayo inawiyana pia na fitra na maumbile ambayo Allah amemuumbia mwanadamu. Kama ambavyo dhati ya maumbile ya mwanadamu haibadiliki katika zama zote, bali watu wote wa zama na mahala popote wana dhati moja ya maumbile ya kiutu, yale ambayo Allah SW ameyateremsha kwa ajili ya saada ya mwanadamu pia yako thabiti na hayabadiliki na yamedhihiri katika dini ya Uislamu, ambayo ni dini ya mwisho ya mbinguni na ya Tauhidi. Pamoja na hayo akthari ya watu wameghafilika na ukweli huu. Kwani badala ya kushikamana na kufuata njia ya Uislamu wanaamua kufuata nadharia zilizobuniwa na wanadamu ambazo zimejaa kasoro na migongano au kufuata dini ambazo zimepotoshwa na kukengeuka njia sahihi ya asili na kuwafanya wasiifikie saada waliyokusudiwa. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Mwenyezi Mungu ameiumba dhati ya mwanadamu kwa namna ya kuwa na hamu ya kupenda haki na kuchukia batili. Dini ya Tauhidi pia imesimama juu ya msingi wa haki; na kuvutiwa nayo kunatokana na fitra na maumbile asili ya mwanadamu. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kitu ambacho ni cha fitra na maumbile kinahitaji kuzingatiwa na kufanyiwa kazi, la sivyo mtu atakisahau na kughafilika nacho. Asili ya dini ni kitu cha maumbile lakini inapasa ishughulikiwe kwa mafunzo na mafundisho ili ikite na kudumu ndani ya nafsi zetu. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba mfumo wa hali ya maumbile ya mwanadamu unawiyana na mfumo wa sharia alizowekewa na Mwenyezi Mungu, kwa sababu vyote viwili vinatokana na asili moja na wala hakuna mgongano wowote baina yao.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 31 na 32 ambazo zinasema:

مُنِيبِينَ إِلَيْهِ وَاتَّقُوهُ وَأَقِيمُوا الصَّلاةَ وَلا تَكُونُوا مِنَ الْمُشْرِكِينَ

Muwe wenye kutubia Kwake, na mcheni Yeye, na shikeni Sala, na wala msiwe katika washirikina.

مِنَ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعًا كُلُّ حِزْبٍ بِمَا لَدَيْهِمْ فَرِحُونَ

Katika wale ambao kwamba wameigawanya dini yao, na wakawa makundi makundi, kila kundi wanafurahia waliyo nayo.

 Katika aya iliyopita tulisema kuwa japokuwa dini ni jambo la fitra na maumbile lakini muda wote kuna hatari ya mtu kuisahau na kughafilika nayo. Kwa sababu hiyo aya tulizosoma zinasema: Wakati wowote ikitokezea kughafilika au kukengeuka njia ya dini basi rudini kwa Mwenyezi Mungu ambako ni kurejea kwenye ileile dhati yenu ya Tauhidi. Kisha zinatoa amri na miongozo kadhaa kwa ajili ya kuilinda dini. Wa kwanza ni kuchunga taqwa na kujiepusha na madhambi na mwingine ni kuendeleza mahusiano na mawasiliano na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sala na dua; kwani endapo misingi hii miwili itazingatiwa mtu hatotumbukia kwenye lindi la shirki katika imani na amali zake. Kisha aya zinaendelea kwa kuashiria moja ya matokeo ya shirki kwa kusema: Shirki huigawa mapande jamii ya wanadamu; kwani kila mtu hukifurahia na kukielekea kwa maombi kile au yule anayemdhania kuwa mshirika wa Allah ili kupata saada na fanaka ya maisha. Hali ya kuwa, kama wanadamu wote wataungana pamoja kiimani na kimatendo katika mhimili wa Tauhidi hazitatokea hitilafu wala migongano yoyote katika jamii bali umoja na mshikamano utatawala katika jamii ya wanadamu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mvuto wa kifitra na kimaumbile wa dini huchanua na kustawi ndani ya nafsi ya mwanadamu pale yeye anapokuwa mtu wa dua na toba na taqwa na Sala. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Tauhidi ni sababu ya kupatikana umoja na mshikamano katika jamii ya wanadamu; na shirki ni sababu ya migawanyiko na mifarakano baina yao. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kuzusha mifarakano na migawanyiko katika jamii ni alama na ishara ya kuwa mbali na njia ya Tauhidi na kutumbukia kwenye shirki.

Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 33 na 34 za sura yetu ya Ar-Rum ambazo zinasema:

وَإِذَا مَسَّ النَّاسَ ضُرٌّ دَعَوْا رَبَّهُم مُّنِيبِينَ إِلَيْهِ ثُمَّ إِذَا أَذَاقَهُم مِّنْهُ رَحْمَةً إِذَا فَرِيقٌ مِّنْهُم بِرَبِّهِمْ يُشْرِكُونَ

Yakiwapata watu madhara humwomba Mola wao Mlezi nao wametubu kwake. Kisha akiwaonjesha rehema itokayo kwake, mara kikundi miongoni mwao humshirikisha Mola wao Mlezi,

لِيَكْفُرُوا بِمَا آتَيْنَاهُمْ فَتَمَتَّعُوا فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ

Ili wapate kuyakana tuliyo wapa. Basi stareheni. Mtakuja jua! 

Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa na aya za kabla yake kuhusu kumjua Mwenyezi Mungu na Tauhidi kwamba hilo ni suala la fitra na maumbile kwa kuashiria moja ya mifano ya jambo hilo katika maisha ya mwanadamu na kueleza kuwa: Wakati wowote mtu anapofikwa na msiba na masaibu ikawa hakuna mtu yeyote mwenye uwezo wa kumsaidia na akawa amekata tamaa na kupoteza matumaini kikamilifu hapo humuelekea Mwenyezi Mungu na kumwomba amtatulie masaibu na matatizo yaliyomtinga. Anapokuwa katika hali hiyo mwanadamu hukikumbuka kile alichokuwa amekisahau kutokana na mghafala. Na kwa njia hiyo hutubia kutokana na mghafala uliokuwa umempata na pia humtaradhia Allah amtatulie masaibu na matatizo yaliyomfika. Lakini baada ya kuteremkiwa na rehma za Mola na kutatuliwa yaliyokuwa yakimtatiza humsahau tena Mwenyezi Mungu na kuwaona watu au vitu vingine kuwa ndivyo vilivyomtatulia matatizo na masaibu aliyokuwa nayo. Endapo hali hiyo ya utovu wa shukurani itaendelea katika maisha yake, hatimaye mtu huwa na mwisho mbaya. Kwani hata kama atafaidika na neema za kidunia lakini hatima yake haiwi ya mwisho mwema. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuna baadhi ya watu wanamjua na wanamkumbuka Mwenyezi Mungu wakati wa shida na misiba, utadhani Mungu ni wa kuwatatulia matatizo yao tu; hivyo kama hawatokuwa na shida wala tatizo huwa hawana haja wala hawamhitajii Yeye Mola. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa wakati wa shida na dhiki vumbi la mghafala huondoka, na mtu hurudi kwenye fitra na asili yake ambayo ni kumjua Mwenyezi Mungu. Aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba raha na uneemevu wa maisha huweza kumfanya mtu amsahau Mwenyezi Mungu na kuishia kwenye kufru na utovu wa shukrani kwa Mola wake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 723 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah ajaalie neema alizotupa na anazoendelea kutupa ziwe sababu ya kumdhukuru na kumshukuru badala ya kughafilika naye na kumkufuru. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags