May 24, 2017 16:51 UTC

Sura ya As-Sajdah, aya ya 7-9 (Darsa ya 739)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’an. Hii ni darsa ya 739 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni aya 32 ya As-Sajdah. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 7 na ya 8 ambazo zinasema:

الَّذِي أَحْسَنَ كُلَّ شَيْءٍ خَلَقَهُ وَبَدَأَ خَلْقَ الْإِنسَانِ مِن طِينٍ

Ambaye ametengeneza vizuri umbo la kila kitu; na akaanzisha uumbaji wa mtu kwa udongo.

ثُمَّ جَعَلَ نَسْلَهُ مِن سُلَالَةٍ مِّن مَّاءٍ مَّهِينٍ

Kisha akajaalia uzao wake utokane na kizazi cha maji madhaifu.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia uumbaji wa mbingu na ardhi pamoja na tadbiri na uendeshaji mambo yake ulioko mikononi mwa Allah SW, ambaye ni Mjuzi na Muelewa wa mambo yote. Aya hizi tulizosoma zinatilia mkazo nukta mbili kuu; ya kwanza ni kwamba kila alichokiumba Mwenyezi Mungu –kuanzia vitu visivyo na roho, mimea, wanyama na watu- vyote hivyo ameviumba katika umbo zuri kabisa na wala hakuna nakisi wala kasoro yoyote katika uumbaji wa Allah. Ama nukta ya pili ni kwamba katika kutaja viumbe vyote, aya hizi zimempambanua mwanadamu na kumzungumzia peke yake kwa sababu Mwenyezi Mungu alimuumba mwanadamu wa mwanzo kutokana na maji na udongo na kukifanya kizazi chake kiendelee kubaki kwa njia ya uzazi kupitia kutunga tone la mbegu ya uzazi ya mwanamme kwenye fuko la uzazi la mwanamke. Inapasa tuashirie hapa kuwa japokuwa mbegu ya uzazi ya mwanadamu inaonekana kwa dhahiri yake kama majimaji hafifu na yasio na thamani lakini kwa mtazamo wa muundo wa seli hai zinazoelea ndani yake, mbegu hizo zina uchangamano tata na makini wa hali ya juu kabisa na ni mojawapo ya ishara za adhama yake Mola na elimu na uwezo wake usio na kikomo.

Nukta nyengine ni kwamba kinyume na nadharia ya Mageuko (Evolution) ya Darwin inayoitakidi kuwa mwanadamu ni kiumbe anayetokana na hatua za mgeuko na mabadiliko tofauti aliyopitia mnyama sokwe, aya hizi zinasema, kwa irada ya Allah mwanadamu wa mwanzo aliumbwa kupitia maji na udongo; na kwa sababu hiyo kuna tofauti baina yake na kizazi chake. Sababu ni kwamba yeye Adam (as) mwenyewe ametokana na udongo, lakini kizazi chake kimetokana na mbegu za uzazi. Hali ya kuwa kwa mtazamo wa nadharia ya Mageuko (Evolution) ya Darwin, mwanadamu wa mwanzo pia ana baba na mama na ameumbwa kutokana na mbegu zao za uzazi.

Si aya hii ya saba pekee ya Suratus-Sajdah, lakini aya nyengine kadhaa za Qur’ani pia zinatilia mkazo nukta hii, kwamba Adam (as) hakuwa na baba na mama. Kwa mfano aya ya 56 ya Suratu Aal Imran inaeleza kwamba uumbwaji wa Isa (as) (wa kutokuwa na baba) ni sawa na uumbwaji wa Adam (as) (ambaye hakutokana na baba na mama) yaani ameumbwa kutokana na udongo.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mfumo uliopo wa ulimwengu ni mfumo bora zaidi kwa sababu umeumbwa kulingana na elimu, hekima na uwezo usio na kikomo wa Mwenyezi Mungu na hakuna hoja yoyote inayoonesha kuwepo ila na kasoro yoyote ndani yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa msanii stadi hasa ni Mwenyezi Mungu, ambaye kutokna na tone duni lenye hali ya majimaji ameumba kiumbe cha kuajabiwa na chenye thamani kubwa, yaani mwanadamu. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kwa kuwa mwanadamu ameumbwa kutokana na maji, udongo na tone dogo la mbegu ya uzazi, hailaiki kwa yeye kuwa na ghururi, kiburi na kujitukuza kwa kujiona bora.

Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 9 ambayo inasema:

ثُمَّ سَوَّاهُ وَنَفَخَ فِيهِ مِن رُّوحِهِ وَجَعَلَ لَكُمُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَالْأَفْئِدَةَ قَلِيلًا مَّا تَشْكُرُونَ

Kisha akamtengeneza, na akampulizia roho yake, na akakujaalieni kusikia na kuona, na nyoyo za kufahamu. Ni uchache mnavyo shukuru.

