Jan 24, 2017 09:41 UTC

Sura ya Ar-Rum, aya ya 39-42 (Darsa ya 725)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwingine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 725 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 30 ya Ar-Rum. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 39 ambayo inasema:

وَمَا آتَيْتُم مِّن رِّبًا لِّيَرْبُوَ فِي أَمْوَالِ النَّاسِ فَلا يَرْبُو عِندَ اللَّهِ وَمَا آتَيْتُم مِّن زَكَاةٍ تُرِيدُونَ وَجْهَ اللَّهِ فَأُولَئِكَ هُمُ الْمُضْعِفُونَ

Na mnacho kitoa kwa riba ili kiongezeke katika mali ya watu, basi hakiongezeki mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini mnacho kitoa kwa Zaka kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi hao ndio watao zidishiwa. 

Katika aya ya mwisho tuliyosoma katika darsa iliyopita tulizungumzia suala la utoaji mali kuwasaidia jamaa pamoja na wanyonge na wahitaji. Aya hii ya 39 inalinganisha utoaji unaofanywa kwa ajili ya Allah na usiofanywa kwa ajili yake Yeye Mola na kueleza kwamba: Kile mnachotoa kuwapa watu, kama ni kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu na si kwa nia na kusudio jingine basi malipo yake mtayapata kwa Mola, Naye ni mwenye kuwapa waja wake malipo yasiyokadirika. Lakini kama utoaji wenu na msaada wenu kwa watu si kwa ajili ya Mwenyezi Mungu bali ni kwa lengo na madhumuni mengine kama kutaka mali za watu ziwe nyingi zaidi na sehemu ya mali hizo ikurudieni nyinyi wenyewe, basi hamtopata malipo kwa sababu hamtokuwa mumetoa kwa ajili ya kupata radhi za Allah. Mtu anayetoa mkopo, lakini akawa na tamaa kwa mkopaji ya kumzidishia fedha zaidi wakati wa kulipa deni lake, atakuwa amekidhi hitajio la mwenye shida, lakini kwa sababu lengo lake ni kujiongezea mali hatopata malipo yoyote mbele ya Allah. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba jambo muhimu katika kutoa mali au kukopesha ni nia na dhamira ya mtoaji na mkopeshaji si kiwango anachotoa wala aina ya utoaji. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kitu kinachoipa thamani na itibari amali ni kufanywa kwake kwa ajili ya Allah; na amali au jambo linalofanywa bila kuwa na msukumo huo huwa haina thamani. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba dunia ni soko ambalo baadhi ya watu wanalifanyia muamala na wanadamu wenzao ili kupata faida na tijara ya dunia, na baadhi ya watu wanafanya muamala na Mwenyezi Mungu ili kupata tijara na malipo ya akhera.

Ifuatayo sasa ni aya ya 40 ambayo inasema:

اللَّهُ الَّذِي خَلَقَكُمْ ثُمَّ رَزَقَكُمْ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يُحْيِيكُمْ هَلْ مِن شُرَكَائِكُم مَّن يَفْعَلُ مِن ذَلِكُم مِّن شَيْءٍ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَى عَمَّا يُشْرِكُونَ

Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni, kisha akakuruzukuni, kisha anakufisheni, na kisha anakufufueni. Je! Yupo yeyote katika hao mnao washirikisha na Mwenyezi Mungu afanyae lolote katika hayo? Yeye ametakasika; na ametukuka na hayo wanayo mshirikisha nayo.

Aya hii inaashiria nafasi isiyo na mfano wala mbadala ya Allah SW katika ulimwengu wa maumbile na kueleza kwamba: Kuumbwa kwenu, riziki zenu katika uhai wenu, kufa kwenu na kufufuliwa kwenu mara ya pili Siku ya Kiyama, yote hayo yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Kwa nini basi mnavidhania na kuviitakidi baadhi ya vitu au watu kuwa washirika wa Mwenyezi Mungu? Je wao wana mchango na nafasi yoyote katika masuala hayo? Kama washirikina wa zama zile na za sasa watalitafakari suali hili, jawabu lao litakuwa ni la. Kwa sababu inawabainikia wazi kwamba vitu hivyo wanavyoviabudu havina nafasi yoyote katika uhai wao, kufa kwao wala riziki yao bali wanaviabudu na kuvitukuza vitu hivyo visivyo na uhai kwa sababu tu ya kuwafuata wazee wao waliowatangulia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba riziki ya wote waliopita, sisi tuliopo na wataokuja baada yetu, iko mikononi mwa Allah ambaye ni Ar-Razzaq. Kwa hivyo tuwe waja wake Yeye tu wala tusikifanye kingine chochote kile kuwa mshirika wake. Aidha aya hizi zinatutaka tujue kwamba sababu, nyenzo na kanuni za maumbile ni vitu vilivyoumbwa na Mwenyezi Mungu na wala haviko mkabala na Yeye. Tuelewe kwamba nguvu zote zisizo za Kiungu hazijitegemei kwa nafsi yake na wala hazina uwezo wa kuumba hata kiumbe kidogo kabisa.

