Mar 09, 2017 01:22 UTC
  • Alkhamisi tarehe 9 Machi, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 10 Jamadithani 1438 Hijria sawa na Machi 9, 2017

Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita Menachem Begin mmoja wa waasisi wa utawala haramu wa Kizayuni na chama cha mrengo wa kulia cha Likud aliangamia. Begin alizaliwa huko Russia mwaka 1913 na baba yake ambaye alikuwa Mzayuni mwenye misimamo mikali alikuwa na taathira na nafasi kubwa katika malezi yake. Akiwa na umri wa miaka 12, Menachem Begin aliasisi kikosi cha vijana wa Kizayuni na miaka miwili baadaye baada ya kuhajiri huko Palestina mwaka 1942 akachaguliwa kuwa kamanda wa Taasisi ya kigaidi yenye misimamo ya kufurutu ada. Taasisi hiyo ilikuwa moja kati ya makundi makuu ya kigaidi na yenye misimamo mikali ya Kizayuni iliyoshiriki kwa kiasi kikubwa katika kuwauwa raia wa Palestina na kuwafukuza katika ardhi zao.

Menachem Begin

Siku kama ya leo miaka 120 iliyopita, Sayyid Jamaluddin Asadabadi mwanazuoni na mmoja wa viongozi wa mapambano dhidi ya ukoloni wa kimaitaifa dhidi ya Waislamu aliuawa. Sayyid Jamaluddin alizaliwa huko Asadabad magharibi mwa Iran na kupata elimu katika taalamu za falsafa, nujumu na historia. Mbali na kufahamu lugha za Kiarabu, Kifarsi na Kituruki, Sayyid Jamaluddin Asadabad alikuwa mtaalamu pia katika lugha za Kiingereza, Kifaransa na Kirusi.

Sayyid Jamaluddin Asadabadi

Miaka 563 iliyopita sawa na tarehe 9 mwezi Machi mwaka 1454 alizaliwa mvumbuzi na baharia wa Kiitalia kwa jina la Americo Vespucci. Vespucci alijishughulisha na kazi za melini kutokana na hamu yake kubwa ya kupenda ubaharia aliyoionyesha tangu akiwa kijana na hivyo kupewa cheo cha unahodha. Baharia Americo Vespucci alisafiri mara nne katika nchi isiyojulikana ambayo hadi wakati huo ilikuwa haina jina na baadaye ikapatiwa jina la mvumbuzi huyo wa Kiitalia yaani Amerika.

Americo Vespucci

Miaka 811 iliyopita katika siku kama hii ya leo ya tarehe 10 Jumadithani kwa mujibu wa nukuu za kuaminika za historia alifariki dunia arif na malenga mashuhuri wa Kiislamu na Kiirani Sheikh Fariduddin Attar Naishaburi. Attar Naishaburi alizaliwa mwaka 513 Hijria na baada ya kufariki dunia baba yake ambaye alikuwa muuza madawa, aliendeleza kazi hiyo ya baba na kupata maarifa mengi kuhusu elimu ya tiba. Katika kipindi hicho alipatwa na mabadiliko makubwa na kuanza safari ya ndani ya nafsi na kutakasa roho. Alifanya safari katika maeneo mengi ya ulimwengu wa Kiislamu ya kupata elimu ya irfani kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo. Baadhi ya nukuu za kihistoria zinasema msomi huyo kubwa wa Kiislamu aliuawa shahidi katika mashambulizi ya Mogul.

Attar Naishaburi ameandika tajiriba na uzoefu wake wa kiirfani katika kalibu ya mashairi na nathari. Miongoni mwa vitabu vya arifu huyo mkubwa Muirani ni "Tadhkiratul Auliyaa" na "Mantwiqut Twair."

Sanamu la Sheikh Fariduddin Attar Naishaburi