Mar 13, 2017 07:07 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Machi 13

Huu ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti ndani ya siku saba zilizopita.......

Iran yaipepeta UAE na kutwaa ubingwa Soka ya Ufuoni Asia

Timu ya taifa ya soka ya ufuoni ya Iran kwa upande wa wanaume imetwaa ubingwa wa Shirikisho la Soka barani Asia AFC mwaka huu 2017, baada ya kuichabanga Umoja wa Falme za Kiarabu katika fainali. Katika mchezo huo wa Jumamosi uliopigwa katika ufuo wa Pantai Batu Buruk, katika mji wa Kuala Terengganu nchini Malaysia, vijana wa Imarati licha ya kuanza mchezo kwa kasi na majaribio ya hapa na pale ya kupata goli bila mafanikio, hatimaye walikubali kuchachawizwa mabao 7-2 na vijana wa Iran. Kiungo Moslem Mesigar ndio aliyeifungulia Iran mvua ya mabao na baada ya hapo, yalimiminika moja baada ya jingine.

Kabla ya ushindi huo mnono wa Iran, Japan iliichananga Lebanon mabao 6-3 katika mchuano wa kutafuta mshindi wa tatu. Mbali na kutwaa Kombe la Mashindano ya Ubingwa wa Soka ya Ufuoni bara Asia AFC mwaka huu 2017, Iran ilitunukiwa mataji matatu zaidi. Mchezaji Mohammadali Mokhtari wa Iran alitawazwa kuwa mchezaji mwenye thamani zaidi katika mashindano hayo sambamba na kutangazwa mwanasoka aliyefunga mabao mengi zaidi katika mashindano hayo. Mokhtari mwenye umri wa miaka 26, alifunga jumla ya mabao 12. Kadhalika timu hiyo ya Iran ilitwaa Taji la Mchezo Mzuri.

Finali AFCON U20; Senegal yadhalilishwa na Zambia

Zambia watwaa ubingwa

Timu ya taifa ya soka ya Zambia ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 20 imeibuka kidedea katika Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka huu baada ya kuikung'uta Senegal mabao 2-0 katika fainali iliyopigwa Jumapili. Katika kipute hicho cha aina yake, kiungo Patson Daka aliipa Chipolopolo bao la kwanza kunako dakika ya 15, huku Edward Chilufya akipiga msumari wa mwisho kwenye jeneza la Senegal kwa bao la pili kunako dakika ya 35.

Kipindi cha pili hakuna timu iliyoliona lango la mwenziwe na hivyo Zambia kutwaa ubingwa wa mashindano hayo ya kibara. Zambia ilifikia hatua ya finali baada ya kupata ushindi hafifu wa bao 1-0 dhidi ya Guinea, katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa mjini Ndola, Zambia. Guinea imeibuka mshindi wa tatu baada ya kuicharaza Afrika Kusini mabao 2-1. Mbali na Zambia na Guinea, Afrika itawakilishwa na Senegal pamoja na Afrika Kusini katika Kombe la Dunia la soka ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 nchini Korea Kusini kuanzia Mei 20 hadi Juni 11, mwaka huu 2017.

Ligi Kuu ya Soka ya wanawake Tanzania

Klabu ya Mlandizi Queens imekuwa ya kwanza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake Tanzania Bara baada ya kuisasambua Panama FC ya Iringa mabao 5-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam. Kwa ushindi huo, malkia hao wamefikisha jumla ya pointi 15, ambazo zimeshindwa kufikiwa na timu zingine tano zilizoshiriki hatua hiyo ya sita bora iliyotoa bingwa. Nyota wa mchezo huo alikuwa mwanadada Mwanahamisi Omary ambaye peke yake alipachika wavuni mabao manne na kufanikiwa kuondoka na mpira baada ya kufunga `hat trick’ pamoja na bao moja zaidi.

Kabla ya hapo, timu ya Marsh Queens iliifunga Fair Play kwa mabao 3-0.

Wanaotajwa kurithi mikoba ya Wenger

Sio siri tena kuwa klabu ya soka ya Uingereza ya Arsenal kwa sasa ipo mbioni kumsaka kocha mpya baada ya tetesi za kutimuliwa mkufunzi wa sasa Arsene Wenger zikipata nguvu. Katika siku za hivi karibuni, mashabiki wa Gunners wameoneka kudhihirisha ghadhabu zao kwa Wenger hususan baada ya klabu hiyo kuondolewa katika michuano ya Ligi Kuu ya Mabingwa almaarufu UEFA Champions League katika hatua ya 16 bora kwa kufungwa jumla ya magoli 10-2. Kichapo hicho kimetonesha kidonda cha mashabiki wa Wabeba Bunduki, haswa kwa kutilia maanani kuwa, Arsenal mara ya mwisho kuchukua taji la EPL ilikuwa ni mwaka 2004. Mashabiki wa klabu hiyo waliandaana hivi karibuni wakimtaka Wenger aondoke, chini ya kaulimbiu Wengxit (Wenger Exit) kama iliyotumiwa wakati Uingereza ilipotaka kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya (Brexit).

Wenger kikaangoni

Kwa sasa kocha wa Juventus Massimilaiano Allegri amethibitisha mbele ya vyombo vya habari kuwa amefanya mazungumzo na Arsenal kuhusu kuchukua nafasi ya Wenger. Wengine wanaokisiwa huenda watarithi mikoba ya Wenger ni Thomas Tuchel (Borussia Dortmund); Diego Simione (Atletico Madrid); Eddie Howe (Bournemouth); Luis Enrique (Barcelona); Manuel Pelligrini (Hebei Fortune China); Rafael Benitez  (Newcastle); Patrick Vieira (New York City); Joachim Low (Ujerumani); Dragan Stojkovic (Guangzhou R&F F.C); Na Leonardo Jardim (AS Monaco). Binafsi unadhani nani anafaa kurithi mikoba ya Wenger?

…………………………….TAMATI………………………