Aya ya 41 na 42 za sura yetu hii ya Ar-Rum ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:

ظَهَرَ الْفَسَادُ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ بِمَا كَسَبَتْ أَيْدِي النَّاسِ لِيُذِيقَهُم بَعْضَ الَّذِي عَمِلُوا لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ

Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa sababu ya iliyo yafanya mikono ya watu, ili Mwenyezi Mungu awaonjeshe baadhi ya waliyo yatenda. Huenda wakarejea kwa kutubu. 

قُلْ سِيرُوا فِي الأَرْضِ فَانظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلُ كَانَ أَكْثَرُهُم مُّشْرِكِينَ

Sema: Safirini katika ardhi muangalie ulikuwaje mwisho wa walio tangulia. Wengi wao walikuwa washirikina. 

Baada ya aya zilizotangulia zilizoelezea itikadi zisizo sahihi za washirikina, aya tulizosoma zinasema: Kuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya imani na mwenendo wa watu na kujitokeza maovu na ufisadi katika jamii yao. Chanzo hasa cha matatizo yote ima ni kumkufuru na kumshirikisha Mwenyezi Mungu au kumsahau Yeye Mola. Mtu ambaye hamfikiri wala hamtangulizi Mwenyezi Mungu katika mambo yake huwa hajali kufanya madhambi na kwa njia hiyo huisababishia masaibu nafsi yake mwenyewe, familia yake na jamii yake nzima kutokana na athari za maovu yake. Athari ambazo sehemu yake moja inadhihirika hapa duniani na katika maisha ya watu, na sehemu nyingine itadhihirika akhera na kuwafanya waovu na wafanya madhambi wafikwe na adhabu ya Moto. Qur'ani tukufu inawausia Waislamu watalii na kusoma historia ya kaumu zilizopita na kujionea maisha ya baadhi ya kaumu za zama hizi ili kubaini taathira mbaya za madhambi na ufisadi katika jamii. Waislamu wanapaswa wajue kwamba Mwenyezi Mungu anawaonjesha watu adhabu ya baadhi ya maovu wanayoyafanya papa hapa duniani ili asaa wazinduke na kuyaacha maovu na madhambi hayo. Leo zinashuhudiwa katika pembe mbalimbali za dunia athari za tamaduni na staarabu kubwa kubwa zilizosalia; staarabu na tamaduni ambazo kuna wakati zilikuwa na umakinifu, nguvu na utajiri mkubwa mno lakini baada ya muda kupita ziliporomoka na kutoweka kutokana na dhulma na uonevu na isirafu na ubadhirifu wa watu wake na leo hii yamebakia magofu tu ya makasri na majengo ya miji yao. Nukta ya kuvutia hapa ni kwamba Qur'ani tukufu inaitaja shirki kuwa ndio chanzo kikuu cha uharibifu na madhambi yote ili kutilia mkazo nukta hii, kwamba shirki ndiyo sababu kuu ya upotokaji na maangamizi; na Tauhidi na kuwa mja halisi wa Mola mmoja tu asiye na mshirika ndio sababu hasa ya mwanadamu kupata saada, sakina na utulivu wa kweli. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba matendo maovu na haribifu ya watu yana taathira kwa mfumo wa maumbile na yanachangia kutokea majanga na maafa ya kusikitisha ya kimaumbile. Kuchafuka na kuharibika mazingira kunatokana na mwenendo haribifu wa watu. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mazingira yaliyotuzunguka, yawe ya ardhi au bahari ni amana tuliyokabidhiwa sisi wanadamu na Allah. Na hakuna shaka, Muumba wa ulimwengu huu hajatupa idhini na mamlaka ya kuitumia amana hiyo vyovyote vile tutakavyo. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Uislamu unawausia watu kusafiri na kutalii endapo utalii huo utafanyika kwa lengo la maana na utawapa funzo, ibra na mazingatio kwa watakayoyaona. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa kama akthari ya wanajamii watakuwa wameghariki kwenye maovu na ufuska jamii hiyo itaghadhibikiwa na kuonjeshwa adhabu na Allah na inapasa mtu aihame jamii kama hiyo. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 725 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa wale ambao wayaonapo maovu katika jamii huyaondoa ima kwa mikono yao, ndimi zao au angalau huchukia nyoyoni mwao. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags