Apr 10, 2017 11:24 UTC

Sura ya Luqman, aya ya 1-6 (Darsa ya 730)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Baada ya kuhatimisha tarjumi na maelezo ya sura ya 30 ya Ar-Rum, katika darsa hii ya 730 tutaanza kutoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 31 ya Qur'ani tukufu ya Luqman. Sura hii iliteremshwa Makka na ina aya 34. Suratu Luqman, mbali na kuashiria ishara na aya za uwezo na adhama ya Allah SW katika uumbaji wa mbingu na ardhi na viumbe mbalimbali, imenukuu pia sehemu ya mawaidha ya hekima ya Luqman kwa mwanawe; na kwa sababu hiyo imepewa jina la Luqman. Baada ya utangulizi huo mfupi, tunaianza darsa yetu sasa kwa aya ya kwanza hadi ya tatu ya sura hiyo ambazo zinasema:

الم

Alif Lam Mim (A.L.M.)

تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ الْحَكِيمِ

Hizo ni Aya za Kitabu chenye hikima.

هُدًى وَرَحْمَةً لِّلْمُحْسِنِينَ

Ni Uwongofu na Rehema kwa wafanyao wema,

Kama tulivyowahi kueleza mara kadhaa katika darsa zetu zilizopita, kuna sura 29 ndani ya Quráni tukufu ambazo zimeanza kwa herufi za mkato; na Suratu Luqman ni miongoni mwa sura hizo. Herufi za mkato zinabainisha adhama ya Quráni, kwamba kitabu hiki kimetokana na herufi hizi hizi za alfabeti za Kiarabu, lakini pamoja na hayo ni muujiza mkubwa wa Mwenyezi Mungu ambao hakuna mwanadamu yeyote mwenye uwezo wa kuleta mfano wake. Ni kitabu ambacho aya zake katika sura hii na sura nyingine za Qur'ani zimebeba hekima kubwa. Na sababu ni kuwa zimeteremshwa na Mwenyezi Mungu mwenye hekima na zina mashiko imara na ukwasi wa kujitosheleza. Neno lolote la batili halipatikani ndani yake, ni kitabu kilicho mbali na khurafa na uzushi na hakizungumzi kingine ghairi ya haki, wala hakiwaiti na kuwalingania watu ghairi ya njia ya haki.

Japokuwa Quráni imeletewa kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu wote kwenye uongofu lakini wanaoweza kunufaika na uongofu wa kitabu hicho ni watu walio safi na wema. Watu wachafu na waovu, ima hawako tayari kusikiliza na kusoma aya za kitabu hicho au kama watazisikiliza na kuzisoma basi nyoyo na roho zao ni chafu kiasi kwamba hawazikubali bali wanazipa mgongo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuwafikishia watu wito wa uongofu kunapasa kufanyike kwa kutumia hekima inayoambatana na hoja madhubuti. Ni kwa sababu hiyo Quráni yenyewe imejiita kitabu chenye hekima. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuwaelimisha na kuwaongoza watu kwenye uongofu kunatakiwa kuambatane na huruma na upendo ili kuweze kuwa na taathira kubwa zaidi kwao.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 4 na ya 5 ambazo zinasema:

الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَهُم بِالآخِرَةِ هُمْ يُوقِنُونَ

Ambao wanashika Sala, na wanatoa Zaka, nao wana yakini na Akhera.

أُوْلَئِكَ عَلَى هُدًى مِّن رَّبِّهِمْ وَأُولَئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

Hao ndio walio na uwongofu utokao kwa Mola wao Mlezi, na hao ndio wenye kufaulu. 

Aya hizi, kwa kuanzia, zinaeleza maana ya neno "muhsinin" lililotajwa katika aya zilizopita kwa kubainisha kuwa ihsani na wema vimegawika katika sehemu mbili. Moja ni ya amali na matendo na nyingine ni ya imani na itikadi.  Sehemu ya amali inajumuisha Sala na Zaka na sehemu ya itikadi inajumuisha imani juu ya akhera.

Kimsingi, katika utamaduni wa dini, kumwabudu Allah kupitia ibada za kiroho hakutenganiki na matendo ya kuwashughulikia waja wa Allah; na kila moja kati ya mawili haya lina ulazima kwa ajili ya ukamilifu wa jingine. Kwa masikitiko, katika dunia ya leo kuna watu wengi ambao ni waswahilina wa kushika Sala, kuvuta nyuradi na kudumu misikitini, lakini hawawajali wala kuwasaidia wahitaji na wanyonge katika jamii. Wao hudhani kule kufanya kwao ibada hizo za kiroho tu kunatosha.

Mkabala na watu hao kuna wale ambao wanajitahidi kuwafikiria na kuwatatulia watu wanyonge na wahitaji matatizo waliyonayo, lakini hawashughuliki kabisa kutekeleza maamrisho ya dini yakiwemo ya Sala, kumtaja na kumkumbuka Mola. Kwa mintarafu ya tuliyoyaeleza, aya tulizosoma zinasema, watu watakaoneemeka na uongofu maalumu wa Allah na watakaofuzu na kuifikia saada ni wale ambao, mbali na kutoa Zaka na kuwatendea watu wema, huwa ni wasimamishaji Sala na wenye kumwabudu Mola wao na wanaizingatia na kuifikiria akhera katika matendo yao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika utamaduni wa Kiislamu Sala na Zaka havitenganiki. Kusimamisha Sala na kutoa Zaka unapasa uwe mwenendo wa kudumu wa watu wenye imani ya kweli. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa waja wema wa kweli ni wale wanaofikiria matatizo ya watu na kujaribu kuwatatulia, na wakati huo huo wanazingatia wajibu wao wa ibada za kiroho na kimaanawi; si kulitoa mhanga moja kwa ajili ya jingine. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kufuzu na uokovu umefungamana na imani juu ya Allah na Siku ya Kiyama pamoja na kutekeleza faradhi za dini kama kusimamisha Sala na kutoa Zaka. Imani tupu bila ya amali au amali tu bila ya imani; kila kimoja peke yake hakitoshi kumuokoa mtu.

Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 6 ambayo inasema:

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّخِذَهَا هُزُوًا أُوْلَئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ

Na miongoni mwa watu wapo wanao nunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu pasipo kujua, na wanaichukulia ni mzaha. Hao watapata adhabu ya kuwafedhehesha.

Aya hii inaashiria moja ya mambo muhimu ya upotoshaji watu ambalo ni maneno ya batili. Imesimuliwa kwenye vitabu vya historia kwamba baadhi ya wafanyabiashara Waarabu wa Hijazi walikuwa wakisafiri kwenda maeneo mbalimbali kama Iran na kujifunza simulizi za habari za ngano za mashujaa wa Kiirani kama Rostam na Esfandiyar pamoja na maisha ya wafalme wao wa kale. Baada ya wafanyabiashara hao wa Kikureishi kurudi Makka walikuwa wakiwakusanya watu na kuwaambia: Kama Muhammad anasimulia habari za kina Aad na Thamudi, sisi pia tunazo hekaya, tena za kusisimua zaidi za kukusimulieni nyinyi. Kwa kutumia mbinu hiyo, walikuwa wakijaribu kuwaweka mbali watu na Bwana Mtume Muhammad SAW pamoja na kuwazuilia kusikiliza aya za Quráni. Sawa kabisa na walivyokuwa wakifanya baadhi ya waimbaji wanawake, waliokuwa wakighani mashairi ya ashiki na nyimbo za kupumbaza na kusisimua ili kuwafanya watu wasishughulike na Bwana Mtume wala kusikiliza aya tukufu za Quráni. Bali hata kwenda mbali zaidi kwa kumfanyia shere na stihzai Mtume wa Allah pamoja na maneno matukufu ya Mola na kuyataja kuwa kitu kisicho na thamani. Aya hii inaeleza kuwa watu ambao kwa namna yoyote ile wanawazuilia watu njia ya Mwenyezi Mungu na kuzielezea aya za Mola kuwa kitu kisicho na mashiko wala thamani au hata kuzifanyia istihzai, watapata adhabu kali na kuwafanya wawe dhalili duniani na akhera.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba maneno yoyote ya kupumbaza, yawe na mahadhi ya kughani au yasiwe ya kughani, yanayomweka mtu mbali na njia ya haki, yakamghafilisha nayo na kumpotosha, yamekatazwa na dini. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, moja ya vitu vinavyopotosha watu hasa vijana ni kusikiliza nyimbo ambazo muziki na mashairi ya mwimbaji wake ni ya maneno yasiyofaa na ya batili, ambayo humghafilisha mtu na Mwenyezi Mungu na kumfanya apumbazike na shahawa na matamanio ya kidunia. Aidha aya hii inatuelimisha kwamba katika kupambana na fikra na itikadi za Kiislamu, adui anatumia kwa kiwango kikubwa nyenzo za kiutamaduni za matamshi na maandiko na kuzieneza katika jamii katika sura tofauti za sanaa kama filamu, muziki na maigizo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 730 ya Quráni imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa Waislamu wa kweli, wa imani sahihi na matendo ya ikhlasi, wanaotekeleza ipasavyo ibada za kiroho za binafsi na kushughulikia itakiwavyo matatizo ya wahitaji katika jamii. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags