Jun 02, 2017 02:24 UTC
  • Ijumaa, Juni Pili, 2017

Leo ni Ijumaa tarehe 7 Ramadhani, mwaka 1438 Hijria inayosadifiana na tarehe Pili Juni, 2017 Miladia.

Miaka 1431 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 7 Ramadhan mwaka wa 10 tangu kubaathiwa na kupewa Utume Nabii Muhammad SAW, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, aliaga dunia Abu Talib, ami na mtetezi mkubwa wa Mtume SAW katika mji wa Makka. Baada ya kufariki Abdul Muttalib, babu mtukufu wa Nabii Muhammad SAW, Abu Talib ndiye aliyebeba jukumu la kumlea Mtume, na akawa bega kwa bega na mwana huyo wa nduguye katika hali zote. Baada ya kupewa Utume Nabii Muhammad SAW, Abu Talib hakumwacha mkono mtukufu huyo na akasimama imara kukabiliana na washirikina wa kikureishi. Lakini baada ya kufariki dunia Abu Talib washirikina walishadidisha maudhi na manyanyaso dhidi ya Bwana Mtume SAW, kiasi kwamba kutokana na hali ngumu mno iliyomkabili, hatimaye kwa amri ya Mwenyezi Mungu, mtukufu huyo alihajiri kwa kuhama Makka na kuhamia Madina ambako aliasisi utawala wa kwanza wa Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 135 iliyopita, yaani tarehe Pili Juni mwaka 1882 alifariki dunia Giuseppe Garibaldi, kamanda mzalendo na kiongozi wa vita vya umoja wa Italia. Katika kipindi cha ujana wake Garibaldi alijishughulisha na kazi mbalimbali, ambapo baadaye alijiunga na jeshi. Hatimaye Giuseppe Garibaldi alifanikiwa kuwa kamanda wa wapigania uhuru wa Italia. Garibaldi alifanya juhudi kubwa za kuijenga Italia moja; na kwa sababu hiyo akajulikana katika historia ya nchi hiyo kama shujaa wa taifa.

Giuseppe Garibaldi

Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 12 Khordad mwaka 1379 Hijiria Shamsia, aliaga dunia Hujjatul Islam Seyyid Ali Akbar Abuturabi, mwanazuoni mwenye mwamko na mwanaharakati wa Iran katika ajali ya gari akiwa na baba yake Ayatullah Seyyid Abbas Abuturabi. Hujjatul Islam Seyyid Ali Akbar Abuturabi alizaliwa mwaka 1318 Hijiria Shamsia sawa na mwaka 1940 Milaadia, katika mji wa kidini wa Qum hapa nchini Iran. Alijifunza elimu ya dini kwa maulamaa wakubwa akiwemo Imam Khomeini (MA). Kwa mara kadhaa msomi huyo alikamatwa na kuteswa na maajenti wa Shah wakati wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu. Aidha katika vita vya Iran na Iraq mwaka 1359 Hijiria Shamsia sawa na mwaka 1981 Milaadia, alikamatwa mateka na askari wa utawala wa Baath wa Iraq na kufungwa kwa miaka 10 katika jela zenye mateso makali za Iraq. Lakini alivumilia kiasi cha kuwa mashuhuri miongoni mwa mateka wa Iran kwenye jela hizo. Alipoachiliwa huru aliteuliwa kuwa mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya mateka na walioachiliwa huru.

Hujjatul Islam Seyyid Ali Akbar Abuturabi

Na siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, mnamo tarehe Pili Juni mwaka 1942 wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, Mjerumani Marshal Erwin Rommel maarufu kwa jina la Mbwa Mwitu wa Jangwani, alianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya jeshi la Uingereza katika maeneo ya kaskazini mwa Afrika. Kabla ya mashambulizi hayo, Waingereza walikuwa wamefanya hujuma nchini Libya na kuitwaa nchi hiyo kutoka mikononi mwa jeshi la Wajerumani wa Kinazi. Hata hivyo mashambulizi ya jeshi la Erwin Rommel ambayo yalidumu kwa kipindi cha mwezi mmoja yaliwawezesha wanajeshi wake kuidhibiti tena Libya na eneo la al Alamein lililoko kaskazini mwa Misri na karibu na bandari muhimu ya Alexandria. Wajerumani walikaribia kuutwaa mfereji wa kistratijia wa Suez lakini mwezi Novemba mwaka 1942 Waingereza wakafanya mashambulizi makubwa dhidi ya jeshi la Erwin Rommel na hatimaye kulishinda.

Marshal Erwin Rommel