May 31, 2017 23:39 UTC
  • Alkhamisi, Juni Mosi, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 6 Ramadhani mwaka 1438 Hijria inayosadifiana na tarehe Mosi Juni mwaka 2017.

Siku kama ya leo miaka 975 iliyopita, yaani tarehe 6 Ramadhani mwaka 463 Hijria Qamaria, alifariki dunia Hamza Bin Abdul Aziz Daylami, ambaye pia alifahamika kwa jina la Sallar, mwanachuoni mkubwa wa karne ya 5 Hijria Qamaria katika mji wa Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran. Ni mzaliwa wa eneo hilohilo la kaskazini mwa Iran na alifahamika kwa lakabu ya Abu Ali. Miongoni mwa kazi muhimu za msomi huyo wa Kiirani ni vitabu vilivyokuwa na anwani za "Al-Marasimul Alawiyya wal Ahkaamu Nabawiyyah" na mkusanyiko wa vitabu kumi alioupa jina la "Jawamiul Fiqhi". Vitabu vingine vilivyochapishwa vya mwanachuoni huyo ni pamoja na "Al-Abwaabu wal Fusul", na "Taqrib" vilivyojadili masuala ya fiqhi.

Kaburi la Sallar Daylami

Siku kama ya leo miaka 975 iliyopita, yaani tarehe 6 Ramadhani mwaka 463 Hijria Qamaria, aliaga dunia Abu Ya'ala Jaafari, mmoja wa wanazuoni wakubwa wa karne ya 5 Hijria. Alikuwa mwanathiolojia na faqihi mkubwa, ambapo alichukua nafasi ya enzi za Sheikh Mufid. Abu Yaala Jaafari alijifunza elimu ya fiqhi na masomo mengine ya sayansi kutoka kwa Sheikh Tuusi, mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu. "Milaadu Swahibu Zaman" na "Takmilah" ni miongoni mwa athari muhimu zilizoachwa na mwanachuoni huyo.

Abu Yaala Jaafari

Miaka 31 iliyopita, yaani tarehe Mosi Juni mwaka 1986 Miladia, wanafunzi kadhaa wa shule za msingi waliwaandikia barua wenzao duniani kote na kuwataka kupitisha muda wao wa siku nzima kwa ajili ya amani. Sehemu moja ya barua ya wanafunzi hao inasomeka kama ifuatavyo: "Wazazi wetu wana imani thabiti na kutupenda, kwa kuwa sisi ni watoto wao. Hata hivyo je, mnafahamu ni dunia ya aina gani waliyotuandalia? Sisi kamwe tusingekuwa na fursa ya kukua, iwapo wazazi wetu wangefanya kosa japo dogo tu. Tunahitaji suhula kwa ajili ya kukua na malezi." Kwa mnasaba huo, siku ya kwanza ya mwezi Juni kila mwaka, imepewa jina la "Siku ya Watoto Duniani". Kwa ajili hiyo marasimu maalumu hufanyika katika pembe mbalimbali za dunia katika kuadhimisha siku hiyo.

Siku ya Watoto Duniani

Na miaka 94 iliyopita muwafaka na siku kama ya leo, moja kati ya zilzala kubwa zilizouwa watu wengi duniani, iliikumba Tokyo mji mkuu wa Japan. Zilzala hiyo ilitokea nyakati mbili tofauti kwa kupishana muda mfupi. Mtetemeko huo wa ardhi uliharibu nusu ya mji wa Tokyo na kuuwa watu zaidi ya laki moja na elfu hamsini mjini humo.