May 24, 2017 17:00 UTC

Sura ya As-Sajdah, aya ya 20-25 (Darsa ya 742)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 742 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 32 ya As-Sajdah. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 20 na 21 ambazo zinasema:

وَأَمَّا الَّذِينَ فَسَقُوا فَمَأْوَاهُمُ النَّارُ ۖ كُلَّمَا أَرَادُوا أَن يَخْرُجُوا مِنْهَا أُعِيدُوا فِيهَا وَقِيلَ لَهُمْ ذُوقُوا عَذَابَ النَّارِ الَّذِي كُنتُم بِهِ تُكَذِّبُونَ

Na ama wale walio tenda uovu, basi makaazi yao ni Motoni. Kila wakitaka kutoka humo watarudishwa humo humo. Na wataambiwa: Onjeni adhabu ya Moto ambayo mlikuwa mkiikanusha.

وَلَنُذِيقَنَّهُم مِّنَ الْعَذَابِ الْأَدْنَىٰ دُونَ الْعَذَابِ الْأَكْبَرِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ

Na kwa hakika tutawaonjesha adhabu khafifu kabla ya adhabu kubwa, huenda labda watarejea.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizoeleza kwamba muumini na mtu fasiki hawako sawa mbele ya Allah SW. Kutokana na waumini kufanya amali njema wanastahiki malipo ya Pepo na hiyo itakuwa ndio makaazi yao. Aya tulizosoma zinaendeleza maudhui hiyo kwa kueleza kwamba watu wanaodai kwa ndimi zao tu kuwa wameamini lakini katika matendo hawatii amri za Allah bali muda wote wanafanya maasi, hao watafikwa na adhabu ya Moto na hawatokuwa na njia yoyote ya kuiepuka adhabu hiyo. Lakini hata hapa duniani, watu hao wataadhibiwa kwa namna tofauti ili asaa watubie na kuacha maovu wanayoyafanya na kuepukana na adhabu ya akhera. Lakini wasipotumia fursa hiyo ya duniani, Siku ya Kiyama mlango wa toba utakuwa umefungwa na hakutokuwa na njia ya kurudi tena duniani. Kwa mujibu wa hadithi, baadhi ya masaibu, maradhi na misukosuko mbalimbali inayomfika mtu hapa duniani huwa ni aina fulani ya adhabu ya Allah ya kumtanabahisha na kumkumbusha ili azinduke na kuyaacha maovu na madhambi anayoyafanya. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba baadhi ya wakati mtu hughariki kwenye lindi la ufasiki na madhambi mpaka ikawa kama kwamba haamini kuwepo kwa akhera na Siku ya Kiyama. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa adhabu za Mwenyezi Mungu hazihusiani na akhera tu. Hapa duniani pia Allah huwaonjesha adhabu baadhi ya watu. Na hiyo yenyewe ni neema ili mtu mwovu na mfanya maasi atubie na kurudi kwenye njia iliyonyooka. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba adhabu ya Allah nayo pia inalenga kumjenga na kumlea mja na inatokana na rehma zake Mola.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 22 ambayo inasema:

وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّن ذُكِّرَ بِآيَاتِ رَبِّهِ ثُمَّ أَعْرَضَ عَنْهَا ۚ إِنَّا مِنَ الْمُجْرِمِينَ مُنتَقِمُونَ

Na ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye kumbushwa Aya za Mola wake Mlezi, kisha akazikataa? Hakika Sisi ni Wenye kuwachukulia kisasi wakosefu.

Katika aya hii, Mwenyezi Mungu anawataja wale watu ambao wanayapa mgongo maamrisho yake na kuzikadhibisha aya zake licha ya kuutambua ukweli na haki kuwa ni madhalimu wanaostahili adhabu. Katika misamiati ya Quráni kuidhulumu mtu nafsi yake na kutumbukia kwenye maovu na kufru kunaweza kukawa kubaya zaidi kuliko hata kuwafanyia dhulma wenzake, kwa sababu dhulma hiyo ya mtu kwa nafsi yake ndio chanzo cha kuwadhulumu wengine. Mtu muumini huwa katu hawadhulumu watu, lakini mtu anayeipa mgongo haki na kufadhilisha kufuata njia ya kufru na ukanushaji huweza kirahisi kupuuza haki za wenzake na kuwafanyia dhulma. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba moyo wa ukaidi na inadi humfanya mtu anayekumbushwa ili aache maovu aamue kushupalia matendo yake hayo na kuzama zaidi kwenye lindi la ufasiki na madhambi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa baada ya kuwakumbusha na kuwapa onyo wahalifu, baadhi ya wakati inahitaji pia kuwachukulia hatua kivitendo za kuwatia adabu kwa kuwapa adhabu.

Darsa ya 742 ya Quráni inahatimishwa na aya ya 23, 24 na 25 ambazo zinasema:

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ فَلَا تَكُن فِي مِرْيَةٍ مِّن لِّقَائِهِ ۖ وَجَعَلْنَاهُ هُدًى لِّبَنِي إِسْرَائِيلَ

Hakika tulimpa Musa Kitabu. Basi usiwe na shaka ya kukipokea kwake. Na tukakifanya kuwa ni uwongofu kwa Wana wa Israili. 

وَجَعَلْنَا مِنْهُمْ أَئِمَّةً يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا لَمَّا صَبَرُوا ۖ وَكَانُوا بِآيَاتِنَا يُوقِنُونَ

Na tukawafanya miongoni mwao waongozi wanao ongoza watu kwa amri yetu, walipo subiri na wakawa na yakini na Ishara zetu.

إِنَّ رَبَّكَ هُوَ يَفْصِلُ بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فِيمَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ

Hakika Mola wako Mlezi ndiye atakaye fafanua baina yao Siku ya Kiyama katika waliyo kuwa wakikhitalifiana.

Aya hizi kwanza zinaashiria kubaathiwa na kutumwa Mitume na kuteremshwa vitabu vya mbinguni katika zama zote za historia na kueleza kwamba hakuna shaka yoyote, ni Sisi tuliompa Kitabu Nabii Musa ili awaongoze Bani Israil kuelekea njia ya uongofu na kuwakomboa na unyongeshaji na uonevu wa Firauni. Na katika kaumu ya Bani Israil wako miongoni mwao walioandamana na Musa (as), wakasimama imara na kushikamana na subira katika njia ya kupambana na Firauni. Watu hao walikuwa na yakini na ahadi ya Mwenyezi Mungu na Kitabu chake cha Taurati na hivyo waliweza kuwashinda maadui zao na kuwa viongozi wa jamii yao. Watu wa aina hiyo walikuwa wakiendesha jamii yao kwa mujibu wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na hukumu zake na wakawa wanatekeleza amri za Mola. Waumini hao wa kweli ambao waliweza kushika hatamu za utawala kutokana na imani na istiqama waliyokuwa nayo hawakuwa wakifuata hawaa na matamanio ya nafsi zao wala matashi ya watu wao bali walikuwa wakitii amri ya Allah na msingi wa kazi na utendaji wao ulikuwa ni maamrisho yake Mola. Walitanguliza mbele hukumu za Mwenyezi Mungu badala ya fikra na rai zao, na badala ya kufuata hawaa na matamanio ya nafsi walitawala na kuongoza kwa mujibu wa Kitabu cha Allah na sharia zake. Tab’an kaumu ya Bani Israil ilikuwa na hitilafu mbalimbali zilizowafanya watu wake wafarikiane; na chanzo cha hitilafu hizo kilikuwa ni kujiweka mbali na haki na kufuata matamanio ya nafsi. Kwa sababu hiyo Allah SW anawazungumzia watu hao kwa lugha kali kwa kusema: Kundi la watu hawa wanaosababisha watu kufarakana katika dini wajue kwamba hisabu yao Siku ya Kiyama iko mbele ya Mwenyezi Mungu na Yeye ataamiliana nao kwa msingi wa uadilifu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kubaathiwa na kutumwa Mitume ilikuwa harakati ya kuendelea katika historia. Harakati hiyo ilikuwepo kwa kipindi kirefu kabla ya kubaathiwa na kupewa Utume Bwana Mtume Muhammad SAW; na kwa hivyo haitakiwi iwepo chembe ya shaka juu ya viongozi waliotangulia wa dini za mbinguni. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa imani na istiqama katika njia ya Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa masharti ya lazima ya uongozi. Inalazimu mtu awe na yakini ya lengo analokusudia na kusimama imara hadi dakika ya mwisho ili aweze kuwa na ustahiki unaotakiwa kwa ajili ya kuongoza jamii. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba viongozi wa dini hawapaswi katu kuvunjika moyo katika kazi yao ya kuwaongoza watu katika njia ya uongofu kwa sababu hitilafu ni jambo ambalo limekuwepo siku zote. Wapenzi wasikilizaji darsa yetu ya leo imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwezeshe kufuata kikamilifu maamrisho na hukumu za dini yetu na kuifanya Qur’ani kuwa katiba na mwongozo wa maisha yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags