Jan 24, 2017 09:45 UTC

Sura ya Ar-Rum, aya ya 43-46 (Darsa ya 726)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwingine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 726 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 30 ya Ar-Rum. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 43 ambayo inasema:

فَأَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ الْقَيِّمِ مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ يَوْمٌ لّا مَرَدَّ لَهُ مِنَ اللَّهِ يَوْمَئِذٍ يَصَّدَّعُونَ

Basi uelekeze uso wako kwenye Dini Iliyo Nyooka kabla ya kufika Siku hiyo isiyo zuilika, inayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo watu watatengana.

Moja ya sifa maalumu za dini tukufu ya Uislamu ni kuwiyana kwake na akili, fitra na maumbile ya mwanadamu. Kwa hiyo katika aya hii tuliyosoma Uislamu umetajwa kuwa ni dini iliyosimama juu ya misingi imara na madhubuti na pia yenye kuzingatia na kujumuisha ndani yake kila lenye maslahi kwa mtu binafsi na jamii kwa jumla. Tab'an athari na baraka zake zitazinufaisha jamii za Kiislamu ikiwa jamii zenyewe zitashikamana na Uislamu kwa ukamilifu wake na kuufanya kuwa ndio mwongozo wao mkuu wa kimatendo katika masuala yao yote ya maisha; na si kuchagua yale ziyapendayo na kuyaacha yale zisiyopendezwa nayo. Ikiwa mtu atajua kwamba fursa aliyonayo katika maisha ya dunia ni ndogo na muda wa kumalizika kwake ni mfupi kuliko anavyofikiria bila ya shaka atajitahidi kuitumia zaidi fursa hiyo kwa ajili ya huko anakoelekea ili asije akafikwa na majuto.

Moja ya hali maalumu ya Siku ya Kiyama ni kwamba siku hiyo watu watakuwa makundi makundi, huku waumini wakiwa na njia yao; na makafiri na waliofuata upotofu, nao pia wakiwa na njia yao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kufuata dini na kushikamana na mafundisho yake kunatakiwa kufanyike kwa uzito na kwa ukamilifu wake na si kuifanya kitu cha kujazia muda na cha msimu maalumu. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kitu kinachoweza kuiokoa jamii na madhara ya kiakhlaqi na kijamii ni kuwa na mtazamo kamili na wa pande zote wa kushikamana na mafundisho ya dini.

Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 44 na 45 ambazo zinasema:

مَن كَفَرَ فَعَلَيْهِ كُفْرُهُ وَمَنْ عَمِلَ صَالِحًا فَلِأَنفُسِهِمْ يَمْهَدُونَ

Anaye kufuru basi ukafiri wake utakuwa juu yake mwenyewe, na anaye tenda mema, basi wanazitengezea nafsi zao.

لِيَجْزِيَ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ مِن فَضْلِهِ إِنَّهُ لا يُحِبُّ الْكَافِرِينَ

Ili awalipe walio amini na wakatenda mema kutokana na fadhila yake. Hakika Yeye hawapendi makafiri.

Tumeona aya iliyotangulia ikieleza kwamba Siku ya Kiyama watu watatawanyika na kuwa makundi makundi huku safu za waumini zikitenganika na kupambanuka na zile za makafiri. Aya tulizosoma zinasema: Malipo ya thawabu na adhabu watakayolipwa watu yatatokana na amali zao wenyewe walizofanya duniani. Ukafiri utamtia hasarani mtu na kumtumbukiza kwenye moto wa Jahanamu na imani na amali njema zitakuwa sababu ya yeye kupata utulivu na raha ya milele kwenye Pepo ya Allah.

Tab'an kwa upande wa makafiri kila mmoja ataadhibiwa kulingana na ukafiri wake na kiwango cha maovu na maasi aliyofanya, lakini kwa upande wa waumini, wao mbali na kulipwa malipo ya thawabu kwa amali njema walizofanya watapata pia fadhila na rehma maalumu za Allah. Na hicho ndicho kitu ambacho ukafiri utawakosesha wafuasi wake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba uumini na ukafiri wa watu haumnufaishi wala haumsababishii madhara yoyote Allah SW, bali faida ya kuamini na hasara ya kukufuru zinawarudia wanadamu wenyewe. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Mwenyezi Mungu Mtukufu anaamiliana na makafiri kwa msingi wa uadilifu, lakini muamala wake kwa waumini wenye kufanya amali njema unatokona na rehma na fadhila zake Mola.

Tunaihatimisha darsa yetu ya leo kwa aya ya 46 ambayo inasema:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَن يُرْسِلَ الرِّيَاحَ مُبَشِّرَاتٍ وَلِيُذِيقَكُم مِّن رَّحْمَتِهِ وَلِتَجْرِيَ الْفُلْكُ بِأَمْرِهِ وَلِتَبْتَغُوا مِن فَضْلِهِ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

Na katika Ishara zake ni kuzituma pepo ziletazo bishara njema, na ili kukuonjesheni baadhi ya rehema zake, na ili majahazi yende kwa amri yake; na mtafute kutokana na fadhila yake, na ili mumshukuru.

Aya hii inaashiria tena ishara na alama za Tauhidi zilizotajwa katika aya za mwanzoni mwa sura hii na kugusia uwiyano na mlingano wa mfumo wa ulimwengu wa maumbile kwa kueleza kwamba: Kama mtatafakari na kuangalia mbinguni na ardhini na kuvizingatia vitu mbalimbali vya kimaumbile kama upepo na mvua ambazo hunyesha na kumiminika ardhini kila mara, mtaweza kubaini qudra, uwezo na hikma ya Mola pekee wa haki na Muumba wa ulimwengu. Mtaweza kumaizi kwamba kupitia vitu viwili hivyo vya kimaumbile vinavyoonekana kidhahiri kuwa vya kawaida, Allah SW anaviwezesha kuishi viumbe kadhaa vyenye uhai kama mimea, wanyama na watu na kuviwekea kwenye kila pembe ya sayari ya ardhi yale yote vinayoyahitajia. Kilimo na ufugaji ambavyo ni vyanzo viwili muhimu vya chakula cha mwanadamu vinapatikana kwa msaada wa upepo na mvua. Kama ambavyo vyombo bora kabisa vya usafirishaji mazao na bidhaa za viwili hivyo pia, iwe hapo kale au katika zama za sasa ambavyo ni meli vinaweza kuifikia kila pembe na kona ya dunia kupitia njia za baharini.

Lakini kwa masikitiko ni kwamba wanadamu waliowengi hawazingatii na kutafakari juu ya neema hizo kubwa walizojaaliwa na Allah, bali wanazichukulia kuwa vitu vya kimaumbile, kama kwamba vinajitokeza vyenyewe kwa sadfa wala hakuna nguvu yoyote ya juu zaidi yenye nafasi katika kujitokeza na kufanya kazi vitu hivyo.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba upepo ndio unaosukuma mawingu katika anga ya sayari ya dunia kutoka sehemu moja hadi nyingine na kukifanya chanzo hicho kikubwa cha maji kisafirishwe kupitia angani hadi kwenye maeneo makavu na yabisi ya ardhi na kuyalainisha na kuyarutubisha kwa maji ya mvua.

Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kwa hakika harakati na mwendo wa meli na merikebu baharini uko kwenye mamlaka ya Mwenyezi Mungu, si nahodha wa merikebu! Sababu ni kuwa Allah SW ameweka kanuni za maumbile zinazowezesha meli kutembea majini. Kwa mujibu wa kanuni hizo mameli makubwa makubwa yanaweza kuelea majini, yakakata masafa marefu kwa gharama ndogo na kusafirisha shehena chungu nzima za bidhaa na wasafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba kufanya juhudi na bidii za kutafuta chumo la halali ni katika mambo yaliyousiwa na Qur'ani. Tab'an mwanadamu anapaswa kumshukuru Allah kwa kile anachojaaliwa kupata na kujua kwamba kimetokana na Yeye Mola; si elimu, ujuzi na uhodari wake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 726 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwezeshe kuwa washurukivu wa neema zake, kubwa na ndogo, tunazozijua na tusizozijua. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags