Apr 10, 2017 11:39 UTC

Sura ya Luqman, aya ya 14-16 (Darsa ya 733)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 733 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 31 ya Luqman. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 14 ambayo inasema:

وَوَصَّيْنَا الإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَى وَهْنٍ وَفِصَالُهُ فِي عَامَيْنِ أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ إِلَيَّ الْمَصِيرُ

Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. Kwamba unishukuru Mimi na wazazi wako. Ni kwangu Mimi ndiyo marudio.

Katika darsa iliyopita tulianza kusimulia nasaha na mawaidha aliyotoa Luqman kumpa mwanawe. Aya hii ya 14 na inayofuatia ya 15 ya sura hii ni mithili ya tungo ingilifu iliyokuja baina ya sehemu mbili za mawaidha ya Luqman lakini pasina kuathiri maelezo ya mwanzo na mwisho wake. Kwa kuzingatia kuwa Luqman alikuwa akimpa nasaha mwanawe kama mzazi na kumhadharisha na shirki, katika aya hizi mbili, Allah SW kwanza anawatanabahisha watoto kuhusu thamani ya wazazi wao kisha kuhusu nafasi ya wazazi katika kuwapa malezi ya kidini watoto wao. Aya hii inasema: Mwenyezi Mungu ameusia kuhusu wazazi kwa sababu anawaumba watoto kupitia wazazi wao wawili ambao kila mmoja anachangia katika kutunga mbegu ya uzazi ya mtoto wao. Tab'an baada ya kutunga mbegu hiyo, mama ndiye anayebeba mzigo wa miezi tisa wa mimba na wa kipindi cha miaka miwili ya kumnyonyesha mtoto kwa kumdhaminia lishe yake kwa maziwa yake mwenyewe na kumlea na kumkuza kwa mahaba na mapenzi ya mama kwa mwana. Hivyo aya inaendelea kwa kuashiria tabu na mashaka anayopata mama, ambayo humwathiri mno kimwili na kiroho na kumfanya adhoofu na kunyong'onyea na kumuusia mtoto amzingatie na kumfikiria zaidi mama yake. Alaa kulli hal, mbali na kutakiwa kuwa washukurivu kwa neema za Allah, tunapaswa tushukuru pia kwa uwepo wa wazazi wetu wawili na kutokana na tabu na mashaka wanayopata kwa ajili yetu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kuwaheshimu wazazi ni haki ya kiutu; hivyo mtoto ana wajibu wa kuwatendea wema wazazi wake hata kama ni makafiri, na hana haki ya kuwadharau na kuwavunjia heshima. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa katika utamaduni wa Kiislamu mama ana hadhi na nafasi maalumu kwa sababu ndiye anayehangaika na kumtaabikia zaidi mtoto na kuchangia zaidi katika uhai na uzima wa mtoto huyo. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba haki za Mwenyezi Mungu zinatangulia haki za wazazi katika hali yoyote ile; hivyo kuwashughulikia na kuwatendea wema wazazi kusije kukatughafilisha na Mola ambaye ni Muumba wetu sote, sisi na wazazi wetu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 15 ambayo inasema:

وَإِن جَاهَدَاكَ عَلَى أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلا تُطِعْهُمَا وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا وَاتَّبِعْ سَبِيلَ مَنْ أَنَابَ إِلَيَّ ثُمَّ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ

Na pindi wakikushikilia kunishirikisha na yale ambayo huna ilimu nayo, basi usiwat'ii. Na kaa nao kwa wema duniani, na fuata njia ya anaye elekea kwangu. Kisha marejeo yenu ni kwangu Mimi, na Mimi nitakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.

Aya hii inaendelea na maudhui ya aya iliyotangulia  kwa kuwatahadharisha watoto kuwa kuusiwa wawe na uhusiano mzuri na wazazi wao kusiubane na kuuondoa uhuru wao wa kifikra; ikawa chochote kile wakisemacho baba na mama watoto wanakikubali; na kutii kila mila na desturi za wazee wao waliotangulia pasina kuhoji na kutafakari. Kwani si hasha wazazi wakawa na fikra batili na imani potofu na wakataka kuwalazimisha watoto wao pia wakubali na kuzifuata itikadi hizo. Kwa sababu hiyo, Allah SW ambaye ni Muumba wa wanadamu wote anamkataza mtoto asikubali kufuata imani na itikadi potofu za wazazi wake kwa kuchelea kuharibika uhusiano na mapenzi ya kifamilia aliyonayo kwa wazazi wake. Asifanye hivyo hata kama wazazi wake watamkasirikia na kuamua kumtenga katika familia. Kisha aya inaendelea kueleza kuwa pamoja na hayo ikiwa wazazi wake mtu ni makafiri au washirikina anatakiwa aamiliane na kulahikiana nao kila mara kwa namna inayopendeza. Katika hali na mazingira yoyote yale, mtoto hana haki ya kuvunja uhusiano na wazazi wake, bali anatakiwa katika muda wote wa uhai wao, aamiliane nao kwa wema na kujiepusha na kuwatolea ukali au kuwafanyia kitendo chochote cha kuwavunjia heshima. Hesabu ya wazazi wa aina hiyo iko kwa Mola mwenyewe. Yeye ni mjuzi na muelewa wa kila kitu. Ama kwa upande wa mtoto, ajiepushe kuwafanyia ubaya wowote wazazi wake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kuwatii wazazi kumewekewa sharti, si kwa kila wanaloamuru! Takwa la wazazi kwa mtoto wao linabaki kuwa na thamani na itibari lisipopingana na takwa la Allah SW. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kufuata mila na desturi za waliotangulia kwa sura ya utamaduni wa taifa au jina jengine lolote lile huwa na thamani endapo hayo yanayofuatwa na kuendelezwa yatakuwa hayapingani na akili na dini; vinginevyo ufuataji huo wa yaliyorithiwa kwa waliotangulia utakuwa ni wa kibubusa, kiupofu na usio na mantiki. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba kwa mtazamo wa Uislamu kuishi kwa amani na masikilizano na wasio Waislamu kunajuzu endapo katika michanganyiko na maingiliano na watu hao, Waislamu hawatoathiriwa na imani na itikadi zao na kufuata mila na utamaduni wao. 

Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 16 ambayo inasema:

يَا بُنَيَّ إِنَّهَا إِن تَكُ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ فَتَكُن فِي صَخْرَةٍ أَوْ فِي السَّمَاوَاتِ أَوْ فِي الأَرْضِ يَأْتِ بِهَا اللَّهُ إِنَّ اللَّهَ لَطِيفٌ خَبِيرٌ

Ewe mwanangu! Kikiwapo kitu cha uzito wa chembe ya khardali kikawa ndani ya jabali au mbinguni au ardhini, basi Mwenyezi Mungu atakileta. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyo fichika, Mwenye khabari za yote.

Kwa kawaida mtu anapohesabu na kutathmini mambo mema na mazuri anayofanya humjia machoni mwake yale mambo makubwa makubwa tu na kughafilika na matendo madogo ya wema. Ilhali kurudia na kudumisha kufanya mambo hayo madogo ndiko kunakochangia kutenda matendo makubwa. Na kama yalivyo mambo makubwa, matendo madogo madogo, nayo pia yana uzito na taathira kwa hatima na majaaliwa ya mtu. Aya hii ya 16 tuliyosoma inaendelea kusimulia nasaha na mawaidha ya Luqman kwa mwanawe, akizungumzia umakini mkubwa wa Allah katika kuhesabu amali za waja wake. Luqman anasema kumwambia mwanawe: Ewe mwanangu! Amali yoyote uifanyayo, iwe kubwa au ndogo, uifanye kwa siri au dhahiri haina tofauti yoyote mbele ya Mwenyezi Mungu. Amali hata yenye udogo wowote ule unaotasawarika uliyoifanya mahala penye usiri wa kiwango cha juu kabisa haiwezi kufichika katika elimu ya Mwenyezi Mungu, Mjuzi wa kila kitu. Allah SW ataidhihirisha amali hiyo katika Mahakama yake ya Siku ya Kiyama na kukulipa thawabu au adhabu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kuwatanabahisha watoto juu ya mahakama ya Siku ya Kiyama na kuhusu hesabu ya amali zao ni moja ya majukumu ya wazazi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa amali zote anazofanya mwanadamu, ziwe kubwa au ndogo. Kuamini mtu Siku ya Kiyama na juu ya kuhesabiwa kwa makini na Mola amali alizofanya ni mwanga wa kunyookewa katika maisha yake. Wa aidha tunajifunza kutokana na aya hii kwamba amali za mwanadamu hazipotei, bali amali zenyewe pamoja na athari zake zitaandamana na mtu hadi Siku ya Kiyama. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 733 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atutakabalie amali zetu, atughufirie madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags