Apr 30, 2017 02:27 UTC
  • Jumapili 30

Leo ni Jumapili tarehe tatu Shaban 1438 Hijria, sawa na tarehe 30 Aprili, 2017

Tarehe 10 Ordebehesht kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani sawa na tarehe 30 Aprili, inafahamika kuwa siku ya kitaifa ya Ghuba ya Uajemi. Siku hii iliitwa siku ya kitaifa ya Ghuba ya Uajemi kutokana na baadhi ya pande zenye chuki dhidi ya Iran, kufanya njama za kutaka kupotosha historia, kwa kuiita kwa majina mengine yasiyo na msingi Ghuba ya Uajemi. Jina la kihistoria la Ghuba ya Uajemi limetafsiriwa katika lugha mbalimbali kwa jina hilo au kwa jina la Bahari ya Pars. Inafaa kuashiria hapa kuwa, Ghuba ya Uajemi ni ya tatu kwa ukubwa duniani baada ya Ghuba ya Mexico na Ghuba ya Hudson. Kutokana na kuwa na vyanzo vingi vya utajiri yakiwemo mafuta na gesi, Ghuba ya Uajemi na pwani yake inahesabika kimataifa kuwa sehemu yenye umuhimu mkubwa na wa kistratijia. Kwa kuzingatia utambulisho wa kiutamaduni na kihistoria wa taifa la Iran, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Utamaduni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, liliitangaza siku ya leo ambayo inakumbusha tukio la kuwaondoa Wareno kutoka lango la Hormuz, kuwa siku ya kitaifa ya Ghuba ya Uajemi.

Ghuba ya Uajemi.

Siku kama ya leo miaka 1434 iliyopita, yaani tarehe tatu Shaban 1438 Hijria alizaliwa Imam Hussein (as), mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Kipindi bora cha maisha ya Imamu Hussein (as) kilikuwa cha miaka sita ya kuishi pamoja na babu yake yaani Mtume wa Uislamu. Imamu Hussein alikulia katika familia ambayo ilikuwa na daraja ya juu ya ukamilifu, umaanawi na akhlaqi na hivyo kuweza kupata malezi bora. Kuwa na baba kama vile Imamu Ali Bin Abitwalib (as) na mama kama Bibi Fatwimat Zahraa (as) ambao wote wawili walilelewa na kukulia nyumbani kwa Mtume Muhammad (saw) kulimfanya Imamu Hussein kuweza kufikia hadhi ya juu ya ubora na fadhila. Kadhalika Imamu Hussein alikumbana na mazingira tofauti hatari yaliyoukumba Uislamu. Mtukufu huyo alichukua jukumu la kuuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi kaka yake, yaani Imamu Hassan Bin Ali (as) mwaka 50 Hijiria, na kuuawa shahidi baadaye hapo mwaka 61 Hijiria huko mjini Karbala, Iraq. Kwa mnasaba wa kuzaliwa mjukuu huyu wa Mtume Muhammad (saw) Redio Tehran inatoa mkono wa kheri na fanaka kwa Waislamu wote duniani.

Siku kama ya leo miaka 1378 iliyopita, msafara wa Imamu Hussein (as) mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) ulifika mjini Makkah. Imamu Hussein aliondoka mjini Madina na kuelekea Makkah, baada ya kuhisi hatari iliyokuwa inamkabili hasa kufuatia hatua yake ya kukataa kutoa baia na kutoukubali utawala wa kidhalimu wa Yazid mwana wa Muawiya. Baada ya kuwasili mjini Makkah, Imamu Hussein alipokelewa na hadhira kubwa ya Waislamu wa mji huo ambapo pia alitumia fursa hiyo kufichua dhulma na ukatili wa Bani Umayyah hususan ufisadi na uovu wa Yazidi Bin Muawiyah kwa mahujaji. Kwa utaratibu huo, mjukuu huyo wa Mtume (saw) akawa ameweza kufikisha ujumbe wa Uislamu katika maeneo tofauti ya dunia. Kadhalika akiwa mjini Makkah Imamu Hussein alipata maelfu ya barua za Waislamu wa mjini Kufa, Iraq, ambapo sambamba na wakazi wa Kufa kutangaza kumpinga Yazidi, walimtaka mtukufu huyo kwenda mji huo kwa ajili ya kusimamisha utawala wa Kiislamu. Imamu Hussein alikaa mjini Makkah kwa kipindi cha miezi minne kabla ya kuanza safari yake kuelekea mjini Kufa.

msafara wa Imamu Hussein (as) mjukuu wa Mtume Muhammad (saw)

Siku kama ya leo miaka 240 iliyopita, alizaliwa Carl Friedrich Gauss mwanahisabati na mnajimu mashuhuri wa Kijerumani. Mama yake Gauss ndiye aliyemshawishi mwanawe huyo ajikite zaidi katika somo la hisabati, na hatimaye mtoto huyo akatabahari kwenye fani hiyo. Msomi huyo wa hisabati na mnajimu mashuhuri wa Kijerumani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 78.

Carl Friedrich Gauss

Siku kama ya leo miaka 187 iliyopita, alizaliwa msomi mashuhuri wa ulimwengu wa Kiislamu na mtaalamu wa irfan, Ayatollah Mirza Muhammad Hassan Isfahani, maarufu kwa jina la Safiyyu Alishah. Ayatollah Mirza Muhammad Hassan Bin Muhammad Baqir Isfahani, aliyekuwa mmoja wa wataalamu wa elimu ya kumjua Mwenyezi Mungu (yaani Irfan) wa karne ya 13 Hijiria, alizaliwa mjini Isfahani, Iran. Akiwa kijana mdogo alifanya safari mjini Yazd na kusoma masomo ya msingi mjini hapo kisha akaelekea nchini India na baadaye mjini Makkah. Katika safari hizo alipata kusoma elimu za sheria ya Kiislamu, usulu fiqhi, historia na irfan. Vitabu kama vile ‘Zubdatul-Asrar’ ‘Bahrul-Haqaaiq’ na ‘Tafsirul-Qur’an’ ni kati ya athari za msomi huyo mkubwa. Ayatullah Safiyyu Alishah alifariki dunia mjini Tehran mwaka 1316 Hijiria akiwa na umri wa miaka 65.

Ayatollah Mirza Muhammad Hassan Isfahani, maarufu kwa jina la Safiyyu Alishah

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, sawa na tarehe 30 Aprili mwaka 1945, vilimalizika Vita vya Pili vya Dunia barani Ulaya baada ya kutekwa mji wa Bernin. Siku hiyo vikosi vya Jeshi Jekundu vilingia Berlin kudhibiti mji huo ambao ulikuwa makao makuu ya dikteta wa Ujerumani Adolf Hitler. Baada ya Jeshi Jekundu kukaribia makazi ya Hitler yaliyokuwa chini ya ardhi, dikteta huyo aliamua kujinyonga pamoja na mpenzi wake, Eva Braun. Hitler ni miongoni mwa wanzilishi wa Vita vya Pili vya Dunia ambavyo vilisababisha vifo vya watu milioni 50. Baada ya kutundika maiti za Mussolini na wenzake, Hitler aliingia kwenye makazi yake chini ya ardhi na kufunga ndoa na mpenzi wake wa zaidi ya muongo mmoja Eva Braun, na masaa machache baadaye wote wawili walijinyonga baada ya Jeshi Jekundu kuteka sehemu kubwa ya mji wa Berlin.

Na siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikata uhusiano wake na Misri. Amri ya kukatwa uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Misri ilitolewa na hayati Imam Ruhullah Khomeini baada ya Rais wa wakati huo wa Misri, Anwar Saadat kutia saini makubaliano ya aibu na fedheha ya Camp David na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusaliti malengo ya Wapalestina na ulimwengu wa Kiislamu. Kutiwa saini makubaliano hayo ilikuwa hatua ya kuhalalisha uvamizi wa Wazayuni dhidi ya Palestina na kusaliti haki za Wapalestina waliokuwa wakipambana na utawala haramu wa Israel na vilevile kupuuza maslahi ya Umma wa Kiislamu. Baadaye kiongozi huyo wa Misri alitiwa adabu na shujaa, Khalid Islambuli aliyemmiminia risasi na kumuua kutokana na usaliti huo.

Rais wa wakati huo wa Misri, Anwar Saadat

 

 


 

 

Tags