Aya hii inaashiria hatua baada ya hatua uumbwaji wa Adam pamoja na kizazi chake na kueleza kwamba, Mwenyezi Mungu aliviumba viungo vya mwanadamu kwa mlingano kamili na kumjaalia kiumbe huyo kuwa na kiwiliwili imara. Kisha akampulizia roho mwanadamu ambayo inampambanua na kumtofautisha na viumbe wengine hai. Baada ya udongo alioumbiwa mwanadamu wa mwanzo kuwa na umbo la mtu, kwa irada ya Allah likawa na roho na kuwa na uhai maalumu. Kizazi chake kinachoendelea hadi hii leo, hupata uhai maalumu kinapokuwa katika sura ya jenini ndani ya kipindi cha miezi tisa, wakati tone la mbegu ya uzazi linapoingia kwenye fuko la uzazi.

Inapasa kuzingatia kuwa makusudio ya roho iliyonasibishwa na Mwenyezi Mungu katika aya hii ni hayo maisha maalumu ambayo yeye Mola amewajaalia wanadamu na kuwapambanua na viumbe wengine wenye uhai; na si kwamba kuna kitu maalumu kimetoka kwake yeye Mwenyezi Mungu na kuingizwa kwa mwanadamu. Kwa sababu jambo hilo haliyumkiniki.

Viumbe vingine hai, navyo pia vina macho na masikio, lakini roho aliyojaaliwa kuwa nayo mwanadamu inaufanya uelewa anaokuwa nao kiumbe huyo kupitia hisi hizo uwe wa juu mno kulinganisha na viumbe wengine. Na sababu ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, mbali na kumpa mwanadamu hisi tano zikiwemo za macho na masikio, amempa pia akili na uwezo wa kufahamu, ili kwa msaada wa hayo aweze kuyachanganua na kuyachambua yale anayoyaona na kuyasikia na kugundua kanuni zinazotawala katika ulimwengu wa maumbile. Ni wazi kuwa mwanadamu amezipanga na kuziratibu kanuni hizo kupitia kemia, fizikia, biolojia pamoja na sayansi na elimu nyenginezo; na kwa kutumia elimu hizo, yeye huwa kila mara katika hali ya mabadiliko ya ustawi na upigaji hatua. Hali ya kuwa, hayashuhudiwi mabadiliko yoyote katika mtindo na aina ya maisha ya viumbe wengine hai. Kwa kutoa mfano, sega la asali linalotengezwa na nyuki wa leo na asali yake linayotoa ni sawa kabisa kulinganisha na sega na asali ya nyuki wa miaka elfu moja iliyopita. Aya hii inaashiria nyenzo muhimu zaidi za utambuzi za mwanadamu yaani macho, masikio na akili ambazo baadhi yao zinaonekana kidhahiri na baadhi ya nyengine ni za batini na zisizoonekana. Utambuzi wa mambo ya jarabati unafikiwa kwa kutumia nyenzo za macho na masikio na utambuzi jumla na wa hoja unapatikana kwa njia ya akili.

Bila ya shaka neema hizi kubwa na adhimu za Allah SW zinastahili hamdu na shukurani, lakini kwa masikitiko, akthari ya watu wamemsahau Muumba wao na wala si washukurivu wa neema alizowajaalia. Na hata wale wanaomshukuru Mwenyezi Mungu ushukurivu wao haufikii kiwango cha ihsani na wema usio na kikomo wa yeye Mola kwa waja wake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba miongoni mwa alama za sharafu na utukufu wa kiumbe mwanadamu ni kupuliziwa roho na Allah na kupewa uhai maalumu na Yeye Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa utangulizi wa kuonesha shukurani ni kujitambua mtu nafsi yake na kumtambua Mola wake. Bila ya mtu kujitambua sawasawa yeye mwenyewe hawezi kumjua Mola wake, na bila ya mtu kumjua Mola wake ipasavyo, hatoweza kuwa mshukurivu kwake kwa namna inavyostahiki. Aidha aya hii inatuelimisha kwamba mwanadamu ni kiumbe wa pande mbili. Upande wake mmoja ni wa kimaada na upande wake mwengine ni wa kimaanawi ambao tab’an ndio upande wenye thamani na umuhimu zaidi. Wanadamu wenye hadhi na utukufu wa kiutu wanautumia upande wao wa kimaada kwa faida ya upande wao wa kimaanawi; lakini wanadamu duni na wasio na utukufu wa kiutu wanauacha upande wao wa kimaanawi, na badala yake wanapumbazwa na kushughulishwa na mahitaji yao ya kimaada tu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 739 ya Qur’ani imefika tamati. Tunamwomba Allah atuwezeshe kuwa washukurivu wa neema zake, kubwa na ndogo, za kimaada na za kimaanawi, za dhahiri na za siri, tunazozijua na tusizozijua. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags