Feb 23, 2017 23:04 UTC
  • Ijumaa, tarehe 24 Februari, 2017

Leo ni Ijumaa tarehe 26 Jamadil Awwal 1438 Hijria sawa na Februari 24, 2017.

Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita sawa na tarehe 24 Februari 1949 wawakilishi wa Misri na utawala wa Kizayuni wa Israel walisaini mkataba wa kusitisha mapigano kati ya pande mbili hizo huko katika kisiwa cha Rhodes kilichoko katika bahari ya Aegean. Ni vyema kutaja hapa kuwa baada ya kuundwa serikali ya Kizayuni mwaka 1948 huko katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu, Misri ilishirikiana bega kwa bega na baadhi ya nchi za Kiarabu katika kupigana vita dhidi ya utawala wa Kizayuni. Hata hivyo wanajeshi wa utawala huo walifanikiwa kuingia katika ardhi ya Misri na Lebanon baada ya kuishambulia safu ya vikosi vya mapambano vya Waarabu ambavyo vilikuwa na zana chache za kisasa za kivita na hivyo kutoa pigo kwa vikosi vya nchi za Kiarabu.

Miaka 169 iliyopita utawala wa muda au duru ya pili ya mfumo wa jamhuri ulianza huko Ufaransa baada ya wananchi kuendesha mapambano ya ukombozi na kumuondoa madarakani Luis Phillipe Mfalme mbeberu wa nchi hiyo. Utawala wa aina hiyo unajulikana pia katika historia ya Ufaransa kwa jina la "Utawala wa Waandishi wa Habari". Hii ni kwa sababu waandishi habari 11 waliokuwa wakipigania mfumo wa jamhuri chini ya uongozi wa Alphonse de Lamartine malenga na mwandishi wa Kifaransa, ndio waliokuwa wakisimamia utawala huo.

Napoleon

Miaka 492 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Luis Vaz de Camoens, malenga mkubwa wa Kireno na mmoja wa wanafasihi wakubwa wa Ulaya huko Lisbon mji mkuu wa Ureno. Mbali na kuwa mshairi, De Camoens alikuwa mpiganaji jasiri. Moja ya kazi muhimu za utunzi za Luis Vaz de Camoens ni ile aliyoipa jina la" The Lusiads."

Luis Vaz de Camoens

Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Allamah Mirza Muhammad Hussein Naini, marjaa na faqihi mkubwa na mmoja wa wahakiki wa elimu ya usulu fiq’h. Allamah Naini alizaliwa mwaka 1276 Hijiria Qamaria mkoani Nain, ambao ni moja ya mikoa ya katikati mwa Iran katika familia ya kidini. Allamah Naini alisoma na kuhitimu masomo yake ya awali nyumbani kwao na kuendelea na masomo ya juu huko mjini Najaf, Iraq. Akiwa mjini hapo, alipata kusoma kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama vile Allamah Mirza Shirazi na kufikia daraja ya juu ya elimu za hesabu, falsafa ya sayansi, falsafa, irfan na fiq’hi. Miongoni mwa athari za Allamah Naini ni pamoja na vitabu vya “Wasiilatun-Najjat” na “Tanbiihul-Ummah wa Tanziihul-Millah” kitabu ambacho kilitoa mchango mkubwa katika kuathiri mapambano dhidi ya viongozi dhalimu wa zama hizo.

Allamah Mirza Muhammad Hussein Naini