Jumatatu, Juni 5, 2017
Leo ni Jumatatu tarehe 10 Ramadhani, mwaka 1438 Hijria inayosadifiana na tarehe 5 Juni, 2017 Miladia.
Miaka 1441 iliyopita katika siku kama ya leo, tarehe 10 Ramadhani mwaka wa tatu kabla ya hijra, aliaga dunia katika mji wa Makka, Bibi Khadija (as), mke mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Bibi Khadija (as), ambaye alikuwa mmoja wa wanawake matajiri na watajika wa Kikureishi alifunga ndoa na Bwana Mtume SAW miaka 15 kabla ya mtukufu huyo kubaathiwa na kupewa Utume. Bibi huyo mtukufu alikuwa mtu wa mwanzo aliyeuamini Utume wa Nabii Muhammad SAW na akajitolea nafsi yake na mali na utajiri wake wote kuihami dini tukufu ya Uislamu. Kuwepo kwa Bibi Khadija kulikuwa na umuhimu mkubwa kwa Bwana Mtume, kiasi kwamba Mtukufu huyo alikuelezea kufariki dunia kwa Bibi Khadija kuwa ni msiba mkubwa mno, hata akaupa mwaka wa kufariki kwake na ambao alifariki pia msaidizi wake mwengine mkubwa, yaani Ami yake Abu Talib kuwa ni "Mwaka wa Huzuni". Baada ya kufariki dunia Bibi Kahdija (as), Bwana Mtume Muhammad SAW alikuwa kila mara akimtaja kwa wema. Miongoni mwa aliyoyasema kuhusu Mama huyo mtukufu wa Waumini ni kwamba: "Wallahi Mwenyezi Mungu hajanipa aliye mbora kuliko Khadija. Aliniamini wakati watu walipokuwa wakikanusha na akanisadikisha wakati watu walipokuwa wakinikadhibisha".

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, wananchi Waislamu wa Iran baada ya kupata habari kwamba Imam Khomeini (MA) alikuwa amekamatwa na utawala dhalimu wa Shah, walifanya maandamano makubwa kote nchini dhidi ya utawala huo. Siku kadhaa kabla yake, Imam Khomeini alikuwa ametoa hotuba kali katika Chuo cha Kidini cha Faidhiyya akifichua maovu yaliyokuwa yakifanywa na utawala wa Shah, jambo ambalo liliuchukiza sana utawala huo na kuamua kumtia nguvuni. Suala hilo liliwakasirisha sana wananchi wa Iran ambao waliamua kufanya maandamano ya kushinikiza kuachiliwa kwake mara moja. Ili kukabiliana na wimbi la malalamiko hayo, utawala wa Shah uliamua kuwashambulia waandamanaji ambapo uliua na kuwajeruhi wengi kati yao. Harakati hiyo ya mapambano ambayo inafahamika humu nchini kama Mapambano ya Tarehe 15 Khordad, kwa hakika ulikuwa mwanzo wa mapambano ya Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi shupavu wa Iran dhidi ya utawala wa kitaghuti wa Shah, mapambano ambayo yaliainisha mustakbali wa kisiasa na kijamii wa Iran. Mapambano hayo yaliendelea kwa uongozi shupavu wa Imam Khomeini hadi Mapinduzi ya Kiislamu yalipofikia ushindi mwaka 1979.

Miaka 13 iliyopita Ronald Reagan, rais wa zamani wa Marekani aliaga dunia kutokana na ugonjwa wa kusahau wa Alzheimer. Alizaliwa mwaka 1911 na kuhitimu masomo yake ya juu katika taaluma ya uchumi na masuala ya kijamii. Reagan alianza kufanya kazi kwenye redio na kisha akawa msanii kwenye televisheni. Taratibu alianza kujishughulisha na masuala ya siasa ambapo kwanza alikuwa mwanachama wa chama cha Democrats na kisha kujiunga na chama cha Republicans. Mwaka 1970 aliteuliwa na chama hicho kuwa gavana wa California na kisha mwaka 1980 akafanikiwa kuwa rais wa Marekani baada ya kumshinda mpinzani wake Jimmy Carter. Katika kipindi cha uongozi wake wa miaka minane Reagan alitekeleza siasa za kijeshi na kichokozi dhidi ya nchi nyingine za dunia. Alianzisha mpango wa kijeshi wa Star Wars na kutoa amri ya kufanyika mashambulio ya kijeshi dhidi ya baadhi ya nchi. Pia alichochea na kuunga mkono kijeshi, kifedha, kipropaganda na kisiasa uvamizi wa utawala wa kidekteta wa Saddam Hussein wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, vita vya tatu vikuu kati ya utawala ghasibu wa Israel na nchi za Kiarabu vilianza. Katika uvamizi wa kushtukiza na wa ghafla, ndege za kivita za Israel ziliingia katika anga ya nchi za Misri, Syria na Jordan na kushambulia kwa muda wa masaa mawili mfululizo majeshi na taasisi za anga za nchi hizo na kukaribia kuvitokomeza kabisa. Baada ya hapo jeshi la nchi kavu la Israel lililokuwa likiungwa mkono na Marekani pamoja na Uingereza, kwa muda wa siku sita, lilivamia kwa silaha nzitonzito na za kisasa majeshi ya nchi hizo tatu za Kiarabu na kuyashinda kikamilifu.

Na siku kama ya leo miaka 234 iliyopita baluni lilirushwa angani kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya jitihada za mwanadamu za kutaka kupaa angani. Baluni hilo lilikuwa na watu wawili, mmoja wao akiwa ni mwanafizikia wa Kifaransa aliyejulikana kwa jina la Jean-Francois Pilatre de Rozier. Tangu alipokuwa shuleni de Rozier alikuwa akifikiria jinsi ya kutengeneza chombo cha kupaa angani na hatimaye baada ya ndugu wawili Montgolfier kutengeneza baluni, naye pia alitengeneza baluni lake na akapaa angani nalo katika siku kama hii ya leo. Mwanafizikia huyo alianguka chini na kufariki dunia katika moja ya safari zake za uhakiki angani.