Ulimwengu wa Spoti, Apr 24
Karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri wiki hii ndani na nje ya nchi....
Iran yatwaa ubingwa wa taekwondo barani Asia
Timu ya taifa ya vijana ya taekwondo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa mashindano ya kieneo ya mchezo huo nchini Kazakhstan. Mabinti wa Iran wamezoa pointi 80 na jumla ya medali 6 za dhahabu katika mashindano hayo na hivyo kuibuka kidedea. Dhahabu hizo zilitiwa kibindoni na wanataekwondo mabingwa wa Kiirani Mobina Nejad Katesari, Zahra Shojaei Rad, Zahra Alizadeh, Mobina Shakeri, Yalda Valinejad na Zahra Pouresmaeil kwa upande wa akina dada katika vitengo vya kilo zisizodizi 42, 63, 46, 55, 59 na kilo zaidi ya 68 kwa usanjari huo. Na kama hilo halitioshi, binti mwingine wa Kiirani Mahla Mo’menzadeh alinyakua medali ya fedha baada ya kuibuka wa pili katika safu ya kilo zisizozidi 44 alipochezea mkong'oto kutoka hasimu wake wa Thailand, Wilasinee Kamjanghan. Thailand iliibuka ya pili ikiwa na alama 43 huku orodha ya tatu bora ikifungwa na Korea Kusini iliyokusanya jumla ya pointi 42.

Kwa upande wa safu ya mabarobaro wa kiume, Iran iliibuka ya pili baada ya kujikusanyia medali 3 za dhahabu, mbili za fedha na shaba moja wakiwa na jumla ya alama 61, nyuma ya mabingwa Korea Kusini waliozoa medali 7 za dhahabu, mbili za fedha huku wakiwa na pointi 99. Vijana wa kiume wa Kakazkhstan walimaliza katika nafasi ya tatu, wakiwa na pointi 29 baada ya kuzoa meshinda medali moja ya fedha na tatu za shaba. Wakati huohuo, Muirani Azam Dorosti, kocha ya timu ya akina dada ya Iran ametawazwa kuwa mkufunzi bora wa taekwondo barani Asia 2017.
Takriban wanataekwondo 246 kutoka nchi 22 za bara Asia wameshiriki mashindano hayo ya kieneo yanayofahamika kwa Kimombo kama Asian Junior Taekwondo Championships, yaliyofanyika mjini Atyrau, Kazakhstan kuanzia Aprili 19 hadi 21.
Riadha: Mkenya avunja rekodi ya dunia London Marathon
Bingwa mara tatu wa New York City Marathon Mary Keitany sasa ni bingwa mara tatu wa London Marathon na mshikilizi mpya wa rekodi ya dunia wa mbio za kilomita 42 ya wanawake. Mkenya huyo mwenye umri wa miaka 35 atatia kibindoni zaidi ya dola 270,000 za Marekani sawa na Shilingi 27, 556,916 kwa kufuta rekodi ya zaidi ya muongo mmoja ya Muingereza Paula Radcliffe ya saa 2:17:42 na kuweka mpya ya 2:17:01. Keitany, ambaye amechukua uongozi wa mapema wa msimu wa 11 wa Marathon Kuu Duniani (WMM), aliongoza mbio hizo za kilomita 42 kutoka mwanzo hadi utepeni.

