Jumanne, tarehe 7 Machi, 2017
Leo ni Jumanne tarehe 8 Jamadithani 1438 Hijria sawa na Machi 7, 2017.
Siku kama ya leo miaka 743 iliyopita, alifariki dunia mwanafalsafa wa Kitaliano, Thomas Aquinas. Alizaliwa mwaka 1225 katika mji wa Napoli na kupata elimu ya dini katika mji huo hadi chuo kikuu. Mwanafikra huyo alibuni falsafa makhususi na kutambua kwamba saada na ufanisi mkubwa zaidi wa mwanadamu ni kupiga hatua za kuelekea kwenye ukamilifu wa kiroho na kwa Mwenyezi Mungu. Aquinas kama alivyokuwa Aristotle, aliamini kuwa ndani ya nafsi ya kila mwanadamu kuna nguvu inayoweza kumfikisha kwenye ukamilifu wa kiroho. Vilevile aliamini kwamba teolojia haipingani na sayansi kwani kila moja kati ya viwili hivyo inataka kujua hakika na kweli. Itikadi za Aquinas na misimamo yake ya kutumia akili na mantiki ambayo ilikuwa ikipingwa vikali na kanisa katika karne za kati, ilisaidia sana kueneza elimu.
Katika siku kama ya leo miaka 252 iliyopita alizaliwa Nicephore Niepce mwanakemia wa Kifaransa na mmoja wa waasisi wa fani ya upigaji picha. Niepce alikuwa mtu wa kwanza aliyefanikiwa kupiga picha ya kwanza duniani. Baada ya hapo, Nicephore alitengeneza kamera ya kupiga picha kwa kushirikiana na marafiki zake. Mwanakemia huyo wa Ufaransa aliaga dunia mwaka 1833.
Siku kama hii ya leo miaka 81 iliyopita vikosi vya jeshi la Ujerumani ya Kinazi vilifanya mashamulizi ya kwanza baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia. Wanajeshi wa Ujerumani walipuuza makubaliano ya Versailles na Locarno kwa amri ya Adolph Hitler na hivyo kuingia eneo la Ranani. Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya Locarno na Warsaw eneo la Rhineland lililokuwa likigombaniwa kati ya Ufaransa na Ujerumani lilitangazwa kuwa eneo lisiloegamea upande wowote. Hata hivyo jeshi la Ujerumani liliamua kuliteka na kulikalia kwa mabavu eneo hilo katika siku kama hii ya leo.
Na siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abdul Hussein Sharafuddin Aamili, alimu na msomi mkubwa wa Kiislamu. Ayatullah Sharafuddin alizaliwa mwaka 1290 Hijria huko Kadhimain moja kati ya miji ya Iraq. Alielekea Jabal Amil nchini Lebanon baada ya kuhitimu masomo yake na kuanza kujishughulisha na harakati za Kiislamu. Msomi huyo mkubwa ametoa huduma za thamani kubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu na daima alikuwa akisisitiza suala la umoja baina ya Waislamu. Ayatullah Sayyid Abdul Hussein Sharafuddin ameandika vitabu na risala nyingi ili kufikiwa lengo hilo.