May 07, 2017 02:37 UTC
  • Jumapili 7 Mei

Leo ni Jumapili tarehe 10 Sha'aban 1438 Hijria, sawa na tarehe 7 Mei 2017.

Siku kama ya leo miaka 1016 iliyopita alifariki dunia Abu Abdillah Abdul-Baqi, mmoja wa malenga mashuhuri wa karne ya tano Hijiria. Abdillah Abdul-Baqi alikuwa akiishi mjini Baghdad, Iraq ambapo mbali na kusoma elimu ya fasihi kwa wasomi wakubwa, alisomea pia elimu mbalimbali kama vile elimu ya hadithi. Hata hivyo alipendelea sana kusoma mashairi na ameacha athari nyingi katika uga huo.

Abu Abdillah Abdul-Baqi

Siku kama ya leo miaka 684 iliyopita alifariki dunia Majdud-Din Abul-Fawaris, mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu. Alizaliwa nchini Iraq na baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alienda kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kwa ajili ya kukamilisha masomo yake kiasi cha kufikia ukufunzi. Kadhalika Abul-Fawaris alibobea katika fiqhi, usulu fiqhi, hadithi, theolojia, tafsiri na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Ameacha athari nyingi moja wapo ikiwa ni kitabu kinachoitwa 'Kanzul-Faawaaid.'

Majdud-Din Abul-Fawaris

Siku kama ya leo miaka 209 iliyopita, wananchi wa Uhispania walianzisha harakati dhidi ya vikosi vya jeshi la Mfalme Napoleon wa Ufaransa, vilivyokuwa vinakalia kwa mabavu nchi yao. Wakati huo Uhispania ilikuwa ikihesabiwa kuwa mmoja ya wakoloni wakubwa wa Ulaya na ilikuwa ikikalia kwa mabavu ardhi nyingi nje ya bara hilo. Lakini katika kipindi hicho wananchi wa Uhispania walionja uchungu wa nchi yao kukaliwa kwa mabavu na vikosi vya kigeni. Baada ya miaka mitano ya mapambano dhidi ya vikosi vamizi vya Ufaransa, walifanikiwa kuvifukuza vikosi hivyo mwezi Disemba mwaka 1813 kutoka nchini kwao. Wakati huo huo kutokana na kushindwa katika Amerika ya Kusini, Uhispania ililazimika kuziacha huru nchi kadhaa ilizokuwa ikizikoloni.

Uhispania

Siku kama ya leo miaka 205 iliyopita, alizaliwa Robert Browning, malenga na mwanafikra wa nchini Uingereza. Akiwa kijana mdogo Browning alikuwa na maandalizi ya kuwa malenga ambapo alitoa shairi lake la kwanza akiwa na umri wa miaka 12. Taratibu akaanza kupata umashuhuri katika jamii ya Uingereza kama malenga mkubwa. Robert Browning alikuwa akiwasilisha itikadi yake juu ya umoja wa Mungu duniani kupitia mashairi yake. Ameacha athari nyingi katika uwanja huo. Robert Browning alifariki dunia mwaka 1889.

Robert Browning

Na siku kama ya leo miaka 129 iliyopita, mwafaka na tarehe 7 Mei 1888 Miladia, serikali ya kikoloni ya Uingereza ilianzisha uvamizi wake katika ardhi ya Zimbabwe ya sasa. Mipango ya kuikalia kwa mabavu Zimbabwe ilibuniwa na mwanasiasa na mfanyabiashara aliyejulikana kwa jina la Cecile Rhodes, ambaye aliasisi shirika la Afrika Kusini la Kiingereza nchini humo. Kwa kusaidiwa na jeshi la Uingereza, Rhodes aliuwa kwa umati maelfu ya raia wazalendo wa Zimbabwe na kuwakamata mateka wengine wengi, na hivyo kuweza kuidhibiti ardhi yote ya nchi hiyo na kuipachika jina lake la Rhodesia.

Zimbabwe