Mar 06, 2017 06:04 UTC
  • Jumapili Machi 5, 2017.

Leo ni Jumapili tarehe 6 Jamaduth-Thani mwaka 1438 Hijria, sawa na tarehe 5 Machi 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 505 iliyopita, alizaliwa Gerhard Kremer maarufu kwa jina la Gerardus Mercator, mwanajiografia wa Ubelgiji. Akiwa kijana mdogo alipendelea sana kusoma elimu ya jiografia ambapo katika hilo aliamua kuandaa ramani sahihi kwa ajili ya mabaharia. Ni kwa ajili hiyo ndio maana mwaka 1534 Miladia, akaasisi kituo kikuu cha masuala ya jiografia. Hata hivyo alichukua miaka miaka 34 yaani hadi mwaka 1568 kuweza kuandaa mchoro wa ramani za mzunguko wa dunia kwa namna sahihi. Kitendo hicho kilihesabiwa kuwa mwanzo wa kipindi cha jiografia ya kisasa barani Ulaya na kwa ajili hiyo Gerhard Kremer akaitwa baba wa jiografia.  Mercatoralifariki dunia mwaka 1594 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 190 iliyopita, yaani sawa na tarehe 5 Machi 1827 alifariki dunia Alessandro Volta, mtaalamu wa fizikia wa Italia akiwa na umri wa miaka 83. Sambamba na kufundisha katika chuo kikuu, Volta alikuwa akifanya uhakiki na akafanikiwa kutengeneza chombo cha kupimia kiwango cha umeme Electrometre.

Siku kama ya leo miaka 190 iliyopita, alifariki dunia Pierre Laplace mwanahisabati mashuhuri wa Kifaransa. Alizaliwa mwaka 1749 na baada ya kuhitimu masomo yake alijishughulisha na kufundisha hisabati. Laplace alitumia sehemu kubwa ya umri wake kutwalii na kufanya uhakiki kuhusiana na elimu za nujumu na hisabati.

Siku kama ya leo miaka 122 iliyopita, alifariki dunia Henry Rawlinson, mwanasiasa na mtaalamu wa masuala ya Mashariki wa Uingereza. Rawlinson alizaliwa mwaka 1810 ambapo awali alikuwa akifanya kazi katika shirika la Uingereza nchini India. Taratibu Henry Rawlinson akaanza kuvutiwa na utamaduni wa Iran na hivyo akaamua kujifunza lugha ya Kifarsi huku akisoma historia ya wataalamu wa masuala ya mashariki waliomtangulia. Katika safari yake nchini Iran alitalii athari za kihistoria na kufanikiwa kuandika kitabu kidogo muhimu alichokipa jina la 'Bestun' ambacho alikiandika baada ya kusoma athari za kihistoria za eneo la magharibi mwa Iran zinazorudi nyuma kwa zaidi ya miaka 2500 iliyopita. Athari hizo zilikuwa zimechorwa kwa mfumo wa kuchongwa na mfalme mkuu wa utawala wa Achaemenid na kuzungumzia baadhi ya matukio ya kipindi chake. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Henry Rawlinson akaamini kuwa, Iran ndio nchi pekee yenye uthibitisho wa umiliki. Aidha mtaalamu huyo wa masuala ya mashariki alifanya utafiti kuhusiana na utamaduni wa zamani wa utawala wa Ashur nchini Iraq. Ameandika pia vitabu kadhaa katika uga wa historia ikiwa ni pamoja na kile kinachoitwa 'Safar Naameh Rawlinson,' 'Yodoshti haye Darbaareye Taarikh Qadim Babel' na 'Mukhtasar az Taarikh Ashur.'

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, alifariki dunia Joseph Stalin, kiongozi na dikteta wa Urusi ya zamani. Stalin alizaliwa mwaka 1879 nchini Georgia na alijiunga na mrengo wa kikomunisti baada ya kusoma fikra za mrengo huo. Joseph Stalin alipelekwa uhamishoni huko Siberia mwaka 1913 kutokana na harakati zake za kisiasa dhidi ya serikali ya wakati huo ya Urusi. Alibakia huko hadi baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Urusi mwaka 1917. Alipata vyeo vya ngazi za juu wakati wa uongozi wa Lenin na alishika uongozi wa nchi hiyo akiwa pamoja na wanasiasa wengine mashuhuri baada ya kufariki dunia Lenin. Mwaka 1927 Stalin aliwafutilia mbali wapinzani wake ndani ya chama na kuwa kiongozi asiye na mpinzani katika Chama cha Kikomunisti.

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita alifariki dunia Allamah Dhabihullah Mahallati, faqihi na mtafiti mkubwa wa Kiirani. Ustadh Dhabihullah Mahallati alizaliwa mwaka 1310 Hijiria katika mji wa Mahallat na kuanza kusoma elimu ya msingi katika mji huo. Kisha alielekea mjini Najaf Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo akiwemo Ayatullah Abdul-Hussein Rashti, Sayyid Hassan Swadr, Sayyid Muhammad Firuzabadi, Sheikh Muhmmad Jawad Balaghi, Mirza Naini na Sayyid Abul-Hassan Isfahani. Baada ya miaka 11 ya kuishi mjini Najaf na kufikia daraja ya ijtihadi alielekea mjini Samarra kwa ajili ya kukamilisha masomo yake kwa Allamah Sheikh Agha Bozorg Tehrani. Akiwa mjini hapo alianza kufundisha na kuandika vitabu mbalimbali. Hatimaye Allamah Dhabihullah Mahallati alirejea mjini Tehran baada ya kuishi kipindi cha miaka 25 mjini Samarra huku akiendeleza utafiti na uandishi wa vitabu. Ameandika vitabu vingi katika elimu mbalimbali za Kiislamu.

Na siku kama ya leo miaka 4 iliyopita alifariki dunia Hugo Chávez, rais wa zamani wa Venezuela. Chávez alizaliwa tarehe 28 Julai 1954. Aidha anatambulika kwa kuwa na misimamo ya kupinga ubeberu wa Marekani na kuunga mkono suala zima la Palestina. Hugo Chávez alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 58 kutokana na maradhi ya saratani. Aliingia madarakani mwaka 1998 huku akishinda chaguzi za mwaka 2002 na 2006 kutokana na uungaji mkono mkubwa aliokuwa nao kutoka kwa wananchi. Aidha alishinda uchaguzi wa mwaka 2012 hata hivyo akafariki dunia mapema hapo tarehe 5 Machi mwaka 2013.