Jumatano, 31 Mei, 2017
Leo ni Jumatano tarehe tano Ramadhani 1438 Hijiria, sawa na tarehe 31 Mei, 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1488 iliyopita, sawa na tarehe 31 Mei 529, dini ya Ukristo ilitambuliwa rasmi huko Roma kwa amri ya Constantine, mfalme wa wakati huo wa Roma. Kabla ya hapo Wakristo walikuwa wakifanya ibada kwa siri huko Roma. Mwaka 324 Miladia Mfalme Constantine aliamua kuamia mji wa Byzantine, mji ambao alikuwa ameutangaza kama mji mkuu wa ufalme wake na uliojengwa na Wagiriki yapata karne nane kabla ya kuzaliwa Nabii Isa (as). Miaka sita baadaye na baada ya kuhamia huko mfalme huyo, ndipo dini ya Ukristo ikatangazwa na kutambuliwa rasmi huku wafuasi wake wakiruhusiwa kuabudu kwa uhuru.

Siku kama ya leo miaka 792 iliyopita, alifariki dunia Afdhulud-Din Abu Abdillah Twabib Khunji, mtoto wa Abdul-Malik Khunji, mmoja wa wasomi wa karne ya saba Hijiria. Alizaliwa mwaka 590 Hijiria katika mji wa Khunji, ambao ni miongoni mwa viunga vya mji wa Khalkhal, kaskazini magharibi mwa Iran na kuanza kusoma elimu ya msingi. Alikuwa tabibu na mtaalamu wa elimu ya mantiki huku akiwa hodari katika elimu nyingine za dini pia kama vile fiqhi na hadithi. Kitabu cha 'Kashful-Asraar na Ghawaamidhil-Afkaar fil-Mantwiq' ni kati ya athari za msomi huyo wa Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 208 iliyopita, alifariki dunia Joseph Haydn, mwalimu na mtungaji muziki wa nchini Austria. Akiwa na kipawa kikubwa aliweza kupata umashuhuri katika kutunga nyimbo. Mwaka 1781 Joseph Haydn alipata kujuana na kuanzisha urafiki na mwanamuziki na mtungaji mwingine mashuhuri wa muziki wa zama hizo Wolfgang Amadeus Mozart wa hukohuko Austria, jambo ambalo baadaye lilikuwa na taathira kubwa kwake katika utunzi wa muziki. Ameacha athari mbalimbali katika uga wa utunzi wa muziki.

Siku kama ya leo miaka 202 iliyopita alizaliwa Haji Mulla Ali Alyari Tabrizi, mmoja wa maulama wakubwa wa nchini Iran huko mjini Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran. Alibobea katika elimu za hadithi, fiqhi, mashairi na fasihi. Kadhalika Alyari Tabrizi alikuwa na ufahamu na elimu za falsafa, hesabati na nyota. Baada ya kujiunga na hawza ya mjini Najaf, Iraq alipata kusoma kwa maulama wakubwa za zama zake kama vile Murtadha Answari na Mirza Shirazi ambapo alitokea kuwa msomi mkubwa katika uga wa fiqhi na usulu fiqhi. Baada ya kurejea Iran alijikita katika shughuli ya ukufunzi na kuwalea wanafunzi. Moja ya athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu kinachoitwa, 'Dalailul-Ahkam fi Sharhi Sharaaiul-Islami.'

Siku kama ya leo miaka 185 iliyopita alifariki dunia Évariste Galois, mwanahisabati mwenye kipawa cha juu wa Ufaransa. Alizaliwa tarehe 26 Oktoba mwaka 1811 Miladia karibu na jiji la Ufaransa. Hadi anafikia umri wa miaka 12 hakuwa na mwalimu mwingine ghairi ya mama yake na kutokana na kipawa cha hali ya juu cha elimu akaanza kusoma vitabu mbalimbali vya kihistoria na hivyo kuinukia kielimu. Baada ya hapo alijiunga na chuo, ambapo alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani katika kila somo. Baadaye Évariste Galois alianza kutalii elimu ya hisabati. Akiwa na umri wa miaka 18 alikamilisha kazi ya uandishi wa kitabu cha Ukweli wa Hisabati na baada ya hapo akaandika vitabu vitatu vipya katika taaluma hiyo na kujipatia umashuhuri mkubwa. Galois aliuawa akiwa na umri wa miaka 21 sawa na tarehe kama ya leo mwaka 1832 Miladia, baada ya kutiwa jela wakati wa harakati zake za kisiasa nchini Ufaransa. Weledi wanaamini kuwa, kama Galois hangeuawa mapema, basi angepiga hatua kubwa katika uga wa hisabati duniani.

Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 31 Mei 1910, nchi ya Afrika Kusini iliyokoloniwa na wakoloni wawili huko kusini mwa Afrika ilijipatia uhuru wa ndani. Afrika Kusini ilivumbuliwa mwaka 1488, na katikati ya karne ya 17 nchi hiyo ilikoloniwa na Uholanzi, na karne mbili baadaye ikakoloniwa na Uingereza. Mnamo mwaka 1910 Uingereza ilikubali kuundwa Muungano wa Afrika Kusini na ilipofika mwaka 1931 muungano huo ulifanikiwa kujipatia uhuru kamili. Mfumo wa Afrika Kusini ulibadilishwa na kuwa Jamhuri mwaka 1961. Mapambano na harakati za ukombozi za weusi walio wengi zikiongozwa na chama cha African National Congress ANC zilipelekea kufikia mwaka 1991 nchi hiyo kujipatia uhuru na kuutokomeza kabisa utawala wa kibaguzi. Afrika Kusini yenye ukubwa wa kilomita mraba milioni moja na laki mbili inapakana na nchi za Msumbiji, Zimbabwe, Botswana, Namibia, Lesotho na Swaziland.

Siku kama ya leo miaka 7 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 31 Mei 2010, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walishambulia msafara wa meli zilizosheheni misaada ya kibinadamu kwa ajili ya wananchi wa Ukanda wa Ghaza waliozingirwa na utawala huo. Shambulio hilo lilipelekea watu 9 kuuawa na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa. Msafara huo uliokuwa na wanaharakati 663 kutoka nchi 37 duniani, ulikuwa umebeba shehena ya misaada ya dawa na chakula kwa ajili ya wananchi wa Ukanda wa Ghaza wanaokabiliwa na mzingiro wa kidhulma wa Wazayuni. Shambulio hilo la kinyama lililaaniwa vikali na mataifa mbalimbali duniani, na hatimaye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likatoa azimio la kufanyika uchunguzi wa haraka na usiopendelea upande wowote kwa lengo la kubaini na kuwekwa wazi wahusika wa jinai hizo.
