Jumamosi, Mei 6, 2017
Leo ni Jumamosi tarehe 9 Shaaban 1438 Hijria sawa na tarehe 6 Mei mwaka 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 957 iliyopita sawa na tarehe 9 Shaaban mwaka 481 Hijria, aliaga dunia Ibn Barraj mmoja wa mafaqihi na maulamaa mashuhuri wa Misri. Ibn Barraj alifahamika sana kwa jina la Trablosi kutokana na kuwa, kwa muda fulani alikuwa na cheo cha kadhi katika mji wa Trablos yaani Tripoli huko kaskazini mwa Lebanon ya sasa. Msomi huyo wa Kiislamu alifunzwa na maulamaa kama vile Sayyid Murtadha na Sheikh Tusi. Ibn Barraj ni msomi mtajika wa Kiislamu ambaye fikra na mitazamo yake ilikuwa ikiheshimiwa na mafaqihi wakubwa wa zama hizo. ***
Katika siku kama ya leo miaka 862 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria aliaga dunia Abul Barakaat Abdul Rahman bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Anbari fakihi na mtaalamu mashuhuri wa lugha wa mjini Baghdad. Alihitimu masomo yake katika Chuo cha Nidhamiyyah mjini Baghdad na kutokana na kupata alama za juu mno katika masomo alianza kufundisha katika chuo hicho. Ibn Anbari hakuwa nyuma pia katika uwanja wa uandishi wa vitabu na amevirithisha vizazi vilivyokuja baada yake vitabu vyenye thamani kubwa. ***

Miaka 158 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia mtaalamu wa jiografia na msomi mkubwa wa Kijerumani Alexander Humboldt. Alizaliwa mwaka 1769 huko Berlin, Ujerumani. Alifanya safari ndefu katika mabara ya Asia na Amerika kwa ajili ya kufanya utafiti. Tafiti nyingi za msomi huyo zilihusu namna dunia ilivyoumbwa. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 135 iliyopita, ilitangazwa habari ya kugunduliwa vijidudu maradhi vya ugonjwa wa kifua kikuu. Vijidudu hivyo viligunduliwa na mtaalamu wa Ujerumani, Robert Heinrich Koch. Mtaalamu huyo wa masuala ya baiolojia alikuwa amegundua vijidudu maradhi hivyo ambavyo vimeua zaidi ya watu bilioni moja, wiki mbili kabla. Baadaye Profesa Robert Koch aligundua njia ya kufubaza na kutenga vijidudu maradhi hivyo ambavyo vilikuwa sugu mkabala wa dawa na vilikuwa na uwezo wa kujificha mwilini kwa miaka mingi na kujitokeza wakati mwafaka. Mbali na kugundua vijidudu maradhi vya kifua kikuu, Robert Koch pia aligundua vijidudu maradhi vya kipindupindu katika safari zake katika nchi za Misri na India na mwaka 1906 alitengeneza dawa ya Atoxyl inayoshabihiana na Quinine. Profesa Robert Koch anatambuliwa kuwa mtaalamu mkubwa zaidi wa vijidudu maradhi duniani baada ya Luis Pastore na alitoa huduma kubwa sana kwa elimu na sayansi ambayo kamwe haitasahaulika. ***