Apr 10, 2017 11:43 UTC

Sura ya Luqman, aya ya 17-19 (Darsa ya 734)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 734 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 31 ya Luqman. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 17 ambayo inasema:

يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنكَرِ وَاصْبِرْ عَلَى مَا أَصَابَكَ إِنَّ ذَلِكَ مِنْ عَزْمِ الأُمُورِ

Ewe mwanangu! Simamisha Sala, na amrisha mema, na kataza maovu, na subiri kwa yanayo kusibu. Hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa.

Katika darsa mbili zilizopita tuliashiria baadhi ya nasaha na mawaidha aliyotoa Luqman kumpa mwanawe. Baada ya kutilia mkazo kwanza misingi ya itikadi, katika aya hii ya 17 tuliyosoma, Luqman anazungumzia masuala muhimu zaidi ya kiibada na kijamii na kumwambia mwanawe: Baada ya kuiamini tauhidi, wajibu wa kwanza ulionao ni kumwabudu Mwenyezi Mungu Mola wa ulimwengu na kumwomba na kutaradhia kwake, ambako kunafanyika kwa njia ya Sala. Sala inakuunganisha wewe na Mwenyezi Mungu na kuifanya imani ndani ya moyo wako iwe imara.

Tabán Sala peke yake haitoshi; na haitoshi pia wewe kuwa mtu kuifikiria nafsi yako mwenyewe tu.  Inapasa uwalinganie na wenzako pia kufanya amali hiyo njema pamoja na amali nyingine za kheri ili mema na mazuri yaenee katika jamii. Kama ambavyo unatakiwa upambane na mabaya na maovu na kutoruhusu yarasimike na kukubalika katika jamii. Kwa kawaida kujishughulisha na harakati za kijamii sambamba na kufanya juhudi na hima ya kueneza mambo mema na ya kheri na kuzuia kuzagaa mambo maovu na machafu kuna misukosuko na matatizo yake; kwa sababu watu waovu hutumia kila njia wanayoweza kupinga na kukabiliana na haki. Pamoja na hayo watu waumini hawapaswi kurudi nyuma wakati wanapokabiliwa na matatizo na masaibu, bali wanatakiwa wasimame imara na kuwa thabiti katika njia ya haki ili jitihada wanazofanya zizae matunda. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kuwa na azma na irada imara ya kuweza kufikia lengo la kidini ni miongoni mwa mambo ya lazima ya imani juu ya Allah; na bila ya kuwa na azma na irada hiyo hakuna harakati yoyote itakayoweza kuwa na tija. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kumuusia mtoto Sala na kulifuatilia jambo hilo ni moja ya majukumu ya wazazi.

Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba inatakiwa tuwalee watoto wetu kwa namna ambayo watajihisi wana mas-ulia juu ya masuala ya jamii na hawatoyapita vivi hivi mambo mema na maovu yanayofanywa katika jamii yao.

Ifuatayo sasa ni aya ya 18 ambayo inasema:

وَلا تُصَعِّرْ خَدَّكَ لِلنَّاسِ وَلا تَمْشِ فِي الأَرْضِ مَرَحًا إِنَّ اللَّهَ لا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ

Wala usiwapindie uso watu kwa kuwabeua, wala usitembee katika nchi kwa maringo. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila anaye jivuna anayejifakharisha.

Katika aya hii tuliyosoma, Luqman anaashiria baadhi ya tabia mbaya na chafu za kimaadili na kumtaka mwanawe ajiepushe nazo. Ghururi na kiburi ambavyo vinatokana na mtu kujiona bora na wa juu ni chanzo cha mienendo mingi ya kijamii. Katika aya hii ya 18 ya Suratu Luqman imetajwa mifano miwili ya tabia hizo mbaya: moja ni kutowajali watu na kuwadharau kwa kuwadunisha na kuwaona si lolote si chochote. Baadhi ya watu hujengeka na hulka hiyo kutokana na kupata umaarufu, utajiri au madaraka. Watu wa aina hiyo hujidhani kwamba kwa dhati yao halisi, wao ni bora na wa juu kuliko watu wengine. Jambo jengine analoliashiria Luqman ni namna ya utembeaji mbele za watu. Baadhi ya watu, badala ya kuwa na upole na unyenyekevu, huwa wanatembea kwa ghururi, majigambo na majivuno utadhani wao ndio mabwana wa watu wote na kila mtu inapasa awanyenyekee na kujidhalilisha mbele yao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kulahikiana na watu kwa uzuri ni miongoni mwa nasaha na wasia wa Luqman kwa mwanawe. Allah SW ameikumbusha nasaha hii ya hekima ikiwa na maana ya kuwaagiza watu wote wapambike na sifa hii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa wazazi wanapaswa wawalee watoto wao kuanzia rika lao la uchipukizi kwa namna ambayo hawatoathirika na maradhi ya kiakhlaqi yakiwemo ya kiburi na ghururi.

Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 19 ambayo inasema:

وَاقْصِدْ فِي مَشْيِكَ وَاغْضُضْ مِن صَوْتِكَ إِنَّ أَنكَرَ الأَصْوَاتِ لَصَوْتُ الْحَمِيرِ

Na ushike mwendo wa katikati, na teremsha sauti yako. Hakika sauti mbaya zaidi ni sauti ya punda.

Baada ya Luqman kumkataza mwanawe kwa kumtaka ajiepushe na tabia mbili chafu, katika aya hii anamtaka ajipambe na mambo mawili mema ya kiakhlaqi kwa kumwambia: Katika mwenendo na harakati za maisha, uwe mtu wa kadiri na wastani. Katika safari ya maisha, usiwe mtu wa kufurutu mpaka wa kufanya mambo kupindukia au kuwa na ajizi isiyo na kiasi ukawa mtu mvivu na goigoi. Usiwe na mwendo wa kasi ya pupa, wala wa kusuasua na kujikongoja; tembea mwendo wa wastani na wa kimaumbile.

Na si katika mwenendo tu bali hata katika uzungumzaji wako pia, kuwa mtu wa kuchunga kadiri na wastani. Usizungumze taratibu mno na kwa sauti ya chini mpaka watu wakashindwa kusikia unayosema, wala usipaze sauti juu mpaka ukawakera na kuwaudhi watu. Usidhani kama watu wanapendezwa na kufurahi unapopaza sauti na kuzungumza kwa makelele na kwa hivyo wanayakubali uyasemayo. Sauti mbaya na inayochukiza zaidi mbele za watu ni sauti ya punda kwa sababu ni kubwa zaidi kuliko maumbile.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba miongoni mwa mambo yanayowalazimu wazazi kuwafunza watoto wao ni kuchunga adabu za kijamii kuhusu namna ya kutembea na namna ya kuongea. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kujiepusha na mwenendo wa kufurutu mpaka kwa kushadidisha kupindukia au kuhafifisha kupindukia katika ufanyaji mambo na badala yake kufanya mambo kwa kadiri na wastani ni miongoni mwa masuala ambayo Allah SW ameyausia katika Kitabu chake cha Quráni. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba kupaza sauti na kupiga makelele kumekemewa na ni jambo lisilopendeza mbele ya Allah. Inatakiwa tushushe sauti zetu, tujiepushe kupiga makelele yasiyo na faida na kuzungumza kwa upole na utulivu.

Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 734 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwezeshe kupambika kwa tabia na akhlaqi njema katika maneno na matendo yetu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags