May 24, 2017 17:04 UTC

Sura ya As-Sajdah, aya ya 26-30 (Darsa ya 743)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 743 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 32 ya As-Sajdah. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 26 ambayo inasema:

أَوَلَمْ يَهْدِ لَهُمْ كَمْ أَهْلَكْنَا مِن قَبْلِهِم مِّنَ الْقُرُونِ يَمْشُونَ فِي مَسَاكِنِهِمْ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ ۖ أَفَلَا يَسْمَعُونَ

Je! Haijawabainikia kwamba kaumu ngapi tuliziangamiza kabla yao, nao wanapita katika maskani zao? Hakika katika hayo zipo Ishara. Basi, je, hawasikii?

Katika darsa iliyopita tulisoma aya iliyozungumzia ahadi ya Allah SW ya kuwalipizia kisasi kwa madhalimu wale waliodhulumiwa. Aya hii ya 26 inawahutubu madhalimu hao kwa kuwauliza: Je haijatosha kwa nyinyi kufuata uongofu kwa mnavyoona na mnavyojua kwamba tumeziangamiza kaumu nyingi zilizopita za wafanya madhambi, na nyinyi mnatembea na kupita kwenye magofu na mabaki ya majengo yao?

Athari zilizobaki za magofu ya kaumu za Adi na Thamudi zilikuwepo katika njia ya baina na Makka na Sham; na watu wa Makka walikuwa wakipita kando ya ardhi hizo zenye mabaki na magofu hayo wakati wa safari zao za kibiashara. Ardhi ambazo kuna siku zilikuwa zikiishi ndani yake kaumu za watu matajiri na wenye nguvu lakini walishukiwa na adhabu na kuangamizwa kutokana na ufisadi, madhambi na dhulma walizokuwa wakifanya. Magofu yaliyobaki ya kaumu hizo utadhani yananadi na kupaza sauti kwa wasafiri wanaopita kando yake kwamba jamani ee, pateni funzo, ibra na mazingatio! Lakini hakuna masikio yanayosikia wala mtu anayejali na kuzingatia wito huo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba badala ya athari za kale zilizobaki kutokana na tamaduni na staarabu zilizopita kuwa mandhari ya kurekodi filamu na kupiga picha ya ukumbusho, zinapasa ziwe mahala pa kupatia funzo, ibra na mazingatio kutokana na hatima zilizowafika wenzetu waliotangulia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa yaliyojiri katika zama zilizopita ni mwenge wa kumulika mustakabali wa wanaofuata, kwa sharti kwamba mtu afumbue masikio na macho yake kutalii matukio ya zama zilizopita na kupata mazingatio na ibra. Aya hii aidha inatuelimisha kwamba, kama tutakuwa na masikio ya kusikia na macho ya kuona tutabaini kuwa magofu na vihame vilivyonyamaa vina ujumbe maalumu vinaotufikishia. Kadhalika tunajifunza kutokana na aya hii kuwa kuna ulazima wa kutunza athari za kale za waliopita ili kuwapa ibra na mazingatio wanaofuata.

Ifuatayo sasa ni aya ya 27 ambayo inasema:

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا نَسُوقُ الْمَاءَ إِلَى الْأَرْضِ الْجُرُزِ فَنُخْرِجُ بِهِ زَرْعًا تَأْكُلُ مِنْهُ أَنْعَامُهُمْ وَأَنفُسُهُمْ ۖ أَفَلَا يُبْصِرُونَ

Je! Hawaoni ya kwamba tunayapeleka maji kwenye ardhi kavu, kisha kwayo tunaitoa mimea wanayo kula wanyama wao na wao wenyewe? Je! Hawaoni?

