Leo Katika Historia
Leo ni Jumatano tarehe 12 Ramadhani mwaka 1438 Hijria, sawa na 7 Juni mwaka 2017 Miladia.
Siku kama ya leo yaani tarehe 12 Ramadhani kwa mujibu wa wapokezi wengi wa kalenda ya Hijria Qamaria, ni siku ambayo Nabii Issa Ibn Maryam, Masih AS aliteremshiwa kitabu kitukufu cha Injili. Neno Injili ni la Kigiriki na lina maana ya bishara. Jina hilo limetajwa mara 12 katika Qur’ani Tukufu na kitabu hicho kinaitambua Injili kuwa ni kitabu cha Mwenyezi Mungu SW chenye sheria na kanuni za mbinginu. Hata hivyo kitabu kinachojulikana hivi sasa kwa jina la Injili si kile kilichoteremshwa kwa Nabii Issa Masih bali ni riwaya na kumbukumbu zilizokusanywa na wanafunzi wake baada ya Yeye kupaa mbinguni.
Siku kama ya leo miaka 1437 iliyopita yaani tarehe 12 Ramadhani mwaka wa kwanza Hijria, muda mfupi baada ya Mtume Mtukufu Muhammad (SAW) kuhama Makka na kuelekea Madina, aliunga udugu baina ya Muhajirina na Ansar. Muhajirina ni watu ambao walihama na Mtume (SAW) kutoka Makka kwenda Madina, na Ansar ni Waislamu wa mjini Madina waliowakaribisha Muhajirina katika mji huo. Kwenye sherehe hiyo ya kuunga udugu bina ya Waislamu, Mtume (SAW) alimtangaza Ali bin Abi Talib (AS) kuwa ndugu yake hapa duniani na Akhera.
Tarehe 12 Ramadhani miaka 840 iliyopita, alifariki dunia Ibn Jawzi, faqihi na mtaalamu mkubwa wa hadithi katika karne ya 6 Hijria. Ibn Jawzi alizaliwa mwaka 510 Hijria na kufanya safari nyingi kwa ajili ya masomo. Mbali na kubobea katika masuala ya elimu ya fiq'hi na hadithi, alikuwa mtaalamu katika uwanja wa kutoa mawaidha na hata akaweza kuaminiwa na maulamaa wakubwa wa zama zake. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi na mashuhuri zaidi ni Al Muntadhim na Mawaidhul Muluk.

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Juni 1980, ndege za kijeshi za utawala wa Kizayuni wa Israel zilishambulia na kukiharibu kituo cha nyuklia cha Tamouz kilichoko karibu na Baghdad, mji mkuu wa Iraq. Licha ya kuharibiwa kikamilifu kituo hicho cha nyuklia, na kusababisha fikra za waliowengi duniani kuchukizwa na kulaaniwa kitendo hicho na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, amma hakuna hatua zozote za kivitendo zilizochukuliwa dhidi ya utawala wa Israel. Hivi sasa utawala huo ghasibu unamiliki zaidi ya vichwa 200 vya makombora ya nyuklia, na umekuwa ukikataa kuwaruhusu wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuikagua mitambo na vinu vyake vya nyuklia.
Siku kama hii ya leo miaka 138 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Juni 1879 vilianza vita vilivyochukua muda wa miaka mitano kati ya nchi za Peru, Chile na Bolivia. Vita hivyo vilianza baada ya serikali ya Bolivia kutiliana saini na shirika moja la Chile na kisha kukiuka makubaliano ya mkataba huo, na kusababisha Chile kuishambulia kijeshi Bolivia. Hatimaye Chile ilijipatia ushindi kwenye vita hivyo, na kutiliana saini makubaliano mapya na nchi za Bolivia na Peru, ambapo kwa mujibu wa makubaliano hayo, ufukwe wote wa Bolivia na sehemu ndogo ya ardhi ya Peru ilichukuliwa na Chile.
Na Siku kama hii ya leo miaka 169 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Juni mwaka 1848 alizaliwa Paul Gauguin, mchoraji mashuhuri wa Kifaransa. Gauguin alizaliwa Ufaransa na kisha kumuoa mwalimu aliyekuwa mahiri katika fani ya uchoraji, hatua ambyo ilimfanya Gauguin kuvutiwa na sanaa hiyo iliyomuwezesha kuacha athari za sanaa ya uchoraji katika kisiwa cha Tahiti, kilichoko kusini mwa Bahari ya Pacific. Gauguin aliishi kwenye kisiwa hicho hadi mwisho wa umri wake mwaka 1903, kwa kuchora picha zinazoakisi mandhari mbalimbali.