Wapinzani wa karibu wa mshindi huyu wa msimu wa tisa wa Marathon Kuu Duniani ni Waethiopia Tirunesh Dibaba na Aselefech Mergia. Mkenya Vivian Cheruiyot alimaliza marathon yake ya kwanza kabisa katika nafasi ya nne.
Vilevile, Keitany alitunikiwa Dola laki 1 na elfu 5 za Marekani sawa na Shilingi 11, 529,916 za Kenya kwa kufuta rekodi ya Radcliffe iliyowekwa katika London Marathon mnamo Aprili 17 mwaka 2005. Keitany alifuta rekodi yake ya Afrika ya saa 2:18:37 aliyoweka Aprili 22 mwaka 2012 katika London Marathon. Naye Daniel Wanjiru aliendeleza umbuji wa Kenya katika London Marathon kwa kushinda taji la wanaume kwa kutumia saa 2:05:48. Mkimbiaji huyu mwenye umri wa miaka 24 alifuata nyayo za bingwa wa mwaka 2014 Wilson Kipsang’ na mshindi wa makala ya 2015 na 2016 Eliud Kipchoge. Wanjiru hakuvunja rekodi yeyote ingawaje ameponegezwa sana kwa kuwa ni mara ya kwanza kushiriki mbio hizi za London Marathon.
Mwanariadha huyu chipukizi amevuna zaidi ya dola 50,000 za Marekani sawa na Shilingi 5,687, 000. Wanjiru amejiweka kileleni mwa Marathon Kuu Duniani baada ya kubwaga magwiji kama bingwa wa Berlin Marathon Kenenisa Bekele na mshindi wa Chicago Marathon Abel Kirui walioridhika katika nafasi za pili na nne, mtawalia. Bedan Karoki alianza maisha ya marathon vyema alipomaliza katika nafasi ya tatu. Mabingwa wa mwaka 2016 Kipchoge na Jemima Sumgong hawakushiriki London Marathon mwaka 2017. Kipchoge, ambaye pia alishinda London Marathon mwaka 2015, hakuingia makala haya ya 37 huku Sumgong akifungiwa nje kwa sababu ya kosa la kutumia dawa za kusisimua misuli. Mwanariadha, Alphonce Felix Simbu wa Tanzania amemaliza nafasi ya tano katika mbio za London Marathon, huku mwenzake Emmanuel Giniki akitwaa medali ya dhahabu katika mbio za Shanghai Marathon zilizofanyika Jumapili. Nyota hao wa Tanzania wamefanikiwa kuweka rekodi katika mashindano hayo makubwa ya riadha duniani pamoja na kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanariadha wa Kenya na Ethiopia. Katika mbio za London Marathon, Simbu alimaliza wa tano akikimbia kwa saa 2:09:10 nafasi sawa na aliyopata kwenye Michezo ya Olimpiki ya Rio 2016. Binafsi anaonekana kuridhishwa na nafasi ile akisisitiza kuwa, wakati umefika wa kunoa makali yake na kujiandaa kwa kwa ajili ya mashindano yajayo ya kimataifa ya riadha. Giniki aling'ara nchini China kwa kumaliza wa kwanza katika mbio za Shanghai Nusu Marathon akitumia saa 01:01:36, huku Mtanzania mwingine, Joseph Panga akimaliza wa sita.
Soka Afrika Mashariki
Marais kutoka mataifa yanayounda Shririkisho la Soka Eneo la Afrika Mashariki na Kati CECAFA, wamekutana jijini Kampala kuzungumzia namna ya kuboresha mchezo wa soka katika ukanda huo. Mkutano huo ulihudhuriwa na marais kutoka mataifa saba ya CECAFA ambao ni pamoja na mwenyeji wao Moses Magogo, Vincent Nzamwita kutoka Rwanda, Jamal Malinzi (Tanzania), Juneidi Tilmo (Ethiopia), Nicolas Mwendwa (Kenya) na Ndikuriyo Reverien (Burundi). Ravia Faina rais wa Shirikisho la soka katika kisiwa cha Zanzibar kilichopewa uanachama wa CAF hivi karibuni, pia alikuwepo. Miongoni mwa mambo yaliyoafikiwa katika mkutano huo ni pamoja na:-Kuibadilisha Katiba ya CECAFA; Kuandaa mkutano mkuu wa CECAFA haraka iwezekanavyo; Kuhakikisha kuwa shirikisho hilo linapata Makao makuu ya kudumu; Kuimarisha michuano ya CECAFA ya vijana chipukizi kwa vijana wasiozidi miaka 15, 17 na 20 kwa wavulana na wasichana pamoj na na soka la ufukweni; Kuimarisha hali ya waamuzi, makocha, uongozi wa soka na kuimarisha afya kwa wachezaji; Kuimarisha mawasiliano na kuitangaza CECAFA; CECAFA kuomba nafasi ya kuandaa michuano ya bara Afrika katika siku zijazo; CECAFA kuwakilishwa ipasavyo katika Kamati kuu ya CAF; Na kuja na mbinu za kuandika mapendekezo kwa Shirikisho la Soka Duniani FIFA ili kufadhili soka la vijana, wanawake na lile la ufukweni.
El-Classico: Barca yaichachafya Madrid
Klabu ya soka ya Barcelona imeisasambua Real Madrid kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Santiago Bernabeu mabao 3-2 katika kipute cha aina yake cha El-Classico, na hivyo kupanda hadi kileleni kwenye msimamo wa La Liga. Ushindi huo unaifanya Barca iwe na pointi 75 sawa na wapinzani wao hao jadi, lakini wakiwa na wastani mzuri wa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Mabao ya Lionel Messi, aliyefunga mara mbili na moja la Ivan Rakitic yalitosha kwa vijana hao wa Luis Enrique kuibuka na ushindi muhimu waliyokuwa wakiuhitaji kufikia alama za Madrid licha ya kwamba wababe hao wa Bernabeu wapo nyuma kwa mechi moja pungufu. Baada ya kuondolewa katika michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya UEFA Champions League, Barcelona walisafiri hadi katika jiji la Madrid kuendeleza harakati zao za kuwania Kombe la LaLiga huku wakiwa wanamkosa mchezaji wao wa kimataifa wa Brazil Neymar kutokana na kutumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu. Licha ya kumkosa Neymar safu ya ushambuliaji ya Barcelona bado ilikuwa imara na kupelekea kupata ushindi huo wa magoli 3-2. Magoli ya Real Madrid yalifungwa na Casemiro dakika ya 28 na James Rodriguez dakika ya 85 akitokea benchi.

Ushindi huo wa Barca unavunja rekodi ya Real Madrid ambao walikuwa wamecheza mechi 22 bila kufungwa katika uwanja Santiago Bernabeu toka February 27 mwaka jana 2016.
Na kutokana na ufinyu wa wakati nikudokeze tu kwamba klabu ya Arsenal imetinga fainali ya Kombe FA baada ya kuichabanga Manchester City mabao 2-1. Fainali ya Kombe la FA itapigwa Mei 27 katika uwanja wa Wembley ambapo Gunners watatoana jasho na The Blues, Chelsea.
……………………………….TAMATI…………………………