Feb 22, 2017 23:34 UTC
  • Alkhamisi, 23 Februari, 2017

leo ni Alkhamisi tarehe 25 Jamadil Awwal 1438 Hijria sawa na Februari 23, 2017.

Katika siku kama ya leo miaka 1374 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Muawiya bin Yazid, Khalifa wa tatu wa ukoo wa Bani Umayyah aliaga dunia katika mazingira ya kutatanisha. Alichukua hatamu za uongozi baada ya kuaga dunia baba yake yaani Yazid bin Muawiya. Hakuwa na hamu ya kuendelea kuongoza kutokana na kuwa alikuwa akitambua kwamba, Ahlul Bayt (a.s) ndio waliostahiki katika hilo. Muawiya bin Yazid anayejulikana kama Muawiya wa Pili alitoa hotuba na kulaani vita vya babu yake yaani Muawiya bin Abi Sufiyan dhidi ya Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) na vita vya baba yake yaani Yazid dhidi ya Imam Hussein (a.s) na kuwasifu Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad (saw).

معاویه بن یزید

Tarehe 5 Esfand hapa nchini Iran inatambuliwa kuwa ni siku ya kumuenzi msomi mkubwa na mashuhuri wa Kiirani Khaja Nasiruddin Tusi. Msomi huyo alizaliwa mwaka 795 Hijria katika mji wa Tus ilioko kaskazini mashariki mwa Iran na kubobea katika elimu za falsafa, hisabati, nujumu na kadhalika. Katika maisha yake aliasisi kituo kikubwa cha kielimu na akademia ya kwanza ya sayansi yaani mahala pa kuangalilia mwenendo wa nyota, mwezi na jua iliyojulikana kwa jina la Maraghe huko kaskazini magharibi mwa Iran. Aalimu huyo aligundua namna mpya za kutumia saa ya jua kwa ajili ya kituo hicho. Kituo hicho kilikuwa na suhula muhimu zaidi ambazo kwa miaka 300 baada ya hapo hazikuweza kushushudiwa katika nchi za Magharibi.

Khaja Nasiruddin Tusi

Siku kama ya leo miaka 218 iliyopita, Napoleon Bonaparte mfalme wa Ufaransa, alianza kuishambulia Sham, ambayo wakati huo ilikuwa ikiundwa na nchi za Syria, Jordan, Lebanon na Palestina. Mashambulio ya Bonaparte dhidi ya Misri yalifanyika kwa lengo la kutoa pigo kwa Uingereza iliyokuwa mkoloni wa Misri. Sababu ya mashambulio ya Napoleon Bonaparte dhidi ya Sham iliyokuwa sehemu ya ardhi ya utawala wa Othmania, ilikuwa ni hatua ya mfalme wa utawala wa Othmania ya kutangaza vita dhidi ya Ufaransa. Katika mashambulio hayo, na licha ya kwamba awali Bonaparte alipata ushindi, lakini baadaye alilazimika kuacha vita na kurejea kwao kutokana na uungaji mkono wa Uingereza na Urusi kwa utawala wa Othmania bila kusahau kuharibika hali ya mambo ndani ya Ufaransa.

Napoleon Bonaparte

Siku kama ya leo miaka 131 iliyopita, Charles Martin Hall, mvumbuzi na mwanakemia wa Marekani alifanikiwa kuvumbua njia mpya ya upatikanaji wa aluminiamu. Aluminiamu ni chuma cheupe na chepesi kinachoweza kukunjwa kwa urahisi. Aluminiamu hiyo ambayo ni nyepesi kuliko chuma, leo hii imekuwa na matumizi mengi katika shughuli za viwanda na kadhalika.

Charles Martin Hall