Katika kuendelea na maudhui ya aya iliyotangulia iliyozungumzia adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa waovu, aya hii inaashiria wema na rehma zisizo na kifani za Mola kwa viumbe wake wote na kueleza kwa kuhoji: Je hamuoni nyinyi jinsi gani Mwenyezi Mungu anayafikisha maji kwenye ardhi kavu, yabisi na zisizo na majani ili kuzirutubisha ardhi hizo na kuzifanya za kijani kibichi na hivyo kuweza kutoa chakula kinachofaa kwa ajili ya maisha ya wanadamu na wanyama? Hakika ya mambo ni kuwa, kutokana na hali ya miinuko na mishuko na kutokuwa tambarare ardhi yote kwa kuwepo milima na mabonde ni jambo lisilowezekana kwa maji ya bahari kuu kufika kwenye maeneo mengi ya sayari ya dunia. Isitoshe, maji ya bahari hayanyweki kwa ukali wa chumvi yake. Kutokana na hayo, Allah SW ameyatatua matatizo yote hayo mawili kwa kujaalia maji hayo kugeuka mvuke kutokana na joto la jua, mvuke ambao hupanda juu angani na kubadilika kuwa mawingu. Na mawingu hayo husukumwa na upepo hadi kwenye ardhi kavu na yabisi, yakageuka tena maji na kudondoka kwa sura ya mvua. Lakini pia, katika mchakato wa kugeuka mvuke, ladha kali ya chumvi ya maji ya bahari hutoweka, na maji safi, matamu na yanayonyweka huwateremkia wakaazi wa sehemu mbalimbali za sayari hii. Hii wapenzi wasikilizaji ni neema kubwa inayoshuhudiwa na watu wote, lakini hawaijali adhama yake; hali ya kuwa mzunguko wa mahesabu maalumu wa maji unaofanyika katika ulimwengu wa maumbile una nafasi kuu na ya msingi katika kuendelea uhai na maisha ya viumbe ardhini. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mazingira ya maumbile ya rutuba na kijani kibichi yaliyowazunguka watu na wanyama ni darasa bora la kujifunza mtu elimu ya kumjua Mwenyezi Mungu; tab'an ikiwa wanafunzi wenyewe wa darasa hilo watakuwa na nia ya kupata elimu na maarifa ya jambo hilo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa harakati na mwendo wa mawingu na kunyesha mvua katika maeneo ya mbali kutoka kwenye bahari na maji makuu si jambo la sadfa na lenye kutokea kwa bahati, bali linafanyika kwa irada yenye hekima ya Muumba wa ulimwengu. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa mfumo wa unyeshaji mvua na uotaji mimea ni moja ya alama na ishara za Mwenyezi Mungu; na haifai kuipita tu kirahisi.

Darsa ya 743 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 28, 29 na 30 ambazo zinasema:

وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَـٰذَا الْفَتْحُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

Na wanasema: Ushindi huu utatokea lini, ikiwa nyinyi mnasema kweli?

قُلْ يَوْمَ الْفَتْحِ لَا يَنفَعُ الَّذِينَ كَفَرُوا إِيمَانُهُمْ وَلَا هُمْ يُنظَرُونَ

Sema: Siku ya Ushindi, wale walio kufuru imani yao haitawafaa kitu, wala wao hawatapewa muhula.

فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ وَانتَظِرْ إِنَّهُم مُّنتَظِرُونَ

Basi wapuuze, nawe ngoja; hakika wao wanangoja.

Aya hizi, na ambazo ni aya za mwisho za Suratus-Sajdah zinaendeleza maudhui ya aya zilizopita na kueleza kuwa: Makafiri na washirikina walikuwa wakimsikia kila mara Bwana Mtume Muhammad SAW akieleza kwamba haki itashinda dhidi ya batili, na hiyo ni ahadi ambayo Allah SW amewaahidi waumini. Kutokana na kusikia hayo, makafiri na washirikina hao wakawa wanamfanyia kejeli na stihzai Bwana Mtume na waumini kwa kuwaambia: Hii ahadi mnayotoa na kusema kuwa Mwenyezi Mungu atalipiza kisasi kwa waovu na kwamba baada ya kutimiza dhima kwao atawaangamiza, itathibiti lini? Na hii adhabu ambayo nyinyi mnaahidi kuwa itatufika sisi papa hapa duniani, itatokea wakati gani? Mwenyezi Mungu Mtukufu akawajibu watu hao kwa kuwaambia: Siku hiyo itafika, lakini msidhani kama wakati huo kuamini kwenu kutakubaliwa na mtapewa muhula na fursa ya kutubia. Siku hiyo hamtopata fursa ya kurudi tena duniani na kwenda kufidia mema ambayo hamkuyafanya. Aya ya mwisho ya sura hii inawaamuru Waislamu kwa kuwaambia jiwekeni mbali na watu wakaidi kama hawa, ambao haki wanaijua lakini wanataka kuifanyia shere na stihzai; na waambieni kwamba: Nyinyi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu atapohukumu baina yetu sisi na nyinyi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba baadhi ya wakati kuuliza suali huwa hakufanyiki kwa nia ya kujua ukweli bali hufanywa kwa madhumuni ya kukejeli na kufanya stihzai. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa imani ya wakati mtu ametingwa na kutanzwa huwa haina thamani kwa sababu inamfanya apoteze irada na asiwe na hiyari. Aya hizi aidha zinatuelimisha kuwa pale mawaidha na utoaji hoja unaposhindwa kuwa na tija inampasa mtu ajitenge na kujiweka mbali na wapotofu. Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo ambayo ndiyo inayohitimisha tarjumi na maelezo ya sura ya 32 ya As-Sajdah imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa wenye kuelimika na kunufaika kivitendo na yale tuliyojifunza katika sura hii. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags