Apr 10, 2017 08:05 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Apr 10

Ufuatao ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti ndani ya siku saba zilizopita, kiaifa na kimataifa......

Mbio za kimataifa za marathon zafanyika Tehran, Wairani wapeta

Mohammad Jafar Moradi, mwanariadha wa mbio za masafa marefu wa Iran ameibuka kidedea katika mashindo ya kimataifa ya mbio za marathon yaliyofanyika hapa Tehran Ijumaa. Moradi mwenye umri wa miaka 26 alishinda mbio za marathon kitengo cha kilomita 42 na kuzawadiwa dola laki 3 za Marekani. Moradhi alifuatwa unyounyo na Mohammad Faraji, aliyeibuka wa pili na kutia kibindoni dola elfu 2 na 500. Ehsan Zainivand, Muirani mwingine alifunga orodha ya tatu bora na kuondoka na dola elfu 2. Katika kitengo cha nusu marathon, Ali Akbar Barzi aliibuka wa kwanza na kuzoa dola 1,500. Hassan Kayani aling'ara katika kitengo cha mbio za kilomita 10 upande wa wanaume na kutwaa dola elfu 1. Kwa upande wa wanawake katika safu hii ya mbio za kilomita 10, Parisa Arab aliibuka kidedea na kutia mfukoni dola elfu 1. Mashindano hayo yamewaleta pamoja maelfu ya wanariadha wa ndani na nje ya nchi. Mohammad Reza Tabesh, Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Bunge la Iran amesema hatua ya maelfu ya wanariadha kushiriki mashindano hayo kutoka nchi mbalimbali duniani ikiwemo Saudi Arabia, ni ithibati kuwa njama za utawala wa Aal-Saud kueneza chuki na woga dhidi ya Iran zimefeli. Duru  ya kwanza ya mashindano hayo yanayojuliakana kwa Kimombo kama Tehran International “Persian Run” 2017 ilifanyika kwa mara ya kwanza hapa Tehran, kuanzia uwanja wa taifa wa Azadi, magharibi mwa Tehran, na kupitia kaika barabara maalumu ya Karaj, kuzunguka medani za Azadi na Enqelab na kisha kutamatishia tena ugani Azadi.

Wanataekwondo wa kike wa Iran wazoa medali Afrika

Wanataekwondo wa kike wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamezoa medali kochokocho katika mashindano ya dunia ya mchezo huo yaliyofanyika nchini Morocco. Ijumaa, siku ya kwanza ya mashindano hayo yanayofahamika kama Kombe la Rais G2 yaliyofadhiliwa na Shirikisho la Taekwondo Duniani, wanataekwondo hao wa Iran walizoa medali mbili za dhahabu, moja ya fedha na moja ya shaba katika michezo iliyochezwa katika mji wa Agadir.

Wanataekwondo wa Iran wang'ara Morocco

Kikosi hicho cha Iran ambacho kiko chini ya mkufunzi Mahrou Kamrani kimeng'ara katika safu za wanataekwondo wa kilo -46, -53, -62 na +73.  Wanataekwondo 239 kutoka nchi mbalimbali duniani wameshiriki mashindano hayo yaliyoanza Aprili 7 na kufunga pazia lake Aprili 9.

CAF: Yanga yaipepeta MC Alger

Klabu ya Yanga ya Tanzania imefanikiwa kuitandika klabu ya MC Alger ya Algeria bao 1-0 katika mchuano wa kufatuta tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho la Soka Afika CAF. Katika kipute hicho kilichopigwa Jumamosi ya April 8 katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam, timu hiyo ya Dar ya Young Africans almaarufu Yanga ilikuwa inacheza mchezo wake kwanza wa duru ya pili hatua ya mtoano kuingia makundi ya Kombe la CAF. Yanga walikuwa wanacheza na timu ambayo imewahi kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika mwaka 1976 na imewahi kutwaa Kombe la Ligi Kuu Algeria mara 7. Hata hivyo pamoja na historia na mafanikio ya MC Alger katika soka la Afrika,  haikuweza kunusurika na kipigo kutoka Yanga. MC Alger ambao walionekana kucheza soka la taratibu na kujiami walijikuta wakifungwa goli 1-0 baada ya wachezaji wa Yanga kupiga pasi nyingi kabla ya Obrey Chirwa kutoa pasi ya mwisho ya goli dakika ya 61 na Thabani Kamusoko akapachika goli hilo la kipekee na la ushindi kwa Yanga. Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alikuwa na haya ya kusema baada ya mtanange huo. Kwa matokeo hayo sasa Yanga wanajiandaa kuelekea mjini Algeirs nchini Algeria kucheza mchezo wao wa marudiano dhidi ya klabu hiyo. Na ili waweze kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, watalazimika kupata ushindi au sare yoyote ugenini ili waitoe MC Alger katika mpambano wa April 15 mwaka huu.

Mwanaridha nyota wa Kenya 'alitumia' dawa za kututumua misuli

Ulimwengu wa riadha nchini Kenya unaomboleza. Hii ni baada ya kubainika kuwa, Jemima Sumgong, mwanariadha wa Kenya wa mbio za masafa marefu aliyeshinda medali ya dhahabu katika mbio za Marathon kwa upande wa wanawake wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Rio mwaka jana 2016 nchini Brazil, alitumia dawa za kututumua misuli aina ya (Erythropoietin) EPO. Sumgong mwenye umri wa miaka 32 na bingwa wa mbio za London Marathon, amebainika kuwa alitumia dawa hizo zilizopigwa marufuku baada uchunguzi uliofanywa na Shirikisho la Riadha Duniani IAAF. Sumgong alikuwa mwanamke wa kwanza kuishindia Kenya medali ya dhahabu katika mbio za Marathon, ushindi ambao ulimfanya ajizolee sifa kedekede kitaifa na kimataifa.

Matokeo ya uchunguzi (Doping)

Binafsi aligubikwa na furaha mpwitompwito baada ya kutwaa ushindi huo wa aina yake na kumuacha awe mchache wa kauli. Hili ni pigo kwa mwanariadha huyu ambaye hivi karibuni alitangaza utayarifu wake wa kushiriki mbio za London Marathon tarehe 23 mwezi huu Aprili,  kutetea taji lake aliloshinda mwaka uliopita. Hata hivyo, kizungumkuti kilichoko ni kuwa, uchunguzi wa mara hii wa IAAF unatofautiana  na ripoti za awali zilizoonyesha kuwa mwanariadha huyo alikuwa safi na hakuwahi kutumia dawa zozote za kututumua misuli. Sumgong kwa sasa atalazimika kusubiri uchunguzi wa pili kuhusu dawa hizo za kuongezea mwili nishati, ili ajue hatua za kinidhamu zinazomsubiri na pia hatima yake katika ulimwengu wa riadha.

Ligi Kuu ya Uingereza

Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza msimu huu wa 2016/2017 iliendelea kutema miale ya moto usiku wa April 5 kwa michezo kadhaa kushuhudiwa. Mchuano kati ya Arsenal dhidi ya West Ham United ni miongoni mwa michezo iliyofuatiliwa kwa karibu usiku huo. Aidha kuna pote kubwa lilikuwa linafuatilia mechi kati ya Man City na ChelseaKatika kipute cha Chelsea dhidi ya Man City kilichipigwa katika uwanja wa Stamford Bridge, The Blues walipata  ushindi wa magoli 2-1. Wabeba Bunduki wa Arsenal usiku huo pia walifanikiwa kupata ushindi wao wa kwanza wa Ligi ya Premier baada ya kushuhudia ukame wa ushindi kwa takrban miezi miwili. Arsenal wakiupiga nyumbani uwanja wa Emirates, walifanikiwa kuisasambua West Ham mabao 3-0, ushindi ambao umeiwezesha kurudi nafasi ya tano na kuishusha Man United hadi nafasi ya 6. Hata hivyo hayo yalikuwa ya muda tu, kwani Mashetani Wekundu waliitandika Sunderland mabao 3-0 Jumapili na kurejea tena walikokuwa katika jedwali la EPL. Sunderland ilicheza na kikosi cha watu 10 baada ya Sebastian Larsson kupewa kadi nyekundi alipomchezea visivyo Ander Herrera. Mabao ya Man U yalifungwa na Zlatan Ibrahimovic, Henrikh Mkhitaryan na Marcus Rashford. Sunderland wanatafuta pointi 10 ili kuepuka madhila ya kushushwa daraja, ikizzingatiwa kuwa, wana mechi 7 pekee za kucheza huku saba wazlizocheza, wakikosa kutikisa nyavu. Man U imeipiku Arsenal ikiwa pointi nne nyuma ya Manchester City.

…………………………….…..TAMATI..……………………….