Jan 24, 2017 09:37 UTC

Sura ya Ar-Rum, aya ya 35-38 (Darsa ya 724)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwingine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 724 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 30 ya Ar-Rum. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 35 ambayo inasema:

أَمْ أَنزَلْنَا عَلَيْهِمْ سُلْطَانًا فَهُوَ يَتَكَلَّمُ بِمَا كَانُوا بِهِ يُشْرِكُونَ

Au tumewateremshia wao hoja inayowaambia juu ya yale wamshirikishayo nayo?

Aya hii inaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya tulizosoma kwenye darsa iliyopita ya kuvunja hoja za shirki na itikadi za washirikina kwa kuhoji kwamba: Je, washirikina wanaomfanyia Mwenyezi Mungu mshirika wana hoja na ushahidi wa kuthibitisha jambo hilo? Katika mfumo wa maumbile au katika nafsi zao wenyewe wamegundua ishara zinazoonesha kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ana mshirika? Au kuna kitabu ambacho Mwenyezi Mungu ameteremsha na ndani yake amekiri kwa kusema Mimi nina mshirika? Ni wazi kwamba hakuna lolote lililotokea kati ya hayo bali washirikina wanafuata imani na itikadi hiyo potofu kwa kung'ang'ania kijahili na kitaasubi njia iliyokuwa ikifuatwa na wazee wao waliowatangulia na wala hawana hoja yoyote ya kimantiki wala kimapokeo ya kuthibitishia imani yao hiyo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Uislamu ni dini ya mantiki na hoja, inayotoa changamoto ya kuwataka wapinzani wake wathibitishe madai yao kwa hoja. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kinyume na Tauhidi ambayo ina hoja imara na zenye ushahidi wa kina, shirki haina mashiko wala hoja zozote za kimantiki.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 36 ambayo inasema:

وَإِذَا أَذَقْنَا النَّاسَ رَحْمَةً فَرِحُوا بِهَا وَإِن تُصِبْهُمْ سَيِّئَةٌ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ إِذَا هُمْ يَقْنَطُونَ

Na watu tunapo waonjesha rehema huifurahia, na ukiwasibu uovu kwa iliyo yatanguliza mikono yao wenyewe, mara wanakata tamaa. 

Aya tuliyosoma inaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia kwa kutaja sifa nyingine ya washirikina na watu wenye imani dhaifu kwamba wao ni watu walio katika hali ya baina ya ghururi na kukata tamaa. Wakati wanapojaaliwa neema huingiwa na ghururi na wakati wanapofikwa na matatizo hukata tamaa na kupoteza matumaini. Hali ya kuwa waumini wa kweli huwa kwenye katika hali ya baina ya subira na ushukurivu. Ni wenye kumshukuru Mola wao kwa neema anazowapa na huwa na subira na uvumilivu kwa matatizo na misukosuko inayowafika. Nukta ya kutaamali na kuzingatia hapa ni kwamba katika aya hii na nyingine zinazofanana na hii, neema zinatajwa kuwa ni rehma itokayo kwa Allah, lakini kinyume chake, masaibu na mabalaa yanaelezwa kuwa yanatokana na matendo yetu wenyewe. Na sababu ni kwamba Mwenyezi Mungu SW hawatakii waja wake kitu kingine zaidi ya rehma na fadhila zake; na mengi ya matatizo na masaibu yanayomfika mwanadamu yanatokana na tabia na mwenendo wake usio sahihi au dhulma anayowafanyia wanadamu wenzake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba uwezo wa kinafsi wa watu wasio na imani au wenye imani dhaifu huwa ni mdogo. Wapatapo neema kidogo tu hujawa na ghururi na wafikwapo na machungu na masaibu madogo tu hukata tamaa na kupoteza matumaini. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mwanadamu hatakiwi kutekwa na kujisahau kwa neema za kidunia kwa sababu si za kudumu wala si za kuendelea. Hivyo pale zitakapomwondokea ataishia kukata tamaa na kupoteza matumaini.

Darsa ya 724 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 37 na 38 ambazo zinasema:

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّهَ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاء وَيَقْدِرُ إِنَّ فِي ذَلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ

Kwani hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye na humdhikisha amtakaye? Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao amini.

فَآتِ ذَا الْقُرْبَى حَقَّهُ وَالْمِسْكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ ذَلِكَ خَيْرٌ لِّلَّذِينَ يُرِيدُونَ وَجْهَ اللَّهِ وَأُولَئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

Basi mpe jamaa haki yake, na masikini, na mwananjia. Hayo ni kheri kwa watakao radhi ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio wenye kufanikiwa. 

Baada ya aya iliyotangulia kueleza kwamba baadhi ya watu wenye imani dhaifu na uwezo mdogo wa kinafsi huingiwa na ghururi na kujiona wanapopata neema za Mwenyezi Mungu na kupoteza matumaini na kukata tamaa wanapoondokewa na neema hizo, aya hizi zinasema: Watu wenye imani ya kweli ya Allah wanaitakidi kuwa riziki inatokana na Mwenyezi Mungu; na kuwa kwake nyingi au chache kunatokana na elimu na hikima yake Mola. Na ndiyo maana si hasha ukaona watu wanajipinda mgongo kutafuta utajiri lakini wanapata chumo dogo na si ajabu kuwaona watu waliofanya jitihada ndogo za kutafuta chumo lakini wana utajiri mkubwa. Jambo muhimu ni sisi kufanya juhudi na bidii kwa kiwango cha kadiri na kinachokubalika; lakini kwamba matunda ya juhudi zetu yatakuwa ya kiasi gani, hilo linategemea mambo kadha wa kadha ambayo mengi kati yao hayako kwenye mamlaka yetu. Kama tutakuwa tumejitahidi sana kutafuta mali na pato kubwa, lakini tukashindwa kufanikiwa kwa sababu yoyote ile, tusikate tamaa na kujiinamia. Tunatakiwa tuitakidi kwamba jukumu letu sisi ni kufanya juhudi na bidii na kumwachia Allah kile alichokadiria kuhusu matunda ya juhudi zetu, na daima turidhike na tulichonacho wala tusione ni wajibu wa Allah kutupa kila tunachokitaka. Kisha aya zinaendelea kwa kuashiria jukumu na mas-ulia aliyonayo mtu kwa wanadamu wenzake na kueleza kwamba: Bila ya shaka mtu aliyejaaliwa ukunjufu wa riziki ana mas-ulia na jukumu kubwa zaidi na inampasa mbali na familia yake mwenyewe awafikirie pia wahitaji katika jamii, na kipaumbele cha kwanza kiwe kwa ndugu na jamaa zake. Sehemu ya mwisho ya aya inagusia pia dhamira na nia ya utoaji na kueleza kwamba: Bila ya shaka amali hiyo ya kheri itabaki na taathira na malipo mema kwa mtoaji ikifanyika kwa kusudio la kupata radhi za Allah SW, si kutaka kutajika na kutafuta jaha na umaarufu. Isitoshe, ikiwa mtu anatoa kwa ajili ya kupata radhi za Mola hatowasimanga na kuwasimbulia wahitaji anaowasaidia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kama tunaamini kuwa riziki tuliyonayo inatoka kwa Allah hatutofanya ubakhili wa kuwasaidia wanyonge na wahitaji katika jamii. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kama utoaji wa kuwasaidia wahitaji utafanywa bila ya ikhlasi na si kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, anayepewa atanufaika na alichopewa, lakini mtoaji hatopata faida wala malipo yoyote Akhera. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba jamaa na wanyonge wana haki zao katika mali na utajiri wa mtu ambazo inapasa zitolewe kwa namna sahihi. Vilevile tunajifunza kutokana na aya hizi kuwa matajiri, mbali na kutoa Khumsi na Zaka wanapaswa watumie pia mali na utajiri wao kwa ajili ya kuondoa ufakiri katika jamii na wala wasitosheke na utoaji mali uliofaradhishwa kisheria tu. Kadhalika aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba Uislamu unalipa umuhimu maalumu suala la kupambana na hali duni za maisha na kuondoa ufakiri na umasikini katika jamii. Kwa sababu hiyo unawafikiria mno wahitaji, masikni na matabaka ya watu wanyonge. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 724 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azijaze nyoyo zetu ukarimu na ikhlasi tuwe wenye kutoa japo kichache tulichonacho kuwasaidia wanyonge na wahitaji. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags