Jumanne, 28 Februari, 2017
Leo ni Jumanne tarehe Mosi Jamadithani 1438 Hijria sawa na 28 Februari, 2017
Tarehe 10 Esfand miaka 38 iliyopita hayati Imam Ruhullah Khomeini kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran aliwasili katika mji wa kidini wa Qum baada ya kuwa uhamishoni kwa kipindi cha miaka 15. Imam alipelekwa uhamishoni na utawala wa Shah hapo mwaka 1343 Hijria Shamsia baada ya matukio ya umwagaji damu ya tarehe 15 Khordad mwaka 1342. Tarehe 12 Bahman mwaka 1357 Imam alirejea nchini akitokea Ufaransa na katika siku kama ya leo baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliwasili katika mji mtakatifu wa Qum na kuishi huko. Miezi kadhaa baadaye Imam Ruhullah Khomeini alihamia Tehran kutokana na udharura wa kuongoza harakati ya Mapinduzi.

Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita inayosadifiana na 28 Februari 1991, George Bush "baba" alitangaza usitishaji vita vya Ghuba ya Uajemi vilivyodumu kwa muda wa siku 40. Mgogoro huo ulianza mwezi Agosti 1990 baada ya majeshi ya Iraq kushambulia ghafla sehemu ya ardhi ya Kuwait na kuikalia kwa mabavu. Ndege za kijeshi za Marekani, Uingereza na Ufaransa zilianza kuyashambulia majeshi ya Iraq baada ya utawala wa Saddam Hussein kukataa amri ya kuyaondoa majeshi yake nchini Kuwait.

Siku kama ya leo miaka 95 iliyopita sawa na tarehe 28 Februari 1922, nchi kongwe ya Misri ilipata uhuru. Misri ilikombolewa na Waislamu miaka 20 baada ya kudhihiri dini tukufu ya Kiislamu. Mwaka 969 nchi hiyo ilidhibitiwa na kutawaliwa na silsila ya wafalme wa Fatimiyya hadi mwaka 1172 ambapo utawala huo ulipinduliwa na Maayyubi. Baada ya hapo Misri ilidhibitiwa na tawala tofauti. Waingereza walianza kuwa na ushawishi huko Misri katika miongo ya mwishoni mwa karne ya 19. Hata hivyo wananchi wa Misri walikabiliana na ukoloni wa Uingereza na mwanzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia hapo mwaka 1914 Uingereza iliitangaza Misri kuwa chini ya himaya yake. Wananchi wa Misri walidumisha mapambano ya uhuru baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na kuilazimisha Uingereza kuutambua rasmi uhuru wa nchi hiyo hapo mwaka 1922.
Siku kama ya leo miaka 484 iliyopita, alizaliwa Michel de Montaigne, mtaalamu wa falsafa wa Ufaransa. Akiwa kijana mwenye umri wa miaka 13 Montaigne alijiunga na chuo kikuu cha Toulouse na kusomea somo la sheria. Baada ya masomo yake alianza kufanya kazi za mahkama huku akifanya utafiti juu ya falsafa. Montaigne ameandika vitabu kadhaa, muhimu zaidi kikiwa ni kitabu cha ‘Makala’ chenye juzuu tatu ambacho kimesheheni masuala tofauti. Aidha msomi huyo wa Ufaransa alikuwa mfuasi wa mrengo wa harakati ya Utu, Akili, Kutafuta amani na Matukufu ya Akhlaqi (tabia njema). Michel de Montaigne alifariki dunia mwaka 1592.
Siku kama ya leo miaka 495 iliyopita, zilianza harakati za mapinduzi ya wananchi wa Sweden dhidi ya utawala na upenyaji wa Christiane wa Pili, mtawala wa Denmark ambaye alizikalia kwa mabavu Sweden na Norway. Kiongozi wa harakati hizo alikuwa Gustav Vasa. Hatimaye kwa msaada wa wakulima, wananchi na wafuasi wa Uprotestanti, Vasa akafanikiwa kuikomboa nchi hiyo kutoka mikononi mwa mtawala Christiane wa Denmark. Baada ya mapinduzi hayo, Gustav Vasa akawa kiongozi wa Sweden. Silsila ya utawala wa Vasa ulioendelea hadi karibu karne tatu, ilipinduliwa madarakani mwaka 1818 na Marshall Baptiste Bernadotte, mmoja wa makamanda wa jeshi la Ufaransa.