Mar 23, 2017 02:26 UTC
  • Alkhamisi 23 Machi, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 24 Jamadithani 1438 Hijria sawa na Machi 23, 2017.

Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita, sawa na tarehe 3 Farvardin 1384 Hijria Shamsia, alifariki dunia Allamah Sayyid Jalaluddin Ashtiyani, mwanafalsafa na mwanafikra wa Kiislamu baada ya kuugua kwa muda mrefu. Allamah Ashtiyani alizaliwa mjini Ashtiyan katikati mwa Iran na kusoma masomo ya awali mjini hapo, ambapo baadaye alielekea mjini Qum na kupata elimu kutoka kwa wanachuoni wakubwa kama vile Imam Khomeini, Ayatullahil Udhma Burujerdi na Allamah Tabatabai. Kisha alielekea mjini Mash'had na kujishughulisha na uleaji wanafunzi hadi mwisho wa uhai wake.

Allamah Sayyid Jalaluddin Ashtiyani

Siku kama ya leo miaka 365 iliyopita, yaani sawa na tarehe 23 Machi mwaka 1652, kulianzishwa shambulizi la manowari za kijeshi za Uingereza dhidi ya majeshi ya Uholanzi. Amri ya shambulizi hilo ilitolewa na Oliver Cromwell aliyekuwa dikteta wa wakati huo wa Uingereza. Akipata uungaji mkono wa Bunge la Uingereza, Cromwell alimpindua mfalme wa Uingereza na kisha kulivunja bunge la nchi hiyo. Inasemekana kuwa, lengo la kutekeleza shambulio hilo lilikuwa ni kulimaliza nguvu jeshi la Uholanzi ambalo lilikuwa na nguvu kubwa ya majini.

Oliver Cromwell

Miaka 268 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Pierre-Simon Laplace mwanahisabati mashuhuri wa kifaransa. Alizaliwa mwaka 1749 na baada ya kuhitimu masomo alijishughulisha na kufundisha  hisabati. Laplace alitumia sehemu kubwa ya umri wake kutwalii na kufanya uhakiki kuhusiana na elimu za nujumu na hisabati.

Pierre-Simon Laplace

Miaka 61 iliyopita katika siku kama hii ya leo katiba mpya ya Pakistan ilibuniwa na kwa mujibu wake utawala wa nchi hiyo ulibadlishwa kutoka utawala wa gavana mkuu na kuwa na mfumo wa Jamhuri. Nawabzada Liaquat Ali Khan Waziri Mkuu wa wakati huo wa pakistan alichukua madaraka ya kuiongoza nchi hiyo mwaka 1948 kufuatia kifo cha Muhammad Ali Jinnah aliyekuwa mwasisi na gavana mkuu wa nchi hiyo. Liaquat Ali Khan naye pia aliuawa na raia mmoja wa Afghanistan mwaka 1951.

Bendera ya Pakistan

Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, liliasisiwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (W.M.O). Shirika hilo linafungamana na Umoja wa Mataifa na taasisi zote za hali ya hewa ulimwenguni hushirikiana nalo. Miongoni mwa malengo ya kuanzishwa shirika hilo ni kutoa msaada wa elimu ya hali ya hewa kwa wataalamu wa anga, mabaharia, wakulima na shughuli nyingine za kibinadamu. Ni kwa ajili hiyo ndio maana siku ya leo yaani tarehe 23 Machi ikajulikana kuwa Siku ya Hali ya Hewa Duniani.

Shirika la Hali ya hewa Duniani

Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, Ayatullahil Udhma Sayyid Muhammad Ridha Golpayegani, alimu, fakihi mkubwa na mmoja wa marajii wakubwa wa Kiislamu ulimwenguni alifariki dunia. Alizaliwa mjini Golpayegan moja ya miji ya Iran na kusoma masomo ya dini kwa maustadhi stadi na waliokuwa wametabahari kielimu katika zama hizo akiwemo Ayatullah Hairi. Ayatullah Golpayegani alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha mjini Qum-Iran baada ya kuasisiwa kwake. Mwanazuoni huyo mkubwa ameandika vitabu vingi katika nyuga mbalimbali.

Ayatullahil Udhma Sayyid Muhammad Ridha Golpayegani