May 21, 2017 22:06 UTC
  • Jumatatu, Mei 22, 2017

Leo ni Jumatatu mwezi 25 Shaaban 1438 Hijria sawa na tarehe 22 Mei mwaka 2017 Miladia.

Jumatatu ya leo inasadifiana na tarehe Mosi Khordad kwa mwaka wa Kiirani 1396 Hijria Shamsia. Tarehe Mosi Khordad ni siku ya kumkumbuka Ṣadr ad-Dīn Muḥammad Qavami Shīrāzī, maarufu kwa jina la Mulla Sadra. Ṣadr ad-Dīn Muḥammad Shīrāzī ni maarufu pia kwa jina la Sadr al Mutaallihin na alizaliwa mwezi 9 Mfunguo Nane Jamadul Awwal mwaka 980 Hijria mjini Shiraz, Iran. Jiwe la msingi la jengo la kielimu na kimaadili la Mulla Sadra liliwekwa na Sheikh Bahai, alimu ambaye hakuwa na mfano wake katika zama za watawala wa Kisafavi nchini Iran na jengo hilo la kimaanawi lilimalizwa kujengwa na mwanachuoni mkubwa na mhadhiri maarufu, Mirdamad. Mulla Sadra alitabahari na kubobea katika ilimu za Rijal, Fikihi na Usuli na alichota elimu hizo kutoka kwa Sheikh Bahai. Alibobea pia katika elimu za Falsafa, Ilmul Kalam, Irfan n.k, na alichota elimu hizo kutoka kwa mwanachuoni mkubwa Mirdamad. Sadr al Mutaallihin alitabahari pia katika elimu za sayansi ya maumbile, hisabati, falaki na nyota, elimu ambazo alinyweshwa na hakim Abul Qasim Mir Fendereski, mmoja wa maulamaa wakubwa wa zama hizo. Baada ya hapo alianza kufundisha na alikuwa na malaka kubwa katika falsafa na alikuwa na nadharia ya kukubalika katika falsafa. Alianzisha pia madrasa nyingi za Irfan, Falsafa na ilmu nyinginezo za kidini na kutoa mchango mkubwa sana katika falsafa ya Kiislamu. Mwanachuo huyo maarufu amewarithisha watu wa baada yake vitabu zaidi ya 40 ambapo kitabu cha Asfar Arbaá ni maarufu zaidi. Hatimaye mwanachuoni huyo maarufu alifariki dunia mwaka 1050 Hijria baada ya kuishi maisha ya kidini yaliyojaa baraka kwa muda wa miaka 70. Alifariki dunia mjini Basra Iraq na kuzikwa katika mji huo huo.

Mulla Sadra

 

Miaka 132 iliyopita katika siku kama ya leo, mwaka 1885 Milaadia, aliaga dunia Victor Hugo mwandishi na malenga mashuhuri wa Kifaransa akiwa na umri wa miaka 83. Hugo alikuwa muungaji mkono mkuu wa mabadiliko kwa maslahi ya matabaka ya wanyonge na masikini nchini humo. Victor Hugo alijitumbukiza kwenye uwanja wa kisiasa akiwa na umri wa miaka 25 na kufanikiwa kuchaguliwa kuwa mbunge. Lakini ulipofika wakati wa utawala wa Napoleon wa Tatu alilazimishwa kuacha siasa na kubaidishwa kwa muda wa miaka 20 baada ya kupinga siasa za dikteta Napoleon wa Tatu. Umaarufu mkubwa wa Victor Hugo ulitokana na uandishi wake hata inasemekana kuwa yenye ndiye mwanzilishi wa Romanticism, kwani wakati wake namna hiyo ya uandishi ilipata nguvu sana. Miongoni mwa vitabu maarufu vya mwandishi huyo wa Ufaransa ni Les Misérables, The Hunchback of Notre-Dame, The Man Who Laughs na Toilers of the Sea. 

Victor Hugo

 

Na miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe Mosi Khordad 1359 Hijria Shamsia, Marekani ilianza kuiwekea vikwazo vya kiuchumi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Marekani ilipoteza manufaa yake haramu humu nchini, hivyo iliamua kuwashinikiza wananchi Waislamu na wanamapambano wa Iran na pia kujaribu kuilazimisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikubali kufanya mapatano ya kujidhalilisha na Marekani. Baada ya serikali ya Marekani kuchukua uamuzi huo, Imam Khomeini MA mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema kuwa maisha ya kiuchumi ya mataifa ya dunia hayategemei madola ya kibeberu na kuliambia taifa la Iran kwamba: Msiogopeshwe kabisa na vikwazo vya kiuchumi. Kama watatuwekea vikwazo vya kiuchumi, watatupa fursa ya sisi wenyewe kuwa amilifu na kujiimarishia wenyewe uchumi wetu na hilo litakuwa ni kwa manufaa yetu. Watu wanaoogopeshwa na vikwazo vya kiuchumi ni wale wanaoona kuwa uchumi ndio msingi wa kila kitu na dunia ndio mwanzo na mwisho wao.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesimama imara kukabiliana na vikwazo