May 30, 2017 01:48 UTC
  • Jumanne, Mei 30, 2017

Leo ni Jumanne tarehe Nne Ramadhan 1438 Hijria sawa na tarehe 30 Mei, 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 862 iliyopita alifariki dunia Muhammad Bin Muhammad, maarufu kwa jina la Ibn Khorasani, mtaalamu wa nahw, malenga na mwandishi wa Kiislamu. Ibn Khorasani alizaliwa mwaka 494 Hijiria mjini Khorasan, kaskazini mashariki mwa Iran na baadaye kusafiri mjini Baghdad, Iraq kwa ajili ya kutafuta elimu. Akiwa mjini Baghdad, Ibn Khorasani alipata kusoma kwa wasomi wakubwa wa zama hizo hadi kuhitimu masomo hayo. Alikuwa na utaalamu mkubwa katika utunzi na usomaji wa mashairi.

Ibn Khurasan

Siku kama ya leo miaka 830 iliyopita, alifariki dunia Abul-Qasim Hibatullah Bin Jaafar, maarufu kwa lakabu ya Qadhi Said Ibn Sinai-Mulk, malenga na fasihi mkubwa wa nchini Misri. Hibatullah aliyekuwa mashuhuri kwa jina la babu yake yaani ‘Ibn Sinai-Mulk’ alizaliwa mwaka 545 Hijiria katika familia ya Kiislamu mjini Cairo. Alijifunza Qur’ani, nahw, elimu ya hadithi na elimu nyingine ya dini akiwa mdogo huko mjini Alexandria. Alipofikia ujana, tayari alikuwa ameshabobea katika uga wa mashairi na fasihi. Alikuwa akiwapenda watu wa familia ya Mtume ambapo pia alitunga shairi la kuelezea dhulma na ukandamizaji ulioipata familia hiyo ya Bwana Mtume Muhammad (saw) hususan Imam Hussein (as). Ameacha vitabu kadhaa hususan katika uwanja wa mashairi.

Qadhi Said Ibn Sinai-Mulk

Siku kama ya leo miaka 239 iliyopita sawa na tarehe 30 Mei 1778, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 84 Francois - Marie Arouet maarufu kwa jina la Voltaire, mwanafalsafa na mwandishi wa Kifaransa. Katika maisha yake, Voltaire aliwahi kufungwa mahabusu mara mbili na kubaidishwa kwa muda wa miaka mitatu nchini Uingereza. Kitendo hicho kilimkasirisha sana Voltaire na kumfanya kuwa dhidi ya utawala wa Ufaransa.

Francois - Marie Arouet

Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita, sawa na tarehe 30 Mei 1918, yalimalizika mapigano makubwa ya Maren yaliyotokana na Vita vya Kwanza vya Dunia kati ya jeshi la Ujerumani na vikosi vya waitifaki vilivyozijumuisha Marekani, Uingereza na Ufaransa. Vita hivyo vya siku 5 vilijiri katika eneo lililo karibu na Mto Maren ulioko kaskazini mashariki mwa Ufaransa, na majeshi ya Ujerumani yalijipatia ushindi na kuwashikilia mateka wanajeshi elfu 55 wa majeshi ya waitifaki.

Vita vya Maren

Siku kama ya leo 93 miaka iliyopita, alifariki dunia Ali Akbar Khan Nafisi aliyejulikana kama Naadhimul Atwiba, daktari na mtaalamu wa lugha wa Kiirani, katika mji wa Tehran. Baada ya kumaliza masomo yake ya mwanzo alianza kujifunza masomo ya kidini na pia udaktari katika chuo cha Darul Funun cha Tehran. Baadhi ya vitabu vilivyoandikwa na Naadhimul Atwiba katika uwanja wa tiba vimetarjumiwa katika lugha za kigeni. Ali Akbar Khan Nafisi ambaye pia alikuwa mtaalamu wa lugha alifanya jitihada nyingi katika kukusanya maneno ya lugha ya Kifarsi na kuandika kamusi inayoitwa 'Kamusi ya Nafisi.'

Ali Akbar Khan Nafisi

Siku kama ya leo miaka 87 iliyopita, alifariki dunia Sayyid Ahmad Peshawar, maarufu kwa jina la Fasihi wa Peshawar, malenga, fasihi na msomi mkubwa wa mjini Tehran. Alizaliwa katika viunga vya mji wa Peshawar nchini Pakistan. Alianza kusoma elimu ya dini kwa maulama wakubwa kama vile Mula Hadi Sabzavari katika mji wa Ghazni nchini Afghanistan na kisha, Khorasan, Iran na baadaye mjini Sabzevar, kaskazini mashariki mwa Iran. Baadaye alielekea mjini Tehran na kuanza kutalii vitabu vya falsafa na mashairi na kutokea kuwa hodari katika kusoma mashairi, fasihi, na elimu nyingine. Pia alijulikana kwa uchaji Mungu na imani.

Sayyid Ahmad Peshawar