Apr 09, 2017 02:37 UTC
  • Jumapili, Aprili 9, 2017

Leo ni Jumapili tarehe 11 Rajab 1438 Hijria sawa na tarehe 9 Aprili 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1167 iliyopita, alizaliwa mjini Baghdad, Iraq Abubakar Muhammad, maarufu kwa jina la Ibn Anbari, mtaalamu wa fasihi, lugha na mfasiri wa Qur'ani Tukufu. Baada ya kusoma elimu ya lugha na elimu ya Qur'ani Ibn Anbari alianza kusomea elimu ya hadithi. Alikuwa na kipawa cha hali ya juu katika kuhifadhi hadithi huku akifundisha pia wanafunzi wengi taaluma hiyo. Ameandika vitabu vingi katika elimu tofauti ambavyo mojawapo ni 'Adabul-Kaatib' na 'Dhamaairul-Qur'an.' Abubakar Muhammad alifariki dunia siku ya Idul-Udh'ha mwaka 328 Hijiria akiwa na umri wa miaka 57.

Siku kama ya leo miaka 865 iliyopita, alifariki dunia Ibn Asakir Dimashqi, mwanahistoria mkubwa na mtaalamu wa hadithi. Abul-Qasim Ali Bin Hassan Dimashqi, maarufu kwa jina la Ibn Asakir alisoma kwa mapenzi makubwa elimu za Qur'ani, hadithi, fiq'hi na usulu fiq'hi kwa wasomi wakubwa wa mjini Damascus, Syria. Baada ya hapo Ibn Asakir alianza safari ndefu yenye lengo la kukamilisha masomo yake na kupata kusoma katika vituo vya kielimu vya mijini Baghdad, Kufa, Musil, Nishabur, Marv, Isfahan na Hamadan. Msomi huyo ameandika vitabu 134 ambapo miongoni mwavyo ni kile cha "Tarikh Dimeshqi."

Ibn Asakir Dimashqi

Siku kama ya leo miaka 391 iliyopita, alifariki dunia Francis Bacon, mwanafalsafa maarufu wa Uingereza akiwa na umri wa miaka 65. Bacon alizaliwa mjini London tarehe 22 Januari mwaka 1561 Miladia na akaanza kusoma elimu ya msingi akiwa kijana mdogo. Baba yake Francis Bacon alikuwa miongoni mwa watu wa karibu sana na mfalme wa wakati huo wa Uingereza. Ni kwa ajili hiyo ndio maana msomi huyo naye akafanya juhudi kubwa za kujikurubisha kwa mfalme ambapo hatimaye alifanikiwa kuchaguliwa kuwa mjumbe wa baraza la kitaifa sambamba na kusimamia vyombo vya mahakama vya nchi hiyo. Hata hivyo haukupita muda ambapo bunge la Uingereza lilimtuhumu kufanya ubadhirifu mkubwa serikalini na hivyo kumnyang'anya mali zake zote. Aidha Bacon alihukumiwa kifungo cha maisha jela. Hata hivyo mfalme wa Uingereza alimsamehe huku akimalizia maisha yake yoye nje ya jiji la London. Ameandika vitabu vingi katika uga wa falsafa na mashairi.

Francis Bacon,

Siku kama ya leo miaka 152 iliyopita, vilimalizika vita vya ndani nchini Marekani maarufu kwa jina la 'Vita vya Kujitenga.' Vita hivyo vilianza tarehe 12 Aprili mwaka 1861 Miladia, baada ya kuingia madarakani Abraham Lincoln vikizihusisha pande mbili za majimbo ya kusini (ambayo yalikuwa ya mrengo wa kulia) na yale ya kaskazini (ambayo yalikuwa ya upinzani.) Vita hivyo vilivyodumu kwa miaka minne vilifikia tamati kwa ushindi wa upande wa kaskazini hapo tarehe tisa Aprili mwaka 1865, huku vikisababisha mauaji ya zaidi ya watu laki tano. Ni kwa kufikiwa ushindi huo, ndipo kukatangazwa rasmi marufuku ya utumwa nchini humo. Hata hivyo na licha ya kupita karne moja na nusu tangu kumalizika kwa wimbi hilo la utumwa, lakini bado kunaendelea kushuhudiwa ubaguzi wa rangi mkubwa hususan dhidi ya jamii ya Wamarekani wenye asili ya Kiafrika.

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, utawala ghasibu wa Israel ulifanya mauaji ya kinyama katika kijiji cha Deir Yassin huko magharibi mwa Baitul Muqaddas. Mauaji hayo yalifanyika wakati wa vita vya kwanza vya Waarabu na Israel na yalitekelezwa na Wazayuni wa kundi la Irgun lililokuwa likiongozwa na waziri mkuu wa zamani wa Israel Menachem Begin. Eneo la Dier Yassi lilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Wazayuni kutokana na kuwa katika njia ya Baitul Muqaddas na karibu na pwani. Baada ya kukivamia kijiji cha Deir Yassin, Wazayuni hao waliwaua kinyama wakazi 270 wa kijiji hicho ambao hawakuwa na hatia yoyote. Mauaji hayo yaliwalazimisha Wapalestina wengi wa eneo hilo kukimbia makazi yao kwa kuhofia kukaririwa mauaji kama hayo ya kinyama.

Mauaji ya kinyama katika kijiji cha Deir Yassin

Na siku kama ya leo miaka 10 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 20 Farvardin 1385 Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilifanikiwa kupata teknolojia ya kurutubisha madini ya urani kwa ajili ya matumizi ya kiraia. Wasomi na wataalamu wa Iran walifanikiwa kukamilisha mfumo wa kuzalisha nishati ya nyuklia licha ya mbinyo na vikwazo vya nchi za kibeberu. Kwa utaratibu huo Iran iliingia katika kundi la nchi zenye teknolojia ya nyuklia duniani. Mwaka mmoja baadaye Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza kuzalisha nishati hiyo viwandani. Mafanikio hayo makubwa ya Iran yalipatikana chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Hata hivyo baadhi ya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zinapinga vikali miradi ya nishati ya nyuklia ya Iran kutokana na sera zao za kindumakuwili na za kibaguzi.

 

 

 

 

 

Tags