Feb 26, 2017 23:20 UTC
  • Jumatatu 27 Februari, 2017

Leo ni Jumatatu tarehe 29 Jamadil Awwal 1438 Hijria sawa na Februari 27, 2017

Siku kama ya leo miaka 6 iliyopita, alifariki dunia Waziri Mkuu wa zamani wa Uturuki Najmuddin Erbakan akiwa na umri wa miaka 84. Baada ya kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Istanbul, Erbakan alijiunga na Chuo Kikuu cha Aachen nchini Ujerumani ambako alipata shahada ya uzamivu. Mwaka 1969 Najmuddin Erbakan aliingia katika uwanja wa siasa na kuchaguliwa kuwa Mbunge. Mwaka 1987 aliongoza chama chenye mielekeo ya Kiislamu cha Refah ambacho kilipata viti vingi vya bunge na kumteuwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 1996. Tukio hilo liliwakasirisha mno wanasiasa wa kilaiki wa Uturuki, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. Serikali ya Erbakan ilipigwa vita na jeshi la Uturuki na miezi 10 baadaye chama cha Refah kilivunjwa na wanajeshi, na mwanasiasa huyo akapigwa marufuku kujishughulisha na masuala ya kisiasa kwa kipindi cha miaka 5. Profesa Najmuddin Erbakan anatambuliwa kuwa baba wa harakati ya Kiislamu ya Uturuki.

Najmuddin Erbakan

Katika siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, Sayyid Mahdi Hakim aliyekuwa mjumbe muhimu wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq na mwana wa Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim mmoja wa marajii wakubwa wa Kiislamu aliuawa shahidi na makachero wa utawala wa Saddam Hussein dikteta wa zamani wa Iraq, huko Khartoum mji mkuu wa Sudan. Sayyid Mahdi Hakim alikuwa mmoja wa wanafunzi wa shahidi Ayatullah Sadr na mmoja wa wapinzani wakuu wa utawala wa Saddam Hussein.

Ayatullah Sayyid Mahdi Hakim

Miaka 41 iliyopita katika siku kama hii ya leo Jamhuri ya Kiarabu ya Sahara ilijitangazia uhuru. Jamhuri hiyo iko kaskazini magharibi mwa Afrika katika pwani ya Bahari ya Atlantic na ina ukubwa wa kilomita mraba laki mbili na 84 elfu na jamii ya watu karibu laki tatu. Jamii ya Jamhuri ya Kiarabu ya Sahara inaundwa na watu wa kaumu mbalimbali za kiarabu, Barbar, Hassaniya na Tuareg. Mwaka 1975 wakoloni wa kihispania waliikabidhi ardhi ya Sahara kwa Morocco baada ya mapambano ya miaka mingi ya watu wa eneo hilo. Baada ya kuondoka wakoloni wa Kihispania, harakati ya Polisario ilitangaza uhuru wa nchi hiyo kwa kuunda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu na kukataa utawala wa Morocco an Mauritania katika ardhi ya eneo hilo. Mwaka 1979 Mauritania pia ilitupia mbali madai ya kumiliki eneo hilo la Sahara lakini Morocco ingali inadai kuwa ni sehemu ya ardhi yake. Lugha rasmi ya watu wa Sahara ni Kiarabu na Hassaniya na asilimia 99 ya wakazi wake ni Waislamu.  

Bendera ya Jamhuri ya Sahara Magharibi

Na siku kama ya leo miaka 115 iliyopita, alizaliwa John Steinbeck mwandishi wa riwaya wa Kimarekani. Steinbeck alizaliwa mwaka 1902 na katika kipindi cha ujana wake alijishughulisha na kazi mbalimbali kabla ya kuchagua kazi ya uandishi ambako alionesha kipawa kikubwa. Mashaka ya kimaisha yalimtayarishia John Steinbeck mazingira mazuri ya kueleza kwa ufasaha maisha ya watu dhaifu na maskini katika jamii ya Marekani. Alikuwa hodari mno katika kueleza mandhari, matukio na hali mbalimbali. Steinbech ameandika vitabu vingi kama Of Mice and Men, Bombs Away na Cup of Gold.

John Steinbeck