Jumatatu, Mei 29, 2017
Leo ni Jumatatu tarehe 3 Ramadhani 1438 Hijria Qamaria sawa 29 Mei 2017 Miladia.
Katika siku kama ya leo, miaka 1025 iliyopita tarehe 3 Ramadhani mwaka 413 Hijria Qamaria alifariki dunia Muhammad bin Muhammad mwenye lakabu ya Sheikh Mufid, msomi na mwanafaqihi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu katika mji wa Baghdad. Sheikh Mufid alilelewa katika familia ya kielimu, kidini na yenye imani na kisha kujipatia elimu kutoka kwa wanazuoni wakubwa katika zama hizo. Miongoni mwa harakati za kifikra na kiutamaduni za Sheikh Mufid ilikuwa ni kufanya midahalo na mafaqihi na wasomi wa madhehebu mbalimbali. Sheikh Mufid ametuachia vitabu mbalimbali vyenye thamani vikiwemo al Irshaad, al Arkaan na Usuulul Fiqh.
Miaka 871 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Ibn Khashshab mhakiki na mwandishi mashuhuri wa Kiislamu wa karne ya sita Hijria. Alizaliwa mwaka 492 Hijria huko Iraq na kuanza kujifunza masomo ya zama hizo tangu akiwa mdogo. Ibn Kashshab hatua kwa hatua alijifunza masomo ya mantiki, hadithi na uandishi na kuanza kuandika vitabu mbalimbali katika nyanja hizo. Ibn Khashshab alikuwa shakhsiya wa aina yake na ndio maana akafahamika sana kwa jina la Allamah. Aidha alitajwa kama bwana wa maqarii wa zama zake kutokana na umahiri wake katika kusoma na kufahamu vyema Qur'ani Tukufu.

Siku kama ya leo miaka 564 iliyopita sawa na tarehe 29 Mei 1453 ilikombolewa bandari ya Constantine iliyokuwa makao makuu ya ufalme wa Roma ya Mashariki na vikosi vya Sultan Muhammad Fatih, mtawala wa dola la Othmaniya. Amri ya kwanza iliyotolewa na Muhammad Fatih baada ya kuudhibiti mji huo ilikuwa ni kudhaminiwa usalama na uhuru wa wakaazi wake. Mfalme huyo alitoa amri ya kukarabatiwa mji huo na kujengwa msikiti, ambao leo hii unajulikana kwa jina la Msikiti wa Sultan Ahmed. Ilipofika mwaka 1930 mji wa Constantine ulibadilishwa jina na kuitwa Istanbul, na ni miongoni mwa miji muhimu zaidi ya Uturuki ulioko magharibi mwa nchi hiyo.
Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita muwafaka na tarehe 29 Mei 1953, Edmund Hillary mpanda milima kutoka New Zealand na Tenzing Norgay mpanda milima kutoka Nepal walifanikiwa kufika kilele cha Mlima Everest, ambao ni mlima mrefu zaidi duniani. Mlima wa Everest wenye urefu wa mita 8,848, (sawa na futi 29,029) toka usawa wa bahari ni kilele kirefu zaidi katika silsila ya milima ya Himalaya nchini Nepal. Baada ya Hillary na Norgay kufanikiwa kupanda mlima huo mwaka 1953, makundi mengine ya wapanda milima kutoka katika nchi nyingine duniani pia yaliweza kukwea kilele cha mlima huo katika miaka iliyofuata.
Na Miaka 28 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 8 Khordad mwaka 1368 Hijiria Shamsia alifariki dunia Ayatullah Mir Sayyid Ali Fani Isfahani msomi wa Kiislamu. Alizaliwa katika mji wa Isfahan mwaka 1294 Hijira Shamsia na alianza kujifunza elimu ya msingi ya Kiislamu akiwa na miaka 9. Alimu huyo alistafidi na maulama wakubwa na kufikia daraja ya ijtihad ambapo alihamia Najaf nchini Iraq na kwa muda wa miaka 30 alifundisha kwenye mji huo masomo ya fikih, usul, ilmul qalam na akhlaq. Mwaka 1352 Hijria Shamsia alirejea Iran na kuendelea kufundisha mjini Qum. Miongoni mwa vitabu vya Ayatullah Mir Sayyid Ali Fani Isfahani ni Dastur Hajj wal Umrah, Fawaid Rijaliyah, Arubain Hadith na Tafsiri ya Suratul Faatiha.