Apr 18, 2017 06:58 UTC
  • Jumanne, 18 Aprili, 2017

Leo ni Jumanne tarehe 20 Rajab 1438 Hijria sawa na Aprili 18, 2017

Miaka 21 iliyopita katika siku kama ya leo, jeshi la anga la utawala wa Kizayuni wa Israel lilishambulia makao ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika kijiji cha Qana, kusini mwa Lebanon. Katika shambulizi hilo la kinyama la Wazayuni, takribani raia 110 wa Lebanon waliuawa shahidi wakiwemo wanawake na watoto. Licha ya hayo, Marekani ilizuia kupasishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa azimio la kulaani mauaji ya kijiji cha Qana yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Mauji ya Qana

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 18 Aprili 1980, Zimbabwe ambayo wakati ule ilikuwa ikijulikana kwa jina la Rhodesia, ilipata uhuru. Zimbabwe ilikoloniwa na Uingereza mwishoni mwa karne ya 19. Mara baada ya Vita vya Pili vya Dunia na kufuatia kudhoofika Uingereza, zilianza harakati za wananchi za kupigania uhuru na hatimaye harakati hizo zilipelekea kuundwa makundi ya mapambano ya silaha. Zimbabwe ina ukubwa wa zaidi ya kilomita mraba 390,000 na inapakana na nchi za Msumbiji, Zambia, Botswana na Afrika Kusini. 

Bendera ya Zimbabwe

Katika siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, mkutano wa kwanza wa wawakilishi wa nchi za Asia na Afrika uliojulikana kwa jina la Mkutano wa Bandung ulifanyika katika mji wenye jina hilo nchini Indonesia. Mkutano huo uliowashirikisha wajumbe kutoka zaidi ya nchi 29 za Asia na Afrika, ulikuwa na lengo la kujenga umoja wa nchi hizo za ulimwengu wa tatu katika kukabiliana na kambi kubwa mbili duniani za Mashariki na Magharibi. Mkutano wa Bandung ndio ulioandaa mazingira ya kuundwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM). 

Mkutano wa Bandung

Miaka 63 iliyopita katika siku kama ya leo, Gamal Abdel Nasser alifanya mapinduzi dhidi ya Muhammad Naguib na kuwa Rais wa nchi hiyo. Gamal Abdel Nasser ndiye aliyeitafisha na kuitangaza kuwa mali ya taifa Kanali ya Suez na alikuwa na nafasi muhimu katika juhudi za kukabiliana na ubeberu katika ulimwengu wa Kiarabu na barani Afrika. Aidha Rais huyo wa zamani wa Misri alikuwa na nafasi muhimu katika kuasisiwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM.

Gamal Abdel Nasser

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, alizaliwa Ayatullah Sayyid Ali Husseini Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika mjini wa Mash'had huko kaskazini mashariki mwa Iran. Alipata malezi bora katika familia ya kidini na kuanza kusoma akiwa na umri wa miaka minne. Sayyid Ali Khamenei alianza masomo ya dini chini ya usimamizi wa baba yake na kupiga hatua zaidi za maendeleo katika uwanja huo. Hatimaye alielekea katika mji mtakatifu wa Qum na kuendelea na masomo ya juu kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kwa muda wa miaka saba. Wanazuoni kama Imam Khomein MA, Ayatullahil Udhma Burujardi na Allamah Tabatabai ni miongoni mwa wasomi ambao Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alipata elimu kutoka kwao. Katika kipindi cha ujana wake Ayatullah Sayyid Ali Husseini Khamenei alijiunga na harakati za Imam Khomein MA za kuupinga utawala wa kidikteta wa Shah. Alieneza fikra za Imam Khomein na kufichua ufisadi wa viongozi waliokuwa katika utawala wa wakati huo. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikamatwa na kutiwa gerezani mara kadhaa.

Ayatullah Ali Khamenei

Na miaka 1425 iliyopita katika siku kama hii ya leo, vilitokea vita vya Yarmuk kati ya jeshi la Kiislamu na jeshi la utawala wa kifalme wa Roma ya Mashariki katika bonde lililojulikana kwa jina hilo huko Palestina. Ushindi wa Waislamu huko Sham, yaani Syria ya sasa ulimpelekea mfalme wa Roma kuandaa jeshi kubwa kwa ajili ya kupigana na Waislamu. Lakini, Waislamu waliweza kutoa pigo kwa wanajeshi wa mfalme wa Roma licha ya kuwa na idadi ndogo ya wapiganaji na suhula chache za kivita. Kufuatia ushindi huo Waislamu walisonga mbele na kufika eneo la Mashariki la Ufalme wa Roma na mwaka mmoja baada ya hapo Waislamu wakafanikiwa kuchukua udhibiti wa mji wa Baitul Muqaddas pasina umwagaji damu.

Vita vya Yarmuk