Apr 10, 2017 11:35 UTC

Sura ya Luqman, aya ya 12-13 (Darsa ya 732)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 732 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 31 ya Luqman. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 12 ambayo inasema:

وَلَقَدْ آتَيْنَا لُقْمَانَ الْحِكْمَةَ أَنِ اشْكُرْ لِلَّهِ وَمَن يَشْكُرْ فَإِنَّمَا يَشْكُرُ لِنَفْسِهِ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّهَ غَنِيٌّ حَمِيدٌ

Na hakika tulimpa Luqman hikima, tukamwambia: Mshukuru Mwenyezi Mungu. Na mwenye kushukuru basi hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake. Na aliye kufuru, basi Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Msifiwa.

Aya hii na nyingine kadhaa zinazofuatia zinamzungumzia Luqman na kunukuu mawaidha na nasaha alizompa mwanawe. Kwa mujibu wa maelezo yaliyokuja katika aya za Quráni na hadithi Luqman hakuwa Mtume, lakini alikuwa mtu mwema na mchamungu ambaye alitunukiwa hekima na Allah. Hekima ni basira na uono mpana na wa kina unaopatikana chini ya kivuli cha mafundisho ya dini; na athari zake huonekana katika maneno na matendo ya mtu. Kuchunga ulimi, kulidhibiti tumbo na ulafi, kuzidhibiti shahawa na matamanio, kuwa mwaminifu na mnyenyekevu na kujiweka mbali na mambo ya lahau na upuuzi ni miongoni mwa sifa zinazopelekea kujengeka hekima ndani ya nafsi ya mtu. Tabán kufikia hadhi na daraja ya kuwa na hekima hakuhusiani na Luqman peke yake; bali kwa mujibu wa hadithi muumini yeyote ambaye atakuwa mkweli na mwenye ikhlasi katika maneno na matendo yake Allah SW humtunukia neema hiyo kubwa. Pamoja na kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu angeweza kuzinukuu Yeye mwenyewe moja kwa moja ndani ya Quráni nasaha zilizotolewa na Luqman, lakini amezinukuu kupitia kwenye kinywa cha Luqman mwenyewe nasaha alizompa mwanawe ili sisi tuweze kubainikiwa na maana halisi ya hekima na pia kuelewa jukumu la wenye hekima katika kuwaaidhi na kuwaongoza watu.

Kwa muhtasari, nasaha na wasia wa Luqman kwa mwanawe umekusanyika katika mambo mawili. La kwanza ni kuwa mwangalifu na mwenye nadhari katika uzungumzaji na kuwa mwangalifu pia katika miamala na milahaka ya kifamilia na kijamii. Na la pili ni kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu katika maisha. Hii ndio maana ya hekima; na mwenye hekima halisi ni mtu mwenye sifa mbili kuu hizi na ambaye huwalingania na kuwausia watu pia wajipambe kwa sifa hizo.

Ni wazi kwamba kufikia kwenye daraja hii, na ili kuweza kutunukiwa neema kubwa kama hiyo kunataka mtu awe mkithirishaji wa hamdu na shukrani kwa Allah SW. Na ushukurivu wa kweli unathibiti kwa mja kuitumia mahala pake kila neema aliyojaaliwa. Na faida ya kufanya hivyo humrudia mtu mwenyewe kwa kujengeka na kutukuka kiroho na kimaanawi; kama ambavyo kuitumia neema isivyo na pasipostahiki huwa ni kuikufuru neema hiyo hata kama mtu atamshukuru Mola kwa ulimi kwa kusema Alhamdulillah. Na sababu ni kwamba, kushukuru tu kwa mdomo huwa hakuna faida yoyote wakati mtu anakufuru kivitendo; na madhara ya kufanya hivyo yanamrejea mtu mwenyewe, si Mwenyezi Mungu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba watu wa kawaida nao pia wanaweza kupata rehma maalumu za Allah endapo watajipamba kwa sifa njema za uchaMungu, usafi wa nafsi na utakasifu wa matendo hata kama hawatokuwa na daraja za juu za elimu na ujuzi. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa faida na hasara ya amali anazofanya mja zinamrejea yeye mwenyewe. Vivyo hivyo athari za kushukuru au kukufuru neema za Allah zinamrejea mtu mwenyewe na si Mola anayemshukuru au kumkufuru kwa kumjaalia neema hizo.

Wapenzi wasikilizaji, aya ya 13 ya sura yetu hii ya Luqman ndiyo inayotuhatimishia darsa yetu ya leo. Aya hiyo inasema:

وَإِذْ قَالَ لُقْمَانُ لِابْنِهِ وَهُوَ يَعِظُهُ يَا بُنَيَّ لا تُشْرِكْ بِاللَّهِ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

Na Luqman alipo mwambia mwanawe kwa kumpa mawaidha: Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu. Kwani hakika shirki ni dhulma kubwa. 

Usia na nasaha ya kwanza ya Luqman kwa mwanawe ni kumtaka ajiweke mbali na shirki.  Ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu, iwe ni katika imani na itikadi au katika amali na matendo. Kuabudu masanamu, kuliabudu jua, mwezi na nyota na hata wanyama ni mambo yaliyokuwa yameenea katika zama mbalimbali za historia katika kaumu tofauti za watu. Kuna watu wengi ambao kwa sababu ya ujinga na kutokuwa na uelewa wanadhani kwamba vitu hivyo visivyo na uhai au baadhi ya viumbe hai vina taathira katika maisha na majaaliwa yao. Kutokana na kuwa na imani hiyo wanavipa vitu au viumbe hivyo hadhi fulani ya uola katika uendeshaji wa masuala ya ulimwengu na ya wanadamu na hivyo kuviomba na kuviabudu.

Lakini mbali na watu hao, kuna Waislamu na waumini wengi wenye imani ya tauhidi ya Mungu mmoja lakini wanafanya shirki katika amali na matendo yao hata kama hawapigi magoti na kumsujudia asiyekuwa Allah. Watu hao ni watumwa wa mali, utajiri na madaraka; na wako tayari kufanya dhambi na uovu wowote ule almuradi waweze kuyafikia na kuyatia mkononi hayo wanayoyatamani.

Kwa kuwa Luqman anajua madhara na maafa ya shirki, kabla ya kuanza kutoa mawaidha yake ya kiakhlaqi, anamhadharisha mwanawe na kila aina ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kulitaja jambo hilo kuwa ni dhulma kubwa mno. Dhulma ambayo, kwanza inamsababishia madhara mtu mwenyewe na kisha kwa Mitume wa Allah na dini yake Mola. Nukta moja ya kuvutia ni kwamba aya hii inazungumzia kwa njia isiyo ya moja kwa moja jukumu la wazazi katika malezi ya watoto wao na juu ya kuwafunza imani na itikadi sahihi. Tabán ni muhimu pia kuzingatia mbinu ya ufundishaji. Kwa mfano, mbinu ya mawaidha na nasaha ni yenye taathira kubwa zaidi kuliko ya utumiaji lugha ya uamrishaji na ukaripiaji; lugha ya mawaidha inakubaliwa zaidi na watoto wenyewe. Na hasa mzazi anapotumia maneno ya upendo kama mwanangu, binti yangu mpenzi n.k. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kila mtu anahitaji mawaidha. Kwa mujibu wa historia, baadhi ya wakati Imam Ali (as) alikuwa akiwaambia wafuasi wake: "Niusieni, kwani katika kusikiliza kuna athari ambayo haipatikani kwa njia ya kujua". Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa tujifunze kwa viongozi wa dini na watu wenye hekima njia za malezi ya watoto. Kwa kufanya hivyo hatutokosea sana katika kutekeleza jukumu hilo zito na hasasi. Aya hii aidha inatutaka tusijisahau tukaghafilika na suala la kushughulikia watoto wetu. Watoto wanahitaji mawaidha na nasaha za wazazi. Na njia moja bora ya malezi ya mtoto ni kumfanya ajihisi ana hadhi, kuamiliana naye kwa upendo na kuzungumzia naye kwa mapenzi.

Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 732 ya Quráni imefikia tamati. Tunamwomba Allah awaongoe watoto wetu. Awajaalie kuwa sababu ya sisi kutajwa na kukumbukwa kwa wema baada ya kufa kwetu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags