Jumatano, Mei 17, 2017
Leo ni Jumatano tarehe 20 Shaaban 1438 Hijria mwafaka na tarehe 17 Mei mwaka 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1053 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Ibn Nadim mwanahistoria na mtaalamu wa masuala ya vitabu wa Kiislamu alifariki dunia. Umashuhuri wa mtafiti huyo unatokana zaidi na kitabu chake maarufu cha faharasa. Katika kitabu hicho Ibn Nadim amezitaja takriban elimu zote mashuhuri katika ustaarabu wa Kiislamu na kisha kufafanua maisha na historia ya wanazuoni maarufu katika elimu hizo. Kadhalika Ibn Nadim amevitaja humo vitabu na makala zilizoandikwa kuhusiana na elimu hizo. ***
Katika siku kama ya leo miaka 268 iliyopita alizaliwa nchini Uingereza Edward Jenner tabibu wa Kiingereza aliyegundua chanjo ya ndui yaani (small pox). Baada ya kumaliza masomo ya awali, alijihusisha na taaluma ya tiba. Akiwa na umri wa miaka 21, Edward Jenner alielekea mjini London na kuanza kujihusha na utafiti kuhusiana na ugonjwa wa ndui. Tabibu huyo alifanikiwa kugundua chanjo ya ndui akiwa na umri wa miaka 45 wakati alipoelekea nchini India. Kuanzia hapo ugonjwa huo wa ndui uliweza kutibiwa kwa kutumia chanjo hiyo. Na ilipofika mwaka 1980 maradhi hayo yaliweza kutokomezwa kabisa duniani. ***
Miaka 152 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitiwa saini mkataba wa kwanza wa kimataifa katika uwanja wa mwasiliano huko Paris Ufaransa. Utiaji saini huo ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi 20 duniani. Kwa utaratibu huo kukawa kumepasishwa hati ya kuasisiwa Muungano wa Kimataifa wa Telegrafu. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana siku hii ikapewa jina la Siku ya Kimataifa ya Mawasiliano. Mwaka 1932 kwa mujibu wa maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano wa Madrid Uhispania, jina la Muungano wa Kimataifa wa Telegrafu au Internatioanl Telegraph Union lilibadilishwa na kuwa, Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano au International Telecomunication Union (ITU) na vipengee pamoja na sheria za jumuiya hiyo zikapitiwa upya. Kuanzia mwaka 1947, taasisi hiyo ikawekwa rasmi katika faharasa ya asasi zilizoko chini ya Umoja wa Mataifa. ***
Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, dola la Uingereza ambalo Palestina ilikuwa chini ya mamlaka yake, lilitoa kitabu kwa jina la The White Paper "Kitabu Cheupe" na hivyo kukawa kumepigwa hatua nyingine katika njia ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel. Wapalestina ambao walikuwa wakifahamu vyema himaya ya Uingereza kwa Wazayuni, waliukataa mpango uliokuwa umependekezwa katika kitabu hicho kwa ajili ya kuipatia ufumbuzi kadhia ya Palestina. ***

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, wakati wa vita vya kulazimishwa vya majeshi ya Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ndege za kivita za Iraq ziliishambulia manowari ya kivita ya Marekani iitwayo Stark katika eneo la Ghuba ya Uajemi, na kupelekea wanajeshi 37 wa Marekani kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa. Baada ya tukio hilo, utawala wa Saddam uliomba radhi kwa serikali ya Marekani na kutangaza kuwa tayari kulipa fidia za uharibifu huo. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 8 iliyopita yaani tarehe 27 Ordibehesht 1388 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Ayatuhil Udhma Muhammad Taqi Bahjat Foumani, mmoja wa Marajii Taqlidi na maurafaa wakubwa wa Kishia. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria Shamsia katika mji wa Fouman ulioko katika mkoa wa Gilan kaskazini mwa Iran. Baada ya kupata elimu ya msingi ya kidini, mwaka 1308 Hijria Shamsia alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq. Ayatullah Bahjat alikuwa mashuhuri sana kutokana na uchaji Mungu wake. Kitabus Swalat, Jamiul Masail na Wasilatun Najaat ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya msomi huyo. ***