Apr 04, 2017 08:12 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (156)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka hapa mjini Tehran. Hii ni sehemu ya 156 katika mfululizo wa vipindi hivi vya Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambavyo ni vipindi vinavyojadili masuala mbalimbali ya itikadi ya Kiislamu.

Katika kipindi cha juma hili tutaendelea kuzungumzia suala linalohusiana na itikadi ya Uimamu ambapo tutajibu swali lililoulizwa na mmoja wa wasikilizaji wetu Bwana Abu Muhammad ambaye hakutaja anakotoka. Swali lenyewe linasema hivi, je, Maimamu wanafahamu kila jambo kama anavyofahamu Mwenyezi Mungu ila kwamba elimu ya Mwenyezi Mungu ni ya dhati hali ya kuwa ya watukufu hao (as) inatokana na ya Muumba wao? Hii ni sehemu ya kwanza ya swali la Abu Muhammad, ama sehemu ya pili ya swali hilo inasema, je, elimu yao hiyo ni ya papo kwa hapo kwa maana kuwa daima huwa wana elimu ya kila jambo wakati wowote  wa maisha yao au la?

Tunarejea sote katika Vizito Viwili ili tupate kujua jibu la swali hili muhimu la Bwana Abu Muhammad, karibuni.

 

Ndugu wasikilizaji, tunatangulia kujibu swali hili kwa kukumbusha kwamba lengo kuu na muhimu la Maimamu katika kila zama ni kuwaongoza waja kuelekea Muumba wao ambaye ni Mwenyezi Mungu na kwa amri yake Yeye na kuwapangia mambo yao kwa mujibu wa muongozo wake. Hii ndio maana ya Imamu kuwa khalifa wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwenye ardhi yake. Huu ndio ukweli wa Quráni Tukufu ambao tulipata kuujua kutokana na aya nyingi za kitabu hicho kitakatifu pamoja na hadithi za viongozi wema wa Kiislamu, jambo ambalo tulilizungumzia kwa urefu katika vipindi vilivyopita. Kutokana na ukweli huo wa Quráni, tunafahamu kwamba ni katika hekima ya Mwenyezi Mungu kuwaandalia makhalifa wake kila suhula wanazohitajia kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao ya ukhalifa wa Mwenyezi Mungu kwenye ardhi yake, majukumu ambayo si mengine bali ni ya kuwaongoza waja wake kwenye njia nyoofu na ya saada ya humu duniani na huko Akhera. Muhimu zaidi katika suhula na mahitaji hayo ya kutekelezea majukumu yao ni kuwa na elimu ya kutosha kuhusiana na kile wanachowaita watu kukifuata. Hili ni jambo lililo wazi kabisa la sivyo, hautakuwa ni uadilifu kumtaka mtu atekeleze jukumu ambalo hajaandaliwa suhula za kulitekelezea. Na Mwenyezi Mungu ni muadilifu na mwenye hekima zaidi, jambo linalomfanya asiweze kumkalifisha Imam Maasumu kutekeleza majukumu ya ukhalifa na uongozi wa waja wake kumuelekea Yeye bila kumpa imam huyo suhula na mambo anayoyahitajia katika utekelezaji wa majukumu hayo. Na muhimu zaidi kati ya mambo hayo yote kama tulivyosema, ni elimu ambayo anapasa kuitumia katika kuwaongoza waja hao kwenye njia nyoofu inayoelekea Kwake Subhanahu wa Taala. Kwa msingi huo tunamwambia msikilizaji Abu Muhammad kwamba jambo lisilo na shaka ni hili kwamba Mwenyezi Mungu humjalia na kumpa walii na khalifa wake elimu yote anayoihitajia katika utekelezaji wa jukumu lake muhimu la ukhalifa, na maandiko mengi matakatifu yameashiria wazi suala hili ambapo tutaashiria baadhi ya maandiko hayo hivi punde, hivyo endeleeni kuwa pamoja nasi.

 

Wapenzi wasikilizaji kati ya hadithi muhimu na kamilifu zaidi katika kujibu swali tunalolijadili hapa, ni hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Imam ar-Ridha (as) katika kubainisha sifa za Imam Maasumu aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwaongoza waja wake. Hadithi hii inatolewa hoja za Kiqur’ani ambapo imepokelewa na kunukuliwa katika vitabu muhimu vinavyotegemewa na madhehebu ya Ahlul Beit vikiwemo viwili hivi vya Uyun al-Akhbar na Aamali vya as-Sheikh as-Swaduq ambapo Imam Ridha (as) ananukuliwa akisema hivi kuhusiana na elimu ya Imam: “Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu huwapa taufiki Manabii na Maimamu na kuwapa kutoka kwenye hazina ya elimu na upole wake kile ambacho hawapi watu wengine. Hivyo elimu yao huwa juu ya elimu ya watu wengine wote katika zama zao (kama) ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 أَفَمَن يَهْدِي إِلَى الْحَقِّ أَحَقُّ أَن يُتَّبَعَ أَمَّن لاَّ يَهِدِّيَ إِلاَّ أَن يُهْدَى فَمَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ

“Sema: Mwenyezi Mungu anaongoa kwendea Haki. Basi, je, anayestahiki kufuatwa ni yule Mwenye kuongoa kwendea Haki au asiyeongoa ila aongozwe yeye? Basi nyinyi mna nini? Mnahukumu namna gani?”

Ni wazi kutokana na dalili ya Imam Ridha (as) kwa kutegemea aya aliyoisoma kwamba elimu ya Maimamu (as) ni kipawa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambacho huwawezesha kutekeleza vyema majukumu yao ya kuwaongoza wanadamu kuelekea haki kwa njia iliyo bora zaidi na kwamba katika zama za Imam yoyote yule hakuna mtu anayeweza kuwa na elimu ya juu kumliko yeye, na hili ndilo jambo linalowahusu Maimamu wote wotoharifu wa nyumba ya Mtume Muhammad (as). Imam Ridha (as) anasema katika sehemu nyingine ya hadithi hii muhimu na timilifu kuhusiana na kauli ya Mwenyezi Mungu kumuhusu Talut inayosema:

إِنَّ اللَّهَ اصْطَفَاهُ عَلَيْكُمْ وَزَادَهُ بَسْطَةً فِي الْعِلْمِ وَالْجِسْمِ وَاللَّهُ يُؤْتِي مُلْكَهُ مَن يَشَاء وَاللَّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ

‘’Hakika Mwenyezi Mungu amemteua yeye juu yenu na amemzidishia ukunjufu wa ilimu na kiwiliwili. Na Mwenyezi Mungu humpa ufalme Wake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mjuzi.”

Na Mwenyezi Mungu alimwambia Mtume wake (saw): ‘’Na fadhila za Mwenyezi Mungu zilizo juu yako ni kubwa. Kisha (as) akasema kuhusiana na Maimamu wotaharifu kurithi elimu ya Manabii (as): ‘’Na Mwenyezi Mungu akasema kuhusiana na Maimamu wa Nyumba ya Mtume na kizazi chake (as): ‘’Au wanawahusudu watu kwa yale aliyowapa Mwenyezi Mungu kwa fadhila yake? Basi tuliwapa ukoo wa Ibrahim Kitabu na hekima na tukawapa utawala mkubwa.’’

 

Kisha Imam Ridha (as) alifupisha natija ya aya hizo tukufu kuhusiana na elimu ya Imam kwa kusema: ‘’Mwenyezi Mungu Mtukufu anapomteua mja wake kusimamia mambo ya waja wake hukunjua kifua chake kwa ajili ya hilo na kuweka humo chemchemi ya hekima na kumpa elimu kwa njia ya ilhamu. Hivyo huwa hachoki kujibu maswali wala kukosea katika kuyajibu naye ni maasumu na mwenye kupata msaada na mwongozo……..Mwenyezi Mungu alimpa uwezo huo ili awe hoja yake kwa waja wake na msimamizi wake kwa viumbe wake, na hiyo ni fadhila ya Mwenyezi Mungu anayompa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa.’’

Kwenye maelezo hayo pia tunapata jibu la sehemu ya pili ya swali la msikilizaji wetu Bwana Abu Muhammad ambalo liliuliza kwamba je, elimu ya Maimamu ni ya papo kwa hapo kwa maana kuwa huwa wana elimu ya kila jambo wanaloulizwa au huwabidi kusubiri na kuchunguza kabla ya kupata jibu?

Kwa maelezo tuliyotangulia kuyapitia tunafahamu vyema kwamba Mwenyezi Mungu huwapa uwezo wa kufahamu kila jambo linalohitajika na waja wake na kwa hivyo huwa hawashindwi kupata jibu la kila swali wanaloulizwa na watu wakati wowote ule.

********

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain kwa juma hili, kipindi ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana nanyi tena juma lijalo panapo majaliwa yake Mola, tunakuageni kwa kusema, kwaerini.