Spoti Wiki Hii, Apr 3
Huu ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya spoti kitaifa na kimataifa ndani ya siku saba zilizopita.......
Iran yaipara China, yajiweka pazuri
Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezidi kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu Kombe la Dunia mwaka ujao 2018, baada ya kuitandika China bao moja la uchungu katika mchuano wa kutafuta tiketi ya kushiriki fainali hizo za dunia. Katika mchuano huo wa Kundi A uliopigwa Machi 28 katika uwanja wa taifa wa Azadi hapa jijini Tehran, vijana wa Iran walianza mchezo kwa kasi nzuri na kupoteza nafasi nyingi za wazi za kucheka na nyavu za China katika kipindi cha kwanza, labda kutokana na Dragon kuwa na kipa mahiri. Hata hivyo baada ya panga pangua, gusa gusa na pasi za hapa na pale, hatimaye vijana wa Team Melli kama wanavyjulikana hapa nchini, walifanikiwa kupata goli la pekee na la ushindi kupitia mshambuliaji Mehdi Taremi, sekunde chache baada ya kuanza kipindi cha pili. Huu unakua ni ushindi wa tano wa vijana wa Iran katika michuano saba waliyocheza hadi sasa. Wiki iliyopita, Qatar licha ya kuchezea nyumbani uwanja wa Jassim Bin Hamad mjini Doha, ilishindwa kufurukuta mbele ya vijana wa Iran na kukubali kichapo cha bao 1-0. Bao la Iran lilipachikwa kimyani na Mehdi Taremi kunako dakika ya 52. Timu ya Soka ya Iran inatazamiwa kuvaana na Uzbekistan hapa Tehran Juni 12 katika mchuano mwingine wa Kundi A. Timu nyingine ambazo ziko katika Kundi A ni Korea Kusini na Syria.
Madagascar yatinga hatua ya makundi AFCON 2019
Timu ya taifa ya soka ya Madagascar maarufu kama Barea, kwa mara nyingine imepata nafasi ya kufuzu kucheza mechi za kuelekea katika fainali ya Mataifa Bingwa barani Afrika mwaka 2019 nchini Cameroon. Madagascar imefuzu kucheza katika hatua ya makundi baada kuishinda Sao- Tome kwa jumla ya mabao 4-2 katika mchuano wa nyumbani na ugenini katika hatua ya awali. Madagascar sasa itakuwa mbioni kutafuta kushinda kundi hilo dhidi ya Senegal, Equitorial Guinea na Sudan. Madagascar haijawahi kufuzu katika michuano ya fainali ya bara Afrika katika historia ya mchezo wa soka. Mwaka 2016, Madagascar ilishindwa kufuzu kwenda nchini Gabon baada ya kufungwa mechi zake zote za kufuzu dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na Kongo DR.

Kwengineko, timu ya taifa ya soka ya Tanzania almaarufu Taifa Stars imeikung'uta Burundi mabao 2-1 katika mchuano wa kimataifa wa kirafiki uliopigwa uwanja wa taifa wa Dar es Salaam Machi 28. Taifa walipata ushinda huo licha ya kukosa ustadi wa nahodha wake Mbwana Samatta ambaye anaichezea KRC Grenk ya Ubelgiji. Taifa Stars ambayo ipo katika nafasi ya 157 katika viwango vya Shirikisho la Soka Duniani FIFA ukilinganisha na Burundi waliyo nafasi ya 139, wamefanikiwa kupata ushindi huu kupitia magoli ya Simon Msuva na Mbaraka Yusuf Abeid. Msuva alicheka na nyavu kunako dakika ya 22 na kuwafanya wenyeji wawe kifua mbele. Hakuna aliyefanikiwa kuona lango la mwenzake tena katika kipindi cha kwanza baada ya goli la Msuva. Hata hivyo baada ya mapumziko, Burundi walijipapatua na kusawazisha mambo kupitia goli la pekee la kufutia machozi lililofungwa na Laudit Mavugo katika dakika ya 54. Vijana wa taifa walipandisha mori tena na kuanza mpira wa kasi. Kiungo Mbaraka Abeid ambaye ndo kwanza nyota yake inaanza kung'aa katika ulimwengu wa soka alifanikiwa kuipa Taifa Stars goli la ushindi licha ya kuonekana limbukeni kunako dakika ya 78. Taifa Stars sasa inakuwa imepata ushindi wa pili ndani ya saa 72, kwa kutilia maanani kuwa walipata ushindi wa kwanza Jumamosi ya March 25, kwa kuibamiza Botswana mabao 2-0.
Riadha: Kenya yazidi kuonyesha ubabe
Kwa mwaka wa pili mfululizo Kenya imenyakua mataji ya Daegu Marathon nchini Korea Kusini baada ya Mathew Kisorio na Pamela Jepkosgei kuibuka kidedea Jumapili. Kulingana na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF), Kisorio alikimbia kilomita tano za mwisho peke yake na kukamilisha umbali huo wa kilomita 42 kwa saa 2:07:32. Mkenya Peter Some (2:09:22) na Mohamed Reda wa Morocco (2:09:50) walikamilisha kitengo cha wanaume katika nafasi za pili na tatu mtawalia. Vincent Kipsang’ pia kutoka Kenya aliridhika katika nafasi ya nne kwa saa 2:10:23. Bingwa wa mwaka 2016, James Kwambai alisalimu amri baada tu ya kilomita 21 za kwanza. Jepkosgei alifuata nyayo za mshindi wa mwaka 2016 Caroline Kilel kwa kunyakua taji la kinadada kwa saa 2:27:48.
Alifuatwa unyounyo na Wakenya wenzake Winnie Jepkorir (2:27:52), Loice Kiptoo (2:28:39) na Nancy Koech (2:29:30) katika nafasi nne za kwanza, mtawalia.
Dondoo: Rooney ataka kuwa mwanamieleka eti
Nahodha wa klabu ya Manchester United, Wayne Rooney, ameweka wazi kuwa mara baada ya kumalizika kwa msimu huu ataondoka ndani ya kikosi hicho na kujiunga na mchezo wa mieleka wa WWE. Mchezaji huyo amedai kuwa mchezo wa mieleka ni miongoni mwa vitu ambavyo vilikuwa kwenye ndoto zake kwa kipindi kirefu, hivyo huu ni wakati wake sahihi wa kufanya maamuzi hayo.

Rooney amekuwa akionekana katika mashindano mbalimbali ya mieleka ya WWE. Mchezaji huyo msimu huu amekuwa akikosa namba mara kwa mara ndani ya kikosi cha Man U chini ya mkufunzi Jose Mourinho na alihusishwa kutaka kukimbilia katika ligi ya nchini China na Marekani. Klabu mbalimbali za nchini China zilikuwa tayari kuweka mezani kitita cha pauni milioni 52, lakini hadi usajili wa Januari mwaka huu unakamilika mwanakandanda huyo stadi hakuweza kuondoka Man United, lakini kwa sasa anasema yupo tayari kuondoka na kujiunga na mchezo huo wa mieleka. Utakumbuka kuwa Rooney mwaka huu ametajwa kuwa mfungaji bora wa kipindi chote ndani ya kikosi cha Mashetani Wekundu, mbali ya kuwa kiungo mwenye mchango mkubwa ndani ya kikosi cha timu ya Taifa ya Uingreza kwa muda mrefu. Anachosema Rooney ni kweli, mzaha, kauli za Siku ya Wapumbavu Aprili Mosi au ni ndoto za Alinacha? Jibu tulisake pamoja kila kona mpenzi msikilizaji. Sina la ziada, jina langu HH, kwaheri.
…………………………………TAMATI